Habari za Punde

Wawakilishi Waombwa kushirikiana na Serikali kutambua kaya masikini majimboni mwao

Na Maryam Kidiko – Maelezo                                  

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Wabunge wameombwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ili kuhakikisha wanazitambua kaya masikini ndani ya majimbo yao na kuzisaidia.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto Mh. Shadia Muhamed Suleiman wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Konde Omar Seif Abeid aliyetaka kujuwa hatua zilizochukuliwa na Serikali kwa familia zenye Watoto wanaoishi katika mazingira magumu.

Amesema kutokana na wingi wa watoto wanaoishi katika mazingira magumu ni vyema Wawakilishi na Wabunge wazidishe mashirikiano yao katika kukabiliana na hali za watoto hao.

Amefahamisha kuwa hadi Disemba 2017 jumla ya watoto ishirini na mbili elfu, mia moja na arobaini na tatu (22,143) wameshatambuliwa na kusaidia misaada mbalimbali Unguja na Pemba.

Naibu Waziri huyo alizitaja misaada hiyo kuwa ni pamoja na kuunganishwa katika kupatiwa huduma mbalimbali kama vile Skuli, Afya, Ushauri nasaha kwa mujibu wa mahitaji ya Watoto.

Aidha Familia za Watoto wengine zimesaidiwa kwa njia ya kuanzishiwa miradi mbali mbali ya kiuchumi katika shehia zao ili ziwawawezesha kimaendeleo.

Alisema kuwa mbali na hayo pia wanapatiwa mafunzo ya ujasiria mali na kupatiwa mitaji midogo midogo kwa watoto husika ambao wanatambuliwa kisheria.

Aidha aliongeza kwa kusema Idara pia inasaidia baadhi ya kaya zinazotambuliwa katika shehia kwa kuwapatia pesa kila mwezi ili ziweze kusaidia kwa mahitaji madogo madogo.

Akifafanua kuhusu Shehia ambazo zimenufaika na hatua hiyo ya Serikali Naibu Shadia alisema ni pamoja na Shehia ya Wazee, Jangombe, Magomeni, Nyerere, Kidongo chekundu na Muembe makumbi.

Hata hivyo alisema watoto hao hutambuliwa katika shehia husika ambapo kamati huundwa na kupewa mafunzo maalum ambayo huwasaidia kujuwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu.

Kamati hizo hupewa mafunzo ya siku mbili hadi nne ya jinsi ya kuwatambua na kuwasajili watoto wa shehia husika kwa kutumia mwongozo ulioandaliwa kwa mashirikiano na wadau.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.