TAARIFA KWA VYOMBO VYA
HABARI
HUDUMA ZA AFYA ZISIFUNGWE WAKATI WA ZOEZI LA
USAFI-MAJALIWA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka
viongozi wa ngazi mbalimbali waweke utaratibu utakaoruhusu huduma za afya
kuendelea kutolewa kwa wananchi katika maeneo yao hata kama zoezi la usafi la
kila mwezi litakuwa linaendelea.
Serikali imeweka utaratibu wa wananchi
kushiriki katika shughuli za usafi wa mazingira siku ya Jumamosi ya mwisho wa
mwezi, zoezi ambalo linashirikisha watu wote wakiwemo wafanyabiashara na watoa
huduma nyingine zoezi linalofanyika kuanzia saa 12.00 asubuhi hadi saa 4.00
asubuhi.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Mei 11, 2017) Bungeni mjini Dodoma
katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu wakati akijibu
swali la Mheshimiwa Abdallah Ulega mbunge wa Mkuranga.
Mheshimiwa Ulega alitaka kupata kauli ya Serikali kuhusu maeneo
ya kutolea huduma mbalimbali zikiwemo za afya ambayo hufungwa wakati wa zoezi
la usafi linalofanyika kila mwezi nchini, jambo linalosababisha kero kwa
wagonjwa na wengine wenye dharula.
Waziri Mkuu amesema “Hospitali na maeneo mengine ya kutolea
huduma za afya hayawezi kufungwa, viongozi wa maeneo husika waweke utaratibu
mzuri utakaoruhusu huduma hizo ziendelee kutolewa bila ya kuathiri zoezi la
usafi wa mazingira,”.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema
Serikali imeagiza tani 131,000 za sukari ili kukabiliana na upungufu uliopo
nchini. Amesema Serikali iko macho na inajua maeneo yanayohitaji kuboreshwa
kulingana na mahitaji.
“Mahitaji ya sukari nchini kwa mwaka ni tani 420,000,
ambapo tunazalisha tani 320,000, hivyo tunaupungufu wa tani 100,000 hata hivyo
tumeagiza tani 131,000 na tayari tani 80,000 zimewasili nchini, ambapo kati
yake tani 35,000 zimeingizwa sokoni,” amesema.
Ametoa kauli hiyo wakati akijibu swali lililoulizwa na
Mheshimiwa Jaku Hashim Ayoub aliyetaka Serikali iwahakikishie wananchi
upatikanaji wa sukari hususan katika kipindi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani
unaotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
ALHAMISI, MEI 11, 2017.
No comments:
Post a Comment