STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 26.08.2017
UONGOZI wa Mkoa
wa Kusini Pemba kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na
Uvuvi umepongezwa kwa kuyabainisha na kuyarejesha Serikalini mashamba ya
Serikali na kuagizwa kwa wale wote ambao bado wanayaficha mashamba hayo ni bora
wayarejeshe wenyewe vyenginevyo wakibainika wawachukulie hatua kali za
kisheria.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliongeza
kuwa hatua hizo kali za kisheria zichukuliwe bila ya kujali wadhifa wa mtu,
cheo alichonacho ama umaarufu wake.
Agizo hilo limetolewa leo na Dk. Shein huko katika
ukumbi wa Makonyo, Jimbo la Wawi, Wilaya ya Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba
wakati akitoa majumuisho ya ziara yake kwa Mkoa huo aliyoifanya kuanzia Agosti
24 mwaka huu.
Aidha, Dk. Shein aliuagiza uongozi wa Mkoa huo
pamoja na Wilaya zake kusimamia vizuri ukusanyaji mapato na kushirikiana na
wafanyabiashara katika kuwashajiisha ili walipe kodi na kuongeza mapato ya
Serikali.
Aliwataka viongozi hao kutojiingiza katika
kuwasaidia kukwepa kodi wala kuwakingia kifua kwa makosa yao wanayoyafanya
katika kukwepa kulipa kodi huku akiwataka kuwashajiisha wafanyabiashara watoe
risiti wanapouza bidhaa zao na kuwaelimisha wananchi wapewe risiti wanaponunua
bidhaa.
Pia, Dk. Shein ameiagiza Wizara ya Habari, Utalii,
Utamaduni na Michezo kufanya mkutano maalum na Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote za
Unguja na Pemba kwa ajili ya kupanga na kupeana majukumu ya utekelezaji wa
mpango wa Utalii kwa Wote huku akiuagiza uongozi wa Mkoa kushirikiana na Wizara
hiyo kulishughulikia eneo la historia la
Mkamandume.
Kwa upande wa wajibu wa Chama Cha Mapinduzi, Dk.
Shein ambaye pia, ni Makamo Mwenyekiti wa chama hicho kwa upande wa Zanzibar
aliwataka wanaCCM kuendeleza umoja na mshikamano uliopo na kuepuka mivutano
miongoni mwao na kama ipo waachane nayo kwani haina tija.
Aliwataka wanaCCM kuandaa utaratibu mzuri wa kusimamia
utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa CCM ya mwaka 2015-2020 sambamba na
kuyatumia Matawi ya CCM kwa ajili ya kukiimarisha chama hicho na kujiandaa kwa
uchaguzi mkuu ujao.
Pamoja na hayo, Dk. Shein aliuagiza uongozi wa
Mkoa na Wilaya zake zote mbili kushirikiana na Maafisa Ukaguzi wa Elimu katika
maskuli na iwapo watawabaini walimu watoro kazini na wale wanaofanya siasa
skuli wamuarifu Waziri wa Eloimu na Mafunzo ya Amali ili awachukulie hatua kwa
mjibu wa sheria ya Utumishi wa Umma namba 2 ya mwaka 2011.
Aidha, katika kuhakikisha kuwa majengo ya skuli
yanakuwa na ubora unaotakiwa na kuweza kutumika kwa muda mrefu alitaka Wizara
hiyo ya Elimu kuhakikisha majengo ya madarasa yanayojengwa yanakuwa na
mazingira bora na yenye viwango.
Pia, alitoa agizo kwa uongozi wa Mkoa kuwa soko
jipya linalojengwa katika eneo la Tibirinzi kuanzia jana (25.8.2017) liitwe
soko la Tibirinzi badala ya soko la Katar na kuutaka uongozi huo kulisimamia
suala hilo kwa nguvu zake zote bila ya kugombana na watu.
Dk. Shein alitoa wito kwa Mabaraza ya Miji ya Mkoa
huo, kusimamia vizuri usafi wa Miji pamoja na mipango miji na kutaka kuendelea
kuwachukulia hatua waatu wanaojenga karibu sana na barabara.
Alisisitiza kuwa Mkoa ni lazima uwe na mpango wa
muda mrefu wa kulishughulikia tatizo la nafasi ya maegesho ya gari
linaloendelea kujitokeza katika mji wa Chake Chake.
Aliwataka
viongozi wote wa Mkoa huo kwenda kubainisha halafu watafute mbinu ya kuiondosha
hali ya wizi wa karafuu na ni vyema wakalifuatilia suala hilo ili kuujua ukweli
huku akiahidi kuwa Serikali inatekeleza ahadi yake ya kumpa mkulima asilimi 80
ya bei ya soko.
Kwa kukinga ajali za barabarani zinazotokea mara
kwa mara kisiwani Pemba pia, Dk. Shein alieleza kupata taarifa ya kuwepo vijana
katika eneo la Chake Chake wenye kuiga nyendo za kundi la ‘T-One hasa nyakati
za usiku na kuutaka Mkoa kushirikiana na Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua
wasiozingatia sheria za barabarani.
Dk. Shein. Alieleza kufurahishwa kwake na
upatikanaji wa maji katika Mkoa wa Kusini Pemba ambao umefikia asilimia 83.
Dk. Shein pia, aliwapongeza wanafunzi wa kike kwa
kufanya vizuri katika masomo yao na kueleza haja ya kufanywa utafiti ili kuweza
kujua ni kwa nini watoto wa kiume wamekwua wakiachwa nyuma.
Katika maelezo yake Dk. Shein alieleza
kutoridhishwa na kuona kuwa hakuna Mkoa hata mmoja uliotoa taarifa juu ya
maendeleo ya skuli 19 za Sekondari za
Wilaya na kueleza kuwa atakuwa anafuatilia matokeo ya skuli hizo ambazo
zimejengwa kwa gharama kubwa na Serikali.
Sambamba na hayo, aliupongeza uongozi wa Mkoa huo
kwa kuimarisha ulizni na usalama katika kuhakikisha wananchi wanaendelea na
shughuli zao za kiuchumi na kijamii katika hali ya amani na utulivu na kuutaka
uendelee kusimamia amani, umoja na mshikamano na kutoa huduma kwa wananchi bila
ya ubaguzi kwani wote ni wamoja.
Aliitaka Mikoa yote ya Pemba iendeleze juhudi za
kushajihisha ufugaji wa samaki katika Mikoa na maeneo mbali mbali yanayoweza kuendeleza
shughuli hizo.
Dk. Shein apia, aliwataka viongozi wote wakiwemo
wa Mawaziri, Wabunge, Wawakilishi, Wakuu wa Mikoa, Makatibu Wakuu, Makatibu Tawala wa Mikoa na
Wilaya, Maafisa Wadhamini, viongozi wa Serikali, chama cha CCM, Masheha,
Makamanda.
Dk. Shein amemaliza ziara yake katika Mikoa yote
ya Unguja na Pemba iliyoanza tarehe 12 Agosti mwaka huu huko katika Mkoa wa
Kaskanini Unguja ikiwa na lengo la kuangalia utekelezaji wa miradi ya maendeleo
chini ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi
Mkuu ya CCM ya mwaka 2015-2020 pamoja na uimarishaji wa Matawi na Maskani za
CCM hapa nchini.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address:
2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment