Habari za Punde

Wanachama wa CCM Kaskazini Pemba: ‘Tunajipanga Kusaka 16/m’

Tawi jipya la CCM Pandani wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba, ambalo August 8, mwaka huu, liliwekewa jiwe la msingi na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Mhe; dk Ali Mohamed Shein, ambapo kwa sasa shilingi milioni 26, zinahitajika huku, Makamu Mwneyekiti huyo wa CCM Zanzbar, akiahidi shilingi milioni 10, mara tu CCM mkoa wa kaskazini Pemba, itakapokusanya shilingi milioni 16, (Picha na Haji Nassor, Pemba).
Na.Haji Nassor - Pemba.
CHAMA cha Mapinduzi CCM Mkoa wa kaskazini Pemba, kimesema kinaendelea kujipanga, ili kuhakikisha wanazipata shilingi milioni 16, kati ya shilingi milioni 26, zinazohitajika, kwa ajili ya kumaliza hatua ya ujenzi wa tawi jipya la kisasa la CCM Pandani.
 August 8, mwaka huu Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Mhe: dk, Ali Mohamed Shein wakati ya ziara yake ya siku nne kisiwani Pemba, alifika kwenye tawi hilo, kwa uwekaji wa jiwe la msingi, ambapo wanaccm wa tawi hilo, waliomba shilingi milioni 26, kwa ajili ya kumalizia ujenzi  tawi hilo.
Hivyo, aliuagiza uongozi wa CCM Mkoa wa kaskazini Pemba, kuzisaka kwa udi na uvumba shilingi milioni 16, ambapo nae baada ya wao kuzipata fedha hizo, aarifiwe ili akamilisheni ahadi yake ya shilingi milioni 10.
Mwenyekiti wa CCM Mkoani humo, Mberwa Hamad Mberwa, akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu, alisema walikuwa wanasubiri kwanza wamalize chaguzi zao za ndani, pamoja na kumalizika kwa kikao cha baraza la wawakilishi, ili wakutane na mwakilishi wa jimbo la Pandani.
Alisema kikao hicho, kitakachojumuisha viongozi kadhaa wa CCM, ndio kitakachozaa wazo na njia za kuzipata shilingi milioni 16, ambapo hapo baadae, ndio watawasiliana na Makamu Mwenyekiti CCM Zanzibar, kwa ajili na yeye kukamilisha ahadi yake ya shilingi milioni 10.
“Lile agizo la Makamu Mwenyekiti wetu wa CCM Zanzibar, bado hatujalikalia kitako, lakini muda sio mrefu tutakutana, ili kuhakikisha tunagawana majukumu, kwa lengo la kujipatia fedha hizo”,alifafanua.
Aliongeza kuwa, mtazamo wake anatarajia kuwashawishi viongozi hao kwamba, sio lazima fedha taslimu ndio zinazohitajika, bali hata vifaa vya ujenzi, ili kufanikisha ujenzi huo.
Alisema, wanatarajia kuwafikishia machango huo viongozi kadhaa, wakiwemo wanachama wa CCM wenyewe, viongozi wa majimbo, wilaya, Mkoa na hata maofisa wadhamani ambao walishaonyesha nia hiyo.
“Siku ile ya August 8, maofisa wadhamini wa kisiwani Pemba, waliomba na wao wakaingizwe kwenye machango  huu wa kumalizia ujenzi wa tawi la CCM Pandani, hivyo siku ikifika na wao watajumuishwa”,alifafanua.
Katika hatua nyengine, Mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa wa kaskazini Pemba, alisema wanaendelea kuyajenga matawi mengine ya CCM ya Njuguni, Wete mjini, kisiwani kwa binti Abeid  na mengine ili yawe na hadhi ya kitaifa.
Wakati alipotembelea tawi hilo la CCM Pandani, kwa uwekaji wa jiwe la msingi, Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe: Dk, Ali Mohamed Shein, alipongeza hatua ya wanaccm hao kuanzisha ujenzi huo.
Alisema, wakati umefika sasa kwa CCM, kuwa na matawi na ofisi za kileo, ambazo zitajengwa kwa nguvu za wanaccm wenyewe, kama walivyofanya kwa wana wa ASP, wakati wao kwa kujenga matawi na ofisi walizozirithi.

Aidha Makamu huyo Mwneyekiti wa CCM Zanzibar, baada ya kuelezwa kuwa, zinahitajika shilingi million 26, ili kukamilishia ujenzi huo, aliahidi kutoa shilingi milioni 10, na shilingi milioni 16 zilizobaki, aliuagiza uongozi wa CCM Mkoa wa kaskazini Pemba, kuzitafuta.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.