Habari za Punde

HESLB Yawakumbusha Waajiri Kuzingatia Sheria.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru (kushoto) akimkabidhi Mwakilishi wa Shule ya Msingi na Sekondari ya Academic Bi. Mariam Mtelesia ngao ya utambuzi wa ushirikiano wao katika kufanikisha kazi ya urejeshaji wa mikopo ya elimu ya juu kutoka kwa wanufaika ambao ni wafanyakazi katika taasisi yao
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru akiongea leo (Jumatatu, Februari 19, 2018) jijini Dar es Salaam katika hafla ya kuwakabidhi waajiri ngao za utambuzi wa ushirikiano wao katika kufanikisha kazi ya urejeshaji wa mikopo ya elimu ya juu kutoka kwa wanufaika wafanyakazi
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa EWURA Bw. Nzinyangwa Mchany (kulia) na Meneja Mawasiliano wa EWURA Bw. Titus Kaguo wakionesha ngao ya utambuzi walioyokabidhiwa leo (Jumatatu, Februari 19, 2018) jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru (kushoto) kutambua mchango wa taasisi katika urejeshaji mikopo ya elimu ya juu kutoka kwa wafanyakazi wanufaika EWURA
Mkurugenzi Msaidizi wa Urejeshaji Mikopo wa HESLB Bw. Phidelis Joseph akiongea leo (Jumatatu, Februari 19, 2018) jijini Dar es Salaam katika hafla ya kuwakabidhi waajiri ngao za utambuzi wa ushirikiano wao katika kufanikisha kazi ya urejeshaji wa mikopo ya elimu ya juu kutoka kwa wanufaika wafanyakazi.


·   Yatambua taasisi 15 zinazotimiza matakwa ya Sheria

·   Yaahidi kuwatembelea waajiri ili kuongeza uelewa wao

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) leo (Jumatatu, Februari 19, 2018) imewakumbusha waajiri nchini kote kuzingatia matakwa ya Sheria ya HESLB inayowataka kuwasilisha kwa HESLB orodha ya majina ya waajiriwa ambao ni wahitimu wa shahada au stashahada ili kuiwezesha Bodi kubaini wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu.

Aidha, Sheria hiyo inawataka waajiri kukata asilimia 15 ya mshahara ghafi wa mwajiriwa na kuwasilisha makato hayo kwa HESLB ndani ya siku 15 baada ya tarehe ya mwisho ya mwezi.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru leo (Jumatatu, Februari 19, 2018) jijini Dar es Salaam wakati wa hafla fupi ya kuwatambua baadhi ya waajiri wanaotimiza masharti ya Sheria ya HESLB. Hafla hiyo imefanyika katika ofisi za HESLB ambapo waajiri 15 walikabidhiwa ngao za kutambua mchango wao katika kuongeza ufanisi wa shughuli za HESLB hususan katika urejeshwaji wa mikopo.

Taasisi zilizotambuliwa
Taasisi zilizokabidhiwa ngao na Mkurugenzi Mtendaji ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PSPF), Benki ya NMB, Benki ya CRDB, Benki ya Stanbic, Deloitte Tanzania, Kampuni ya Sigara Tanzania, na Kamouni ya Coca Cola Kwanza. Kampuni nyingine ni Vodacom Tanzania, Nokia Solution Tanzania, Shule za Academic, Shule za Al-Hikma na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).

Taasisi nyingine za serikali ni Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Wizara ya Fedha ambao watakabidhiwa ngao zao mjini Dodoma hivi karibuni.

“Nyie ni wadau wetu muhimu sana. Tunavyosema tumeongeza makusanyo ya mikopo iliyoiva kutoka wastani wa TZS 2 bilioni kwa mwezi miaka mitatu iliyopita hadi wastani wa TZS 13 hivi sasa ni kwa sababu ya waajiri kama ninyi … tunawashukuru sana,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB katika hafla hiyo.

Kwa mujibu wa takwimu za HESLB, Benki za CRDB na NMB kwa pamoja ziliwasilisha kiasi cha TZS 274.4 milioni kama makato ya mikopo ya elimu ya juu kutoka kwa wafanyakazi wao kwa mwezi Disemba, 2017 pekee. Fedha hizi zinaweza kukopeshwa kwa wanafunzi 78 wa elimu ya juu kwa wastani wa TZS 3.5 milioni kwa mwaka ambazo hutolewa na HESLB hivi sasa.      

Bw. Badru ameongeza kuwa baadhi ya waajiri waliokabidhiwa ngao wameanzisha utaratibu nafuu ndani ya mashirika yao unaowawezesha waajiriwa wanaodaiwa mikopo ya elimu ya juu kuchukua hati ya deni HESLB na kulipa kwa mkupuo kwa uwezeshaji wa mwajiri.

Waajiri waliowawezesha wafanyakazi kumaliza madeni yao
“Hatua kama hizi za EWURA na Benki ya CRDB zinapaswa kuigwa na waajiri wengine kwa kuwa zinamsadia mfanyakazi na zinatuwezesha sisi kupata fedha haraka na hivyo kuwasomesha watanzania wengine wengi zaidi,” amesema Mkurugenzi Mtendaji huyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Urejeshaji Mikopo wa HESLB Bw. Phidelis Joseph amesema wataendelea kuwatembelea waajiri ili kubadilishana mawazo kwa lengo la kuongeza ufanisi na makusanyo.

“Ni wajibu wetu kuwafikia waajiri popote walipo ili kuwasikia na kubadilishana mawazo ili hatimaye tuwe na waajiri wengi zaidi wanaotimiza matakwa ya kisheria,” aliongeza.

HESLB ilianza kazi rasmi mwaka 2005 ili, pamoja na majukumu mengine, kutoa mikopo ya elimu ya juu kwa watanzania wahitaji na wenye sifa na kukusanya mikopo iliyoiva ambayo ilitolewa na Serikali tangu mwaka 1994/1995.

Waajiri wazungumza
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa ngao, Mwakilishi wa Nokia Solution Tanzania Bi. Doroth Namuhisa mara baada ya kuajiri, huchukua majina kamili ya mwajiriwa, jina la chuo alichosoma na namba kamili ya mtihani yenye mwaka aliofanya mtihani huo wa kidato cha nne na kuwasilisha HESLB ili wanufaika waweze kubainika.

“Tumejiwekea utaratibu wa kuwasilisha taarifa zote muhimu kwa Bodi ya Mikopo na ndiyo sababu hatupati changamoto kubwa,” alisema Bi. Namuhisa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Rasilimali Watu wa Benki ya Stanbic Bi. Eutropia Vegula ameipongeza HESLB kwa ushirikiano inaowapatia na kuongeza kuwa benki yake imeingiza matakwa ya Sheria ya HESLB katika sera yao ajira kwa kuhakikisha kila mwombaji kazi anafahamika kama ni mnufaika wa mikopo ya elimu ya juu au hapana.   

Imetolewa na:
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu

DAR ES SALAAM

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.