Habari za Punde

Mlinda mlango Miembeni City asema: wanasubiri kucheza ligi kuu, kazi waliyotumwa wameshaimaliza


Na: Abubakar Khatib Kisandu, Zanzibar.

Golikipa mahiri wa timu ya Miembeni City Aley Ali Suleiman “Manula” amesema mzigo waloagizwa tayari wameshaufikisha panapostahiki wanachosubiri sasa ni kucheza ligi kuu soka ya Zanzibar msimu ujao.

Mbali ya kuwa mabingwa City lakini bado hawana uhakika wa kucheza ligi kuu msimu ujao ambapo Chama cha Soka Visiwani Zanzibar “ZFA” kimepania kuchezesha vilabu 12 tu pekee kwenye ligi kuu msimu huo, wakati huo huo mpaka sasa vipo vilabu 28.

Timu hizo 28 ni zile 12 za Unguja na 12 za Pemba zilizobakia msimu huu, na nyengine 2 za Unguja na 2 za Pemba zilizotoka Daraja la Kwanza, ndipo hapo kwa pamoja watapanga ni mfumo gani utumike ili zipatikane timu 12 za msimu ujao ambapo mpaka sasa inasubiriwa imalizike 8 bora ndipo mchakato huo uanze.

Aley amesema wao kama wachezaji walitumwa wafanye kazi kuipandisha timu daraja na tayari wameshafanya hivyo, kilichobakia wanasubiri ZFA wataamua vipi kuhusu vilabu 12 vitakavyocheza ligi kuu msimu ujao.

“Sisi wachezaji tushafanya kazi tuliyoagizwa, na tunajua tumeshapandisha timu ligi kuu, mana sisi ndio wa kwanza na ndio mabingwa daraja la kwanza, hivyo mimi kama mchezaji sina maneno mengi ya kusema kwa vile tushapigana na tayari mzigo tushaufikisha panapotakiwa, uamuzi wa ZFA tena hapo sijui watapangaje lakini sisi wachezaji tushamaliza kazi”. Alisema Aley.

Miembeni City wamemaliza msimu wa mwaka 2016-2017 wakiwa mabingwa wa daraja la kwanza Taifa Unguja ambapo Mlinda mlango huyo alipigana kuhakikisha kuwa timu yake inapanda daraja baada ya kucheza michezo 17 na kufungwa mabao 7 tu pekee langoni mwake na ndio timu pekee kwenye daraja hilo kuruhusu lango lao kufungwa mabao kidogo ambapo safu yao ya ulinzi ilikuwa imara sana inayoongozwa na kipa huyo pamoja na walinzi Abuu Luiz na Ali Mwinyi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.