Habari za Punde

Viongozi wa Baraza la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar Watembelea Ujenzi wa Skuli Kuangalia Mahitaji ya Watu Wenye Ulemavu Katika Ujenzi Huo.

Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la watu wenye Ulemavu Mzee Haidar Hisham Madowea katikati akiongoza ujumbe wa maafisa wa Watu wenye ulemavu walipokuwa kwenye msafara wa kuzitembelea skuli tano za ghorofa zinazojengwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mkopo kutoka Opec Fund.
Mwalimu Khalifa Rashidi (kulia) ambae ni Mjumbe wa Baraza la Taifa la watu wenye Ulemavu kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, akiwa katika ziara ya kutembelea majengo ya Skuli za Ghorafa zinazoendelea kujengwa katika maeneo ya Skuli ya Muembeshauri, Fuoni, Chumbuni, Bububu na Kinuni, kushoto ni Abushiri Saidi Khatibu Afisa Mipango wa Idara ya watu wenye Ulemavu Zanzibar
Mkandarasi wa Ujenzi  wa jengo la Skuli ya Mwembeshauri  Frances Kitupa akitoa maelezo kwa viongozi wa Baraza la Taifa la watu wenye Ulemavu Zanzibar walipofanya ziara ya kuangalia miondombinu rafiki kwa watu  hao
Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la watu wenye Ulemavu Mzee Haidar Hisham Madowea (mwenye Kaunda suti) akiangalia michoro ya Ramp na maafisa kutoka Idara ya Watu wenye ulemavu walipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa skuli tano za ghorofa zinazojengwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mkopo kutoka Opec Fund.
 Picha na Miza Othman-Maelezo Zanzibar.

Na Takdir Ali-Maelezo Zanzibar. 08-03-2018.
Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu Zanzibar limeziomba taasisi za kiserikali na binafsi zinazojenga majengo ya umma kuzingatia mahitaji ya Watu wenye ulemavu wakati wa ujenzi ili kuepuka usumbufu wanaoupata wanapotafuta huduma katika majengo hayo.

Hayo yameelezwa na mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watu wenye ulemavu Zanzibar Haidar Hisham Madowea wakati alipofanya ziara  ya kuangalia skuli tano zinazojengwa na serikali ya mapinduzi ya Zanzibar kwa msaada wa serikali ya Jamuhuri ya watu wa China.

Amesema watu wenye ulemavu wamekuwa wakipata usumbufu kutokana na baadhi ya majengo yanayojengwa kutozingatia masuala yao na kupelekea kutofikia malengo waliojipangia.

Januari Fusi ni mjumbe wa Baraza hilo kwa niaba ya katibu mkuu wa wizara ya kazi,uwezeshaji wanawake,wazee na watoto amesema wamefanya ziara hiyo kwa lengo la kuangalia na kuhajkikisha vigenzo vilivyowekwa na serikali juu ya mazingatio ya watu wenye ulemavu vinazingatiwa katika ujenzi kama vile Hospitali na skuli.

Amesema kwa kiasi kikubwa mazingatio juu ya mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu yamezingatiwa lakini kumegundulika kasoro ndogo ndogo ambazo zinahitaji marekebisho ikiwemo vipimo vya vyoo ambavyo vinatakiwa viwe na upana maalum unaokidhi mahitaji ya watu hao.

Hata hivyo amesema wamewaelekeza Wakandarasi hao kuhusiana na changamoto hiyo na wamekubali kuzifanyia marekebisho ya haraka.

Kwa upande wake mwalimu Halifa Rashidi kwa niaba ya katibu mkuu wa wizara ya elimu na mafunzo ya amali Zanzibar amesema ziara hiyo imeleta manufaa kwani wameifanya mapema ili kuweza kugunduwa zile kasoro ndogo zilizizojitokeza na kuweza kupatiwa ufumbuzi.

Amefafanuwa kuwa wamekuwa wakipata usumbufu mkubwa ikiwemo ya kufikia juu ya baadhi ya majengo kutafuta huduma jambo ambalo ni kinyume na utaratibu wa serikali katika kunyanyua na kupigania haki za watu wenye ulemavu Zanzibar.

Francis Kitupa ambae ni mkandarasi wa ujenzi wa baadhi ya skuli zinazojengwa amesema ujio wa uongozi wa baraza la taifa la watu wenye ulemavu umeweza kuwapa mwamko wa kufahamu masuala mbali mbali yanayowahusu watu wenye ulemavu kwani hapo awali walikuwa hawayafahamu.

Katika ujenzi wao wamekuwa wakizingatia masuala ya watu wenye ulemavu ikiwemo kuweka ramp zitazako wawezesha Wanafunzi wenye mahitaji maalum kuyafikia kwa urahisi bila usumbufu wowote.

Baraza la Taifa la watu wenye ulemavu limefanya ziara katika skuli za sekondari za  Muembeshauri,Fuoni,Chumbuni,Bububu na Kinuni ili kuweza kuhakikisha watu wenye ulemavu wanasoma katika mazingira mazuri kama wanafuzi wengine.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.