Habari za Punde

Bei mpya za mafuta kuanza kutumika kesho

 Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) Hassan Juma Amuor akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu mabadiliko ya bei za mafuta .
Waandishi wa habari  wakiwa katika mkutano ulioandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati (ZURA) huko Maisara Zanzibar kuhusu mabadiliko ya  bei mpya za mafuta  (Picha na Kijakazi Abdalla Maelezo)

Na Kijakazi Abdalla .Maelezo Zanzibar.    
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) imetangaza bei mpya ya mafuta ambayo itaanza kutumika kesho Jumanne 13/03/2018.
Akizungumza na Waandishi wa habari Afisa Uhusiano wa  Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati(ZURA) Hassan Juma Amuor amesema kuwa  Zura imetangaza bei  mpya kwa kuzingatia mambo yafuatayo.
Alisema kuwa wastani wa mwenendo wa mabadiliko ya bei za mafuta duniani,thamani ya shilingi ,gharama za usafiri ,kodi za Serikali pamoja na kiwango cha faida kwa wauzaji wa jumla na rejareja.
Aidha alisema kuwa bei hizo Petroli kwa mwezi wa Machi 2018 imepanda kwa shilingi moja(1)kwa lita kutoka shilingi 2,256 hadi kuwa shilingi 2,257 sawa na ongezeko la asilimia 0.04%.
Bei ya mafuta ya Dizeli kwa mwezi wa Machi .2018 imepanda kwa shilingi(68)kwa lita kutoka shilingi 2,175 hadi kuwa shilingi 2,243 sawa na asilimia 3%.
Pia Afisa Uhusiano huyo alisema  bei ya Mafuta ya taa kwa mwezi wa Machi.2018 imepanda kwa shilingi (5) kwa lita kutoka shilingi 1,641 hadi shilingi 1,646 sawa na ongezeko la asilimia 0.3%.
Vilevile alisema kuwa bei ya mafuta ya Banka kwa mwezi wa Machi 2018 imepanda kwa shilingi (68) kwa lita kutoka shilingi 2,017 hadi shilingi 2,085 sawa na ongezeko la asilimia 3%.
Hata hivyo alisema kuwa bei ya Mafuta ya Ndege (Jet A-1) kwa mwezi wa Machi 2018 imeshuka kwa shilingi 4.46 kwa lita kutoka shilingi 1,811.80 hadi shilingi 1,807.34 sawa na upungufu wa asilimia 0.24%.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.