Habari za Punde

Rais wa Zanzibar Awapongeza Viongozi Waliopandishwa Vyeo.

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
 Zanzibar                                                                                                            6.2.2017
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa pongezi kwa viongozi wote waliopandishwa vyeo na kuapishwa katika hafla iliyofanyika leo Ikulu jijini Dar-es-Salaam na kueleza kuwa Jeshi la Ulinzi la Tanzania limejijengea sifa kubwa ndani na nje ya Tanzania.

Dk. Shein alisema hayo katika hafla ya kumuapisha Mkuu mpya wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Jenerali Venance Salvatory Mabeyo,  na viongozi wengine  akiwemo Mnadhimu Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi , Mabalozi na wengineo.

Katika hotuba yake fupi ya kusalimia na kutoa pongezi kwa viongozi hao walioapishwa, Dk. Shein alisema kuwa Jeshi la Ulinzi wa Tanzania limeweza kufanya kazi kubwa ya ulinzi hapa nchini sambamba na kuwa na nidhamu ya hali ya juu ambayo imeipa sifa kubwa Tanzania.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alimpongeza Mkuu wa Majeshi Mstaafu Jenerali Davis Mwamunyange kwa ufanyaji kazi wake katika muda wake wote wa kazi na kumpongeza na kumuahidi Mkuu huyo mpya wa Jeshi la Ulinzi Jenerali Mabeyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya itaendelea kutoa ushirikiano mkubwa kwake na kwa Jeshi hilo.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumpongezi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli kwa kumualika katika hafla hiyo kubwa.

Mabeyo aliteuliwa Februari 2 mwaka huu na Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Magufuli kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Jenerali Davis Mwamunyange.

Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewaapisha viongozi aliowateua hivi karibuni kushika nyadhifa mbali mbali katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Viongozi walioapishwa na Rais Dk. Shein ni Ibrahim Mzee Ibrahim ambaye anaendelea kuwa Mkurugenzi wa Mshatka (DPP), Jaji Rabia Hussein Mohamed kuwa Mwenyekiti wa Mahkama ya Rufaa ya Idara Maalum za SMZ, Asha Ali Abdalla ambaye anakuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Wengine ni  Yakut Hassan Yakout ambaye anakuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Seif Shaaban Mwinyi ambaye anakuwa Naibu Katibu Mkuu katika Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utum,ishi wa Umma na Utawala Bora anayeshughulikia Utumishi wa Umma.

Hafla hiyo ilifanyika Ikulu mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd, Jaji Mkuu wa Zanzibar  Omar Othman Makungu, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Said Hassan Said, Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji.

Mkuu wa  Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohamed Mahmoud,  Wakuu wa Vikosi vya SMZ, Meya wa Manispaa ya Mji wa Zanzibar Khatib Abrahman Khatib, Washauri wa Rais wa Zanzibar pamoja na viongozi wengine wa Serikali.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.