Na.Haji Nassor - Pemba.
BARAZA la wazee shehia ya Vitongoji
wilaya ya Chakechake mkoa wa kusini Pemba, wamesema kama wakipatiwa mashine ya
kusagia nafaka, wana uhakika wataondokana na utegemezi, ndani familia zao, kama
ilivyo sasa.
Wakizungumza
na mwandishi wa habari hizi, walisema mkombozi wa kweli wanaemfikiria ndani ya
baraza lao, sio jambo jengine, bali ni kupatiwa mashine hiyo, ambayo wanaamini
haina msimu.
Walisema
kutokana na kuanza kupoteza nguvu za kuendeleza kilimo, inakuwa ni vigumu kuwa
na miradi inayohitajika kutumia nguvu, bali miradi ya aina hiyo, ndio wanayoimudu.
Katibu wa
baraza hilo Ali Juma Khamis, alisema wanaamini kuanzishwa kwa mabaraza hayo,
yanayolelewa na JUWAZA na Help Age International Tanzania, kunaweza kuwakomboa,
hasa wakiwa na miradi.
Alisema
jamii imekuwa ikiwapa kisogo wazee kwa kutowapatia huduma kamili, kama
walivyobinadamu wengine, na ndio maana baada ya kujikusanya pamoja ndani ya
mabaraza hayo, yanaweza kuwanawirisha.
“Sisi kulima
hatuna nguvu tena, lakini kama wafadhili au hata serikali yetu itatupatia
mashine kama ya kusagia nafaka, basi tutajiongezea kipato na kuondokana na
utegemezi ndani ya familia zetu”,alisema.
Nae mshika
fedha wa baraza hilo Jine Ali Abeid, alisema aina yoyote ya miradi, ambayo
haihitaji kutumia nguvu sana, inaweza kuwasaidia kujikomboa.
“Hata kama
tukipata miradi kama ya ufugaji, biashara ndogo ndogo kwa mujibu mazingira
yetu, sisi tunaamini kwa umoja wetu, basi tutafikia pahala pazuri”,alisema.
Kwa upande
wake mjumbe wa baraza hilo la wazee shehia ya Vitongoji Ali Omar Abdalla,
alisema waliamua ,kujikusanya pamoja ili wawe na sauti moja, ya kutetea haki
zao.
Alisema,
wazee wanamahitaji kadhaa ikiwa ni pamoja na matibabu kuwa na dirisha pekee la
dawa, kwenye vyombo vya usafiri kutokaa foleni, haki ambazo wasipokaa pamoja ni
vigumu kutekelezwa.
“Wazee wa
shehia hii ambao bado hawajajiunga, muda ndio huu, maana wakikaa pembeni na
kisha kudai haki zao inakuwa vigumu kuzipata”,alisema.
Kwa upande
wake mlezi wa bara hilo, ambae ni sheha wa shehia hiyo Salim Ayoub Suleima,
alisema kutokana na idadi ya wazee 180 walio na umri wa kuanzia miaka 6o na
kundelea bado baraza hilo ni dogo.
Alisema
wazee wa shehia yake, wanakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na
waliofika umri wa miaka 70 kutopata pencheni jamii, kwa vile hukosa msimazi wa ndani
ya shehia yake.
“Naamini
wazee hawa wa Vitongoji, sasa kama wakikaa pamoja hakutakuwa na mzee ambae
anastahiki kupewa pencheni jamii kukosa, maana itakuwa wanamfuatiliaji”,alieleza.
Mapema
Mratibu wa mabaraza ya wazee kisiwani Pemba kutoka JUWAZA, Sifuni Ali Haji,
alisema waliamua kuwashawisha wazee, kuanzisha mabaraza hayo, ili wapate kutetea
haki zao wakiwa pamoja.
Alifafanua
kuwa, wazee wa Zanzibar kama walivyowazee wengine duniani kote, wanazo haki zao
mbali mbali ikiwemo wa matibabu, mitaji na kutoa maoni yao katika kuendesha
nchi, hivyo kupitia mabaraza hayo itakuwa rahisi.
“Mabaraza
haya ya wazee yana malengo mbali mbali, na kama wenyewe wakiyaendelea yanaweza kupiga hatua kubwa,
huku na sisi JUWAZA tukiwa bega kwa bega nayo”,alifafanua.
Shehia ya
Vitongoji wilaya ya Chakechake kisiwani Pemba, ina wazee 173 wenye umri wa
miaka 70, na wazee 180 wenye umri wa kuwanzia miaka 60 hadi 69, ambapo baraza
hilo la wazee lililoanzishwa mwaka jana linawanachama 15.
Katika ziara
hiyo ilioratibiwa na Jumuia ya wazee Zanzibar JUWAZA, ilianzia shehia ya Wingwi
mapofu na kumalizia shehia ya Vitongoji.
No comments:
Post a Comment