Habari za Punde

Wadaiwa sugu ukodishwaji mikarafuu Pemba kukabidhiwa ZAECA

Na.Haji Nassor - Pemba.
WIZARA ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi kisiwani Pemba, imesema ikiwa hadi Oktoba 23 mwaka huu, wananchi wanaodaiwa zaidi ya shilingi bilioni 1. 492 zinazotokana na ukodishwaji wa mikarafuu hawajalipa fedha hizo, Wizara hiyo itawakabidhi kwa ZAECA.

Kauli hiyo, imetolewa na Afisa Mdhamini wa wizara hiyo, kisiwani humo Sihaba Haji Vuai, wakati alipokuwa akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, juu ya mwenendo wa ukodishaji na namna ya wananchi waliokodi walivyolipa fedha hizo.

Alisema tayari mashamba 1,451 yameshakodishwa kwa wananchi mbali mbali kisiwani Pemba, ambapo kama ingekuwa wameshalipa, serikali ingepata zaidi ya shilingi bilioni 2.393, ingawa hadi sasa, ni zaidi ya shilingi milioni 900.661 zilizokwishalipwa .

Alisema ambacho bado kimo mikononi mwa wananchi hao waliokodia amshamba ya mikarafuu ya serikali, ni shilingi bilioni 1.492 ambazo hizo, zinatakiwa kulipwa sio zaidi ya Oktoba 23, mwaka huu.

Alisema kuanzia Oktoba 24, mwaka huu wadaiwa hao kama hawajalipa fedha hizo, wizara hiyo itawakabidhi kwa Mamlaka ya Kuzuia rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar ZAECA, ili kuwashikilia kisheria.

“Zoezi la ukodishaji bado linaendelea, lakini kwa sasa fedha nyingi bado ziko mikononi mwa wananchi, waliokodi mashamba kwa hiari zao na mikataiba iliwataka walipe ndani ya wiki mbili, lakini kuanzia Oktoba 24, basi tutawakabidhi kwa wenzetu ZAECA”,alifafanua.

Akatika hatua nyengine Afisa Mdhamini huyo, aliwataka wananchi wema wanaopenda maendeleo ya nchi hii, kuendelea kuyafichua mashamba ya serikali na kuyaripoti kwa mamla husika, ili yarudi serikali kisheria.

Alieleza kuwa, katika zoezi hilo lililoanza Julai 1, mwaka huu lilisaidia kuyaibua mashamba kadhaa mapya, ambayoa kwa muda mrefu serikali ilikuwa haijawayatambua.

Alisema kwa mfano kwenye wilaya ya Micheweni walitarajia kuwa na mashamba …lakini baada ya wananchi wema kuona umuhimu wa kuyafichua mashamba hayo, kwa msimu huu wameyapata mashamba …..

“Aidha kwa mfano kwenye wilaya ya Chakechake shehia za Gombani, Kwale, Tibirinzi na Mkoroshoni tulikuwa hatuna mpango wala uwelewa kuwa kuna mashamba ya mikarafuu lakini kwa sasa tunayo mashamba 10 mapya”,alisema.

Aidha alifafanua kuwa kwenye wilaya ya Micheweni, walijiwekea malengo ya kuwa na mashamba 50 pekee, ingawa wakati zoezi hilo likiendelea limeibua mashamba 169, sawa na ongezeko la mashamba 119 yaliokuwa yakimilikiwa na wananchi kinyume na sheria.

Hata hivyo alisema sio kweli kuwa zoezi hiloi lengo lake ni kuwany’ang’a wananchi mashamba yao, bali lengo ni kutaka mali ya serikali kurudi mikononi mwake na wananchi walipokwisha tumia panatosha.

Alisema wakati zoezi hilo likitaka kuanza mapema mwaka huu, walidhamiria kuwa watayaibua mashamba ya ya serikali 1,525  ingawa hadi sasa wakati zoezi halijamalizika tayari wameshayapaa mashamba ya eka tatu tatu 1,451 pamoja yake matano makuwa likiwemo la Makuwe, Daya Mtambwe, Kianyasini, Gando na Mkoani.

Kwa upande wake Afisa Mashamba ya serikali kisiwani Pemba, Haji Mussa Haji, alisema kwa vile zoezi hilo linazingatia sheria zilizopo, yapo mashamba 84 waliyoyakodisha kinyume na taratibu, wamesharejeshewa wenyewe, baada ya kuyonyesha nyaraka halali.

“Tunapokodisha mmiliki wa shamba akija na nyaraka basi tunakaa nae meza moja, kuipitia kifungu kwa kifungu na aya kwa aya, na tukibaini wakabidhiwa wenyewe, kama ambapo sasa tumeshafanya kwa madhamba 84, yakiwa 20 Kusini na 64 kaskazini Pemba”,alifafanua.

Aidha Afisa huyo, alisema pia zipo shilingi milioni 528 ambazo hazijalipwa kama kifuta jasho kwa wananchi wale ambao walikuwa wakiyalea mashamba hayo ya serikali, ambapo hupatiwa fedha hizo, hata kama aliekodi ndie anaelilea.

Wakati huo huo   Mdhamini wa ZAECA Pemba, Suleiman Ame Juma alisema, wako tayari kushirikiana na wizara yoyote ikiwemo hiyo ya Kilimo, katika kutetea na kunusuru mali ya umma isiishie kwenue mikono ya wachache.

“Sisi hiyo ni kazi yetu kwa mujibu wa sheria, tunaweza kuwahoji na kuwashikilia kisheria, mtu yeyote ambae anaenda kinyume na uwajibikaji wa fedha za umma”,alifafanua.

Zoezi la ukodishaji wa mashamba ya serikali ambao ulianza Julai 1, mwaka huu, umesaidia kwa kiasi kikubwa kuyafichua mashamba kadhaa ya serikali ambayo, yalikuwa mikononi mwa wananchi wa kawada.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.