Habari za Punde

Watoto wanaoishi kwenye nyumba za maendeleo waaswa kuacha kupururuka

Na Haji Nassor, Pemba

WAZAZI wenye watoto wanaoishi kwenye nyumba za maendeleo kisiwani Pemba, wametakiwa kuwaangalifu na kuwapiga marufuku watoto wao kuacha mtindo wa kupururuka kwa kutumia makalio, wanaposhuka ngazi za nyumba hizo.

Watoto hao wamebainika kupururuka kuanzia hata ngazi ya nne wanaposhuka chini na wakati mwengine wakiwa zaidi ya watatu jambo ambalo linaweza kusababisha maafa pindi wakianguka.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti majirani wa nyumba hizo, wamesema imekuwa ni mtindo kwa watoto wanaoishi nyumba hizo kujihatarishia maisha yao.

Amina Khamis Makame wa Mtemani Wete, alisema mtendo huo zaidi hufanywa kati za usiku au kwa siku za mapunziko wanapokua hawakwenda chuoni au skuli.

“Hupururuka kwa kutumia makalio yao kutoka ngazi ya nne hadi ya chini, na wakati mwengine huwa zaidi ya watatu, ni hatari maana akikosa mtelezo anaweza kuanguka’’,alifafanua.

Nae Mwanahija Kombo Omari wa eneo hilo, alisema lazima wazazi wa watoto hao, wajiwekee mikakati ya kuwazuia watoto hao kabla halijatokeza kubwa.

Kwa upande wake Said Khamis Juma wa Madungu Chakechake, alilizishauri kamati za sheha kuwaita wakaazi wa nyumba hizo ili kuwapa habari za watoto wao.

Mwadini Ali Mchama ‘bamcha’ alisema imekuwa ni kwaida hata kwa watoto wasioishi nyumba hizo za maendeleo kufanya mchezo wa kuteleza kwenye mgomgo wa ngazi 
hizo.

Mmoja wa wazazi wanaoishi kwenye nyumba hizo za maendelo za Madungu aliejitambulisha kwa jina moja la Salum, alisema imekuwa vigumu kuwazuia watoto wa familia nyengine.

“Mwandishi miaka hii kila mmoja analea mwanawe, wangu hawaingia kwenye mchezo, huu lakini wa wenzangu wasiokatazika wanaendelea’’,alifafanua.

Nae mzazi Hassina Mjaka Mathias wa Mtemani Wete, alisema ghorofa analoishi yeye kwa mwaka mmoja sasa wamefanikiwa kuwazuia watoto na hasa baada ya kutokezea mmoja wao kuanguka.

“Alikuja mtoto kwangu kuja kutembea, wakati anafanya mtelezo huo aliangua ngazi wa chini na kuumia ndio maana wazazi tulikutana na kupiga marufuku’’,alifafanua.

Mtoto Himid Salum anasema kwa sasa mchezo huo wameuawacha, ingawa wanaofanya ni wenzao wasioishi kwenye nyumba hizo.

“Wanaofanya ni watoto wale wanaokuja mara moja kwa kutumwa kwenye nyumba hizi za ghorofa, lakini sisi tumeshaacha mchezo huo wa kutekeleza’’,alifafanua.

Sheha wa shehia ya Mtemani, Mrisho Juma Mtwana alisema alishapiga marufuku kwa muda mrefu juu ya mchezo huo kwa kushirkiana na wazazi husika.

“Nashukuru tumefanikiwa kuuzima mchezo wa kuteleza, ambao ulishashashiika kasi, lakini sasa twashukuru baada ya kukutana na wazazi hakuna tena michezo hiyo’’.alifafanua.


Katika miaka ya hivi karibuni watoto wanaoishi na wasioishi kwenye nyumba za maendeleo wamekuwa wakiendesha mchezo wa kuteleza kwa kutumia kuza za vidaraja vilivyomo kwenye nyumba hizo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.