Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi DK.Ali Mohamed Shein akisalimiana na mgeni wake Balozi wa Namibia katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe,Theresia Samaria Balozi wakati alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo,[Picha na Ikulu.]30/05/2017.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi DK.Ali Mohamed Shein akizungumza na mgeni wake Balozi wa Namibia katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe,Theresia Samaria Balozi wakati alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo,[Picha na Ikulu.]30/05/2017.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi DK.Ali Mohamed Shein akifuatana na mgeni wake Balozi wa Namibia katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe,Theresia Samaria Balozi baada ya mazungumzo yao wakati alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo,[Picha na Ikulu.]30/05/2017.
STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 30.05.2017

RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa ipo
haja kwa Zanzibar kushirikiana na Namibia katika kuimarisha sekta za maendeleo
zikiwemo biashara na uvuvi hatua ambayo itaimarisha uhusiano na ushirikiano wa
kihistoria kati ya Tanzania na nchi hiyo.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo, Ikulu mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Balozi wa Namibia katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bi Theresia Samaria.
Katika mazungumzo
hayo, Dk. Shein alimueleza Balozi Samaria kuwa Zanzibar na Namibia zina mambo mengi ya kushirikiana kwa pamoja
ambayo yanaweza kuleta mafanikio makubwa kwa pande zote mbili.
Dk. Shein alieleza
kuwa uhusiano na ushirikiano wa
kihistoria uliopo kati ya Tanzania na Namibia ni njia moja wapo kubwa
itakayopelekea kuimarika zaidi kwa mahusiano na mashirikiano hayo hasa katika
sekta za maendeleo ikiwemo biashara na uvuvi.
Aidha, Dk. Shein
alimueleza Balozi huyo kuwa kutokana na nchi hiyo kupiga hatua kubwa katika
sekta ya uvuvi, itakuwa ni muwafaka zaidi hasa ikizingatiwa kuwa Zanzibar imezungukwa
na bahari ya Hindi na hivi sasa imejiwekea mikakati mikubwa katika kuimarisha
sekta hiyo hasa katika uvuvi wa bahari kuu.
Aliongeza kuwa, kwa
upande wa sekta ya biashara pande hizo mbili zinaweza kuimarisha na kuendeleza
sekta hiyo hasa ikizingatiwa kuwa nchi zote hizo zimepakana na Bahari ya Hindi
hivyo ni rahisi zikatumia usafiri wa majini.
Dk. Shein alieleza
kuwa katika kuhakikisha Zanzibar inaimarika katika sekta ya biashara ikiwa ni
pamoja na usafiri na usafirishaji imo katika mikakati ya kujenga bandari yake
mpya ya Mpigaduri ambayo itasaidia zaidi kuimarisha sekta hiyo kwani itakuwa
kubwa na itaweza kutoa huduma bora zaidi kuliko bandari iliyopo hivi sasa.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imenunua meli yake
mpya ya MV Mapinduzi II ambayo kwa mashirikiano ya pamoja baada ya Serikali
kulifanyia kazi suala hilo inaweza kufanya safari kati ya Zanzibar na Namibia
hatua ambayo itaimarisha sekta ya biasahara na hata sekta ya utalii.
Dk. Shein alieleza
kuwa mbali ya mashirikiano ya sekta hizo mbili muhimu, nchi hizo zinaweza
kuimarisha ushirikiano katika sekta ya elimu, afya pamoja na kuanzisha ziara za
kutembeleana kati ya viongozi, wataalamu pamoja na watendaji wa pande mbili
hizo ili kukuza uhusiano, kupanua wigo wa kitaalamu na kimaendeleo kwa manufaa
ya pande zote mbili.
Nae Balozi wa Namibia
katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bi Theresia Samaria alimueleza Dk. Shein
kuwa Namibia itaendelea na dhamira yake ya kuimarisha zaidi uhusiano wa kidugu
uliopo kati yake na Tanzania ikiwemo Zanzibar ambao umejengwa kabla na baada ya
uhuru wa nchi hiyo wa mwaka 1990.
Balozi Samaria
alitumia fursa hiyo kufikisha salamu za Rais wa nchi yake Rais Hage Geingob kwa
Dk. Shein ambapo alisisitiza kuwa nchi hiyo itaendeleza ushirikiano wake na
kukuza uhusiano wa kihistoria na Zanzibar.
Katika maelezo yake
Balozi Samaria alimueleza Dk. Shein, kuwa ni vyema nchi za bara la Afrika zikashirikiana
katika sekta za maendeleo kwani anaona
fahari iwapo nchi yake itakuza ushirikiano na Zanzibar hasa katika sekta ya
biashara.
Alieleza kuwa kwa
upande wake ameona kuna faida nyingi zinaweza kupatikana katika sekta ya
biashara iwapo mashirikiano yatakuwepo hasa ikizingatiwa kuwa Zanzibar imekuwa
ikizalisha mazao mbali mbali ambayo kwa
nchi yake yanahitajika kwa kiwango kikubwa .
Aidha, Balozi Samaria
alieleza kuwa mashirikiano katika sekta ya uvuvi pamoja na biashara kati ya nchi yake na Zanzibar yanaweza kupata
mafanikio hasa ikizingatiwa kuwa nchi yake imepiga hatua kubwa katika kupambana
na uhalifu baharini.
Aliongeza kuwa nchi
hizo zinaweza kushirikiana katika sekta kadhaa za maendeleo hasa ikizingatiwa Namibia
imelingana na Zanzibar kutokana na
kupitiwa wa Bahari ya Hindi kwa upande wake wa Mashariki na kupelekea shughuli
za uvuvi kuimarika zaidi.
Balozi Samaria
alieleza kuwa utekelezaji wa Sera ya Diplomasia ya Uchumi kutaimarisha hatua za
kukuza uhusiano na ushirikiano katika
sekta za maendeleo kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar na
Namibia.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment