Habari za Punde

Muhtasari wa Hotuba ya Uwasilishaji wa Ripoti ya Kamati ya Sheria Utawala Bora na Idara Maalum


Mhesmiwa Spika; 
Kwanza kabisa naomba nitumie nafasi hii adhim kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehma, Muumba wa Mbingu na Ardhi pamoja na vilivyomo ndani yake, kwa kutupa neema ya uhai na uzima katika kutekeleza majukumu yetu ya kila siku kwa hali ya amani na utulivu.
Aidha, napenda kuchukuwa nafasi hii kukushukuru wewe binafsi kwa kunipa nafasi hii ya kuwasilisha muhtasari wa Ripoti ya Kamati yetu ya Sheria, Utawala Bora na Idara Maalum, Ripoti ambayo inawasilisha shughuli zetu zote ambazo tumezitekeleza kwa kipindi kilichopita.

Mheshimiwa Spika;
Kamati ya Sheria, Utawala Bora na Idara Maalum imeundwa kwa mujibu wa Kifungu cha 85 cha Katiba ya Zanzibar, 1984 na Kanuni ya 106(1) ya Kanuni za Baraza la Wawakilishi – Zanzibar, Toleo la 2016 na kuainishwa majukumu yake chini ya Jadweli la Kwanza la Kanuni hizo la mwaka 2016.

Mheshimiwa Spika;
Napenda kuchukua nafasi hii muhimu kwa kuwashukuru Wajumbe wa Kamati hii kwa mashirikiano yao makubwa ambayo yameiwezesha kamati yetu kufanya kazi zake kwa ufanisi na uzoefu mkubwa. Wajumbe wenyewe ni hawa wafuatao:-
1.    Mhe. Machano Othman Said                       -       Mwenyekiti
2.   Mhe. Mwantatu Mbarak Khamis          -       Makamo M/kiti
3.   Mhe. Wanu Hafidh Ameir                            -       Mjumbe
4.   Mhe. Nadir Abdullatif Yussuf                        -       Mjumbe
5.   Mhe. Saada Ramadhan Mwendwa               -       Mjumbe
6.   Mhe. Mohammed Said Mohammed      -       Mjumbe
7.   Mhe. Ali Khamis Bakar                                -       Mjumbe    
8.   Ndg. Rahma Kombo Mgeni                         -       Katibu
9.   Ndg. Ali Alawy Ali                              -       Katibu.

Mheshimiwa Spika;
Katika utaratibu uliowekwa katika utekelezaji wa kazi za Kamati kwa muda wote uliopita, Kamati yetu ilipanga kufuatilia utekelezaji wa malengo na majukumu ya Wizara zifuatazo:-
i.             Wizara ya Nchi (OR) Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
ii.           Wizara ya Nchi (OR) Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ

Mheshimiwa Spika;
Kamati ilifanya kazi zake kwa muda wa wiki sita (06) ambapo kwa upande wa Unguja ilitumia wiki nne (04) na Pemba wiki mbili (02). Muda huo ulikuwa mdogo sana kwa namna ya wizara hizi zilivyo na ukubwa wa Idara na Taasisi zake.

Mheshimiwa Spika;
Hata hivyo, Kamati inawapongeza sana na kuwashukuru viongozi wa Wizara hizo wakiongozwa na Mawaziri wao, Naibu waziri, Makatibu Wakuu, Manaibu makatibu wakuu, Makamishna, Wukurugenzi, Maafisa Wadhamini Pemba na watumishi wao wote kwa ushirikiano wao mkubwa waliotuonesha katika kufanikisha majukumu yetu, licha ya kuwepo kwa changamoto mbali mbali zinazowakabili na kufanyakazi katika mazingira magumu na yenye upungufu wa nyenzo lakini wameweza kutekeleza majukumu yao ya kazi kadri hali ilivyokuwa inaruhusu.

Mheshimiwa Spika;
Naomba sasa uniruhusu nieleze kwa ufupi kabisa baadhi ya mambo yaliyojitokeza katika kazi za Kamati kwa Wizara kama ifuatavyo:-

WIZARA YA NCHI (OR) KATIBA, SHERIA, UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA:

Mheshimiwa Spika;
Wizara ya Nchi (OR) Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora inazo Idara na Taasisi mbali mbali ambazo zinafanya kazi kwa mujibu wa malengo yaliyopangwa chini ya Wizara hii. Hivyo, katika kukamilisha majukumu ya Kamati yetu tulifanikiwa kuzitembelea Idara na Taasisi kadhaa ambazo zimeunda Wizara hii na kujionea shughuli zao mbali mbali ambazo zimekabiliwa na changamoto kubwa kutokana upungufu wa vitendea kazi na udogo wa ukomo wa Bajeti.

Mheshimiwa Spika;
Kamati inaipongeza sana Wizara ya Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na Serikali kwa juhudi zake za kuanzisha mahkama ya watoto Mahonda, ambayo imefunguliwa hivi karibuni na Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohammed Shein, hivyo mahkama hiyo inatarajiwa kupunguza idadi ya kesi za udhalilishaji na ukatili dhidi ya watoto kwani vitendo hivyo vimeshamiri sana katika Mkoa huu wa Kaskazini Unguja. Ni matumaini yetu kuwa uanzishwaji wake utasaidia sana katika uendeshaji wa kesi zote zinazohusu watoto na kurahisisha upatikanaji wa haki za mtoto katika Mahkama zote za watoto ikiwemo Vuga na Chake-Chake kisiwani Pemba.

Mheshimiwa Spika;
Kamati ya Sheria, Utawala Bora na Idara Maalum katika ziara zake imebaini kuwepo kwa changamoto kubwa ya vyombo vya usafiri katika Idara na Taasisi mbali mbali zilizochini ya wizara hii, jambo ambalo linarudisha nyuma juhudi zao katika utekelezaji wa majukumu yao. Aidha, changamoto hii inaikabili zaidi Idara ya Nyaraka na Kumbu kumbu za Taifa, ambapo hadi sasa wana gari moja tu na kutokana na uhaba huo wameona wanunue vespa moja, wakati Tume ya Utumishi Serikalini hawana hata gari moja la kuwasaidia, hivyo huenda katika majukumu yao ya kazi kwa kutumia usafiri wa Daladala jambo ambalo ni kikwazo kikubwa katika utekelezaji wa majukumu yao.

Mheshimiwa Spika;
Afisi ya Afisa Mdhamin Pemba inajitahidi sana katika kusimamia na kutekeleza majukumu yao na kuhakikisha wameenda sambamba na malengo ya wizara na Serikali kwa ujumla. Aidha, Kamati imebaini kuwepo kwa baadhi ya Idara kutoingiziwa fedha za matumizi moja kwa moja isipokua fedha hizo huingizwa katika kurugenzi zao kuu ziliopo Unguja kitu ambacho kinasababisha Ofisi kuu Pemba kutumia fedha zake kwa ajili ya kuendeshea Idara hizo. Aidha, kutokuwepo kwa baadhi ya TaasisiS Pemba ikiwemo ikiwemo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Tume ya Kurekebisha Sheria, Tume ya Utumishi Serikalini na Ofisi ya Serikali Mtandao (E- Government) kunasababisha kuzorota kwa kazi za Taasisi hizo muhimu za Serikali.

Mheshimiwa Spika;
Kamati inaagiza kuchukuliwa hatua zinazofaa suala la kutoingizwa fedha za matumizi moja kwa moja katika baadhi ya idara zilizopo Pemba na kufanyiwa haraka uwepo wa Taasisi  zilizokosekana kisiwani Pemba ili kuondoa changamoto zinazojitokeza kwa kukosekana ofisi hizo.

Mheshimiwa Spika;
Lengo la Serikali ni kuona kwamba Idara na Taasisi zake zinafanikiwa katika utekelezaji wa majukumu yao na zinaleta ufanisi katika kuleta maendeleo kwa Nchi yetu. Aidha, Kamati imegundua kuwepo kwa changamoto kubwa ya vitendea kazi kwa upande wa Mahkama zote zilizopo Unguja na Pemba jambo ambapo kwa kiasi kikubwa linachangia kurundikana na kuchelewa   kwa uendeshaji wa kesi katika Mahkama zetu. Vile vile, tatizo hili linaonekana kuwa kubwa zaidi katika Taasisi ya ZAECA, CAG na Idara ya Nyaraka. Taasisi ambazo zinajukumu zito la kulinda na kusimamia rasili mali za Serikali ili zisipotee kwa watu wabadhirifu na watu wasiokuwa na imani na maendeleo ya Nchi yetu.

Mheshimiwa Spika;
Kamati inasisitiza tena kwa mara nyengine na kuishauri Serikali kwamba juhudi za makusudi zifanyike za kupatiwa vitendea kazi ili kuhakikisha malengo ya Taasisi hizi yanafikiwa kwa mujibu wa taratibu walizopangiwa.

Mheshimiwa Spika;
Katika kukabiliana na changamoto hii kwa upande wa Chuo cha Utawala wa Umma, Zanzibar, Kamati inashauri katika bajeti inayokuja Chuo kizingatie mahitaji ya watu wenye ulemavu kwa kuwapatia vifaa vya kisasa vya kujifunzia na kuboresha miundombinu ya majengo ili iweze kuwa rafiki kwao.
Vile vile kamati inaagiza chuo kuajiri wakalimani ambao watasaidia wanafunzi wenye ulemavu wa uziwi kupata nafasi ya kujifunza kwa uhakika na urahisi zaidi tofauti na ilivyo sasa kutokana na uhaba wa vitendea kazi na wataalamu. Kamati pia inakitaka Chuo hiki kujiimarisha tawi la Pemba kwani hivi sasa yupo mtumishi mmoja tu wa kudumu.

Mheshimiwa Spika;
Kamati imesikitishwa sana juu ya maendeleo ya baadhi ya Taasisi zetu ambazo zinatuongoza na kulinda haki za raia wa Nchi hii, huku tukiamini kwamba baadhi ya Taasisi hizo ni mihimili mikuu katika kuchunga na kulinda haki za wananchi. Ni dhahiri kuwa mazingira mazuri na salama kwa watendaji wa Taasisi hizo ndio yatakayo leta tija kwa maendeleo ya Nchi.

Mheshimiwa Spika;
Kuwepo kwa uchakavu na ubovu wa majengo ya Mahkama kwa Unguja na Pemba kunarudisha nyuma nguvu na ari ya utendaji katika mazingira yao ya kazi. Kamati ilifanya ziara katika Mahkama ya Mfenesini na Mwanakwerekwe na kuona hali ya majengo yake hayafai kabisa, hayana nafasi, lakini hadi leo bado Mahkama ya Mfenesini wana choo kimoja ambacho wanatumia Mahakimu, Makarani, mahabusu na wananchi wanaokuja katika kufatilia kesi zao; hali hii pia ipo katika Mahkama ya Mwanakwerekwe.

Mheshimiwa Spika;
Kwa upande wa Mahkama ya Wete nayo hairidhishi katika mazingira yake ya kazi kwani jengo lake ni bovu na halina nafasi ya kutosha pamoja na miundombinu mibovu ya maji. Mahkama hii inakabiliwa na ukosefu wa vitendea kazi kama vile makabati ya kuhifadhia majalada, ukosefu wa kompyuta ambapo ofisi nzima ipo kompyuta moja tu, lakini hata meza na viti vimechakaa kiasi ambacho havifai kwa matumizi ya Mahkama.

Mheshimiwa Spika;
Kamati imebaini kuwepo kwa ongezeko kubwa la kesi za ubakaji na udhalilishaji na jamii kutokua na uelewa wa kutosha juu ya kesi hizo, lawama kubwa ya ikiwahusisha Mahkama na Muendesha Mashtaka wa Serikali na Jeshi la Polisi.

Mheshimiwa Spika;
Kamati inaagiza kufanyiwa kazi suala zima la kesi za udhalilishaji katika jamii kwani limekua ni changamoto kubwa inayoikabili jamii na hata kukosekana imani kwa chombo cha mahkama na jamii. Adiha, Kamati inasisitiza kuwepo kwa mashirikiano mazuri wakati wa uendeshaji wa kesi za udhalilishaji kwa Jeshi la Polisi, DPP na Mahkama kwa kuhakikisha wamesimamia vyema upatikanaji wa ushahidi ambao utawatia hatiani watendaji wa kesi hizi bila kujali utafutaji wa suluhu unaopelekwa kutoka jamii ya waathirika. Pia, ni vyema Serikali kuziangalia na kuzifanyia marekebisho sheria ili adhabu ya wabakaji iwe kubwa kuliko ilivyo sasa.

Mheshimiwa Spika;
Vile vile, Kamati inaagiza ofisi ya Mufti kuimarisha mashirikiano yake na ofisi ya DPP katika kuangalia kesi za Walimu wa Madrasa ili kuweza kujua na kupata taarifa juu ya kesi hizo. Kamati inaishauri ofisi ya Mufti itoe maagizo ya barua kwa Maimamu wote Unguja na Pemba ili watoe elimu ndani ya Miskiti yao kwa lengo la kuisaidia jamii juu ya kuepuka na janga la vitendo vya ngono za jinsia moja.

Mheshimiwa Spika;
Kamati inaziagiza Idara na Taasisi ambazo bahazijafungua Ofisi zao Kisiwani Pemba zifanye hivyo katika mwaka huu wa fedha.

Mheshimiwa Spika;
Kamati yetu inahisi kuwa pamoja na juhudi za Serikali kusimamia utekelezaji wa majukumu ya watumishi wake, bado kuna changamoto ya wataalamu katika Idara na Taasisi mbali mbali za Serikali kitu ambacho kinaleta ukakasi katika ufanikishaji wa malengo ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika;
Kutokana na changamoto hii Kamati inaishauri wizara kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwasomesha watumishi wake katika ngazi mbali mbali za kielimu pamoja na kuajiri watu ambao ni wazalendo na wenye sifa za kutosha katika maeneo husika.

Mheshimiwa Spika;
Kamati yetu imebaini kuwa lipo tatizo la upatikanaji wa ajira pamoja na tatizo sugu na la muda mrefu la wafanyakazi waliofikia umri wa kustaafu kutokufanya hivyo. Kamati inashauri kwamba Serikali iweke wazi Kada ambazo zitaruhusiwa kuongezewa muda wa kazi wafanyakazi wake waliofikia umri wa kustaafu badala ya kuangalia umaarufu wa mfanyakazi wa sehemu husika. Hatua hii itasaidia kutoa ajira kwa vijana wapya ili nao watoe mchango wao katika ujenzi wa maendeleo ya Nchi yao.

WIZARA YA NCHI (OR) TAWALA ZA MIKOA, SERIKALI ZA MITAA NA IDARA MAALUM ZA SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR

Mheshimiwa Spika;
Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ inaundwa na kusimamiwa ni Idara na Taasisi mbali mbali zilizogawika maeneo makuu manne katika kutimiza majukumu yake pamoja na Ofisi ya Afisa Mdhamini Pemba. Aidha, Kamati inaipongeza sana Serikali kwa kuweza kuwapatia fungu lao la bajeti kwa asilimia kubwa katika Taasisi na Idara zake zote tofauti na miaka ya nyuma. Kamati imebaini kwa Taasisi zote za wizara hii imepatiwa bajeti kwa zaidi ya asilimia 95%.

Mheshimiwa Spika;
Kamati inaunga mkono mpango wa Serikali wa kuleta mfumo mpya wa Ugatuzi wa Madaraka Mikoani ambao utatumika kuendeshea Taasisi hizi. Hivyo, katika kukabiliana na changamoto ambazo zitakuja kuwa ni kikwazo cha majukumu yao, Kamati inaagiza Serikali za Mitaa kuwapa elimu watendaji wake wakiwemo masheha, madiwani na wafanyakazi wa kawaida kulingana na mabadiliko ya sheria na mazingira halisi ya utekelezaji wa sheria hizo katika mfumo wa Ugatuzi.

Mheshimiwa Spika;
Kamati imegundua katika baadhi ya Mabaraza ya Miji pamoja na Halmashauri zake kuwepo kwa tatizo la ukusanyaji wa Mapato pamoja na usiamamiaji mbovu uliopo kwa wafanyabiashara na wamiliki wa mahoteli. Hali hii imejitokeza kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini A na B kwa Unguja na Baraza la Mji Wete na Mkoani kwa Pemba. Kamati inaagiza Serikali za Mitaa kuhakikisha kuwa wamefikia malengo waliyojipangia na wamesimamia vyema ukusanyaji wa mapato katika vyanzo vyao mbali mbali na kuhakikisha hakuna mianya ya uvujaji wa mapato hayo ya Serikali.

Mheshimiwa Spika;
Katika uanzishawaji wa mfumo wa Madaraka kwa Wananchi (Ugatuzi) ni vyema Taasisi zitakazo husika na Mfumo huu kupewa elimu ya kutosha juu utoaji wa huduma kwa wanajamii badala ya kujikita katika uzalishaji wa mali pekee kama inavyoeleweka kwa baadhi ya Halmashauri na Mabaraza. Vile vile, Kamati inashauri Serikali za Mitaa kusimamia vyema utoaji wa huduma za kijamii na kuhakikisha kila mmoja zimemfikia na kwa kiwango chenye ubora kutokana na mapato wanayokusanya kupitia vyanzo vyao vya mapato.

Mheshimiwa Spika;
Katika ziara ya Baraza la Mji Chake-Chake, Wete na Mkoani, Kamati imeona wamekabiliwa na tatizo kubwa la uhaba wa wataalamu kama wahandisi, maafisa mipango na maafisa wa manunuzi na ugavi. Kamati inashuri kwa Mabaraza haya na yale yenye matatizo sawa na haya kuhakikisha wameajiri wataalamu wa fani mbali mbali ambao wanahitaji ili kusaidia kuleta ufanisi wa majukumu yao.
Mheshimiwa Spika;
Kamati imebaini kuwepo kwa baadhi ya Masheha ambao uwezo wao wa kazi umepunguwa kutokana na ugonjwa au umri mkubwa, hivyo Kamati inaagiza wizara kufanya mabadiliko ya Masheha ambao uwezo wao wa kazi umepungua kutokana na ugonjwa, umri mkubwa au kukosa uadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao.

Aidha, Kamati inaona ni vyema kuchukuliwa hatua za haraka kwa Askari Jamii ambao watabainika vitendo vyao haviendani na maadili ya uaskari au wanatumia vibaya majukumu waliyopewa kwa mujibu wa taratibu walizowekewa na kusababisha kuitia Serikali doa kwa wananchi au wageni wanaoingia Nchini, hususan maeneo ya Mji Mkongwe ambako ni kioo cha Nchi yetu.

Mheshimiwa Spika;
Kamati ya Sheria, Utawala Bora na Idara Maalum ilifanya ziara ya kutembelea vikosi vyote vitano (5) vya SMZ kwa upande wa Unguja na Pemba na kujionea shughuli zao mbali mbali za kizalendo na kuleta maendeleo ndani ya Nchi.
Aidha, Kamati inapongeza sana juhudi zinazofanywa na wapiganaji wetu wa vikosi hivi kwa kazi ngumu na nzito wanazozifanya za kulinda usalama na kuhakikisha wanadumisha uwepo wa amani na utulivu katika Nchi yetu.

Mheshimiwa Spika;
Sambamba na hayo, Kamati katika ziara yake hiyo imeweza kubaini changamoto mbali mbali zinazorudisha nyuma maendeleo ya Idara hizi kama vile:- Kuwepo kwa maslahi madogo ya wapiganaji, kuwepo kwa majengo na vitendea kazi ambavyo havikidhi haja ya askari wetu, ukosefu wa sare (uniform) za askari pamoja na kuwepo kwa ukosefu wa Hatimiliki na zaidi kwa upande wa Kambi za Pemba.

Mheshimiwa Spika;
Tatizo la ukosefu wa mahanga ya askari vituoni ni changamoto kubwa katika kufanikisha majukumu ya vikosi vyetu kwa unguja na Pemba, kwani vipo baadhi ya vikosi ambavyo havina kabisa makaazi ya askari wake na wanalazimika kutumia majengo yao ya ofisi kama mahanga ya kulala kwa muda wa usiku. Hali hii imejitokeza zaidi katika Kikosi cha Zimamoto na Uokozi Mwanakwerekwe, Wete na Uwanja wa Ndege wa Chake-Chake Kisiwani Pemba.

Mheshimiwa Spika;
Kamati inaishauri Serikali katika kutafuta majengo yanayostahiki ya ofisi na makaazi mazuri, uniform za askari wake pamoja na mambo mengine, basi isiwaachie vikosi peke yake katika kupambana na changamoto hizi na badala yake wajiwekee utaratibu maalum wa kusaidia ujenzi wa mahanga ya askari kupitia miradi ya maendeleo kama ilivyo kwa Taasisi nyengine za Serikali.  

Mheshimiwa Spika;
Kamati inaishauri Serikali kuangalia umuhimu wa kuanzisha kiwanda ambacho kitashughulika na utengenezaji wa Sare na viatu vya askari wetu ili kuepusha gharama kubwa inayotumika kwa kuagizia nje ya Nchi.

Mheshimiwa Spika;
Aidha, Kamati inashuri Serikali kuandaa Mfuko wa Bima ya Afya kwa wafanyakazi wote wa Idara Maalum katika kuwajengea mazingira mazuri ya utendaji wao, kwani baadhi ya askari wa vikosi hivyo hujitolea maisha yao moja kwa moja katika kuokoa maisha ya watu, hivyo nao wafikiriwe kwa kuangaliwa maisha yao wakati watapofikwa na matatizo ya kiafya. Hata hivyo, Kamati inaiomba Serikali kuanzisha mfuko wa Hifadhi ya jamii kwa upande wa vikosi vya SMZ kwa kuangalia utaratibu unaotumika wa vikosi vya ulinzi na usalama vya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili nao wapate kujifariji wakati wanapofikia muda wa kustaafu.

Mheshimiwa Spika;
Kamati inaagiza Wizara kufuatilia maeneo yote ya Kambi za Idara Maalum na kusimamia upatikanaji wa Hatimiliki za maeneo hayo hususan kwa upande wa vituo vya JKU Pemba kama vile Msaani, Chokocho na Ngezi pamoja na kituo cha KMKM Sengenya - Mtambwe, Kojani, Tundauwa, nk. Vile vile, kwa kuwa Serikali imeamua kurudisha tena utaratibu wa kuwapeleka vijana wa kujenga Taifa katika vituo vya JKU, Kamati inaishauri Serikali kuwapatia vifaa na vijana wa kutosha katika Jeshi la Kujenga Uchumi ili kuweza kuzalisha kwa kiwango kizuri.

Mheshimiwa Spika;
Baadhi ya kambi za vikosi vya SMZ vimekosa huduma ya Afya kama vile Chuo cha Mafunzo Kengeja, JKU Chokocho na Chuo cha Mafunzo Tungamaa na kufuatilia maeneo ya mbali na makaazi yao jambo ambalo ni kikwazo kwa wapiganaji wetu waliovituoni. Kamati inaona ipo haja ya kuwa na vituo vya Afya katika kambi zote za Unguja na Pemba ambazo pia, vituo hivyo hutumiwa na Wananchi jirani wanaoishi karibu na Kambi hizo. Aidha, Kamati inaitaka Serikali ifanye juhudi zake zote ili Kambi ya KMKM Sengenya ipatiwe Rada mpya kutokana na kuharibika kwa muda mrefu kwa Rada iliyokuwepo awali.

Mheshimiwa Spika;
Tatizo la kutoshirikishwa kwa maafisa wa vikosi vya Pemba katika uandaaji wa Bajeti za Idara zao pamoja na tatizo la kutokuwa na sub-vote kwa upande wa vikosi vilivyopo Pemba, imekuwa ni changamoto kubwa katika kufanikisha miradi yao na hivyo kushindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa. Aidha, Kamati inaiagiza Wizara ya Nchi (OR) Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ kuhakikisha wanasimamia vikosi vyote vya zoni ya Pemba kupatiwa Voti zao wenyewe na kuachana na mfumo wa kufikiriwa matumizi kwa kutengewa kiasi kidogo cha fedha ambazo hazisaidii chochote katika kutatua matatizo yao pamoja na kuendesha kazi za vikosi. Pia ni vyema kwa maafisa wa vikosi hivyo zone ya Pemba washirikishwe wakati wa uwandaaji wa Bajeti ya vikosi vyao.

HITIMISHO
Katika kutimiza wajibu na majukumu yake Kamati ya Sheria, Utawala Bora na Idara Maalum, imeitumia vyema Kanuni ya 106 (1) ya mwaka 2016 na kutoa ushauri na maelekezo ambayo matumaini yetu ni kuleta ufanisi katika ukamilishaji wa majukumu ya kila siku kwa Serikali, kupitia Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa pamoja na Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maaalumu za SMZ.

Aidha, Kamati inashauri kwamba wakati Kamati inapofanya ziara zake za kikazi basi awepo Waziri au Katibu Mkuu wa Wizara husika ili kujua matatizo yanayokabili Idara na Taasisi zao.

Kamati inawashukuru sana Mheshimiwa Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Katibu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar pamoja na watendaji wengine wote wa Afisi ya Baraza la Wawakilishi waliochangia kwa njia moja ama nyengine katika kufanikisha majukumu ya utekelezaji wa kazi za Kamati hii.

Mheshimiwa Spika;  NAOMBA KUTO HOJA

Ahsante;
(Mhe. Machano Othman Said)
Mwenyekiti,
Kamati ya Sheria, Utawala Bora na Idara Maalum
Baraza la Wawakilishi,
Zanzibar.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.