Habari za Punde

Dkt. Akwilapo Azindua Baraza la Wafanyakazi HESLB · Asema ufanisi umeongezeka, malalamiko ya wanafunzi yamepungua · Makusanyo yaongezeka kutoka Tshs 28bn mwaka 2015/2016 hadi Tshs 130 mwaka huu · Awakumbusha kusimamia uadilifu, kuimarisha ushirikiano

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru akiongea katika mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB). Kulia kwake ni Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi (RAAWU), Tawi la HESLB Bw. Deo Mwiliko na kushoto ni Katibu wa Baraza hilo Bi. Sara Fihavango.
Mjumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Bw. Venance Ntiyalundura akiongea katika mkutano wa baraza hilo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo (katikati walioketi) katika picha ya pamoja na wajumbe na waalikwa kwenye mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB). 

Na Eline Maronga, HESLB.Bagamoyo. Juni 1, 2018
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo leo (Ijumaa, Juni 1, 2018)amefungua mkutano wa siku moja wa Baraza la Wafanyakazi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) uliofanyika mjini Bagamoyo na kuwataka watumishi kuzingatia uadilifu na kuimarisha ushirikiano katika utendaji kazi wao.
“Baraza la Wafanyakazi mahali pa kazi lina wajibu mkubwa wa kuhakikisha kunakuwepo maelewano, ushirikiano na mshikamano kati ya wafanyakazi na uongozi,” amesema Dkt. Akwilapo katika mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo.

Ameongeza kuwa Baraza lihakikishe kunawepo na nidhamu ya kazi kwa madhumuni ya kuleta tija na ufanisi katika uendeshaji wa shughuli za HESLB ili kuhakikisha malengo ya Serikali kuanzisha HESLB yanafikiwa kwa ufanisi mkubwa.

Pamoja na wito huo, Dkt. Akwilapo pia amewapongeza watumishi wa HESLB kwa kutekeleza majukumu yao ya kutoa na kukusanya mikopo ya elimu ya juu kwa ufanisi.
“Mmekuwa mkifanya kazi kwa bidii na kutoa taarifa kwa umma na hivyo kupunguza malalamiko kwa kuwa wananchi wanaelewa mnachokifanya,” amesema Katibu Mkuu.
Awali akimkaribisha Dkt. Akwilapo, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru amesema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Serikali kupitia HESLB imefanikiwa kuongeza idadi ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanaokopeshwa kutoka wanafunzi 28,383 mwaka 2016/2017 hadi wanafunzi 33,941 mwaka huu wa masmo 2017/2018.

Kuhusu urejeshaji wa mikopo iliyoiva, Bw. Badru amesema kasi ya kukusanya fedha za mikopo iliyoiva kutoka kwa wanufaika nayo imeongezeka kwa kiasi kikubwa.

“Mwaka 2015/2016 tulikusanya TShs 28bn na makusanyo hayo yameongezeka hadi kufikia Tshs 130bn katika miezi tisa tu ya mwaka wa fedha 2017/2018, yaani Julai 2017 hadi Machi, mwaka huu,” amesema Bw. Badru.

Kuhusu malengo kwa mwaka 2018/2019, Bw. Badru amesema Serikali imetenga Tshs 427bn kwa ajili ya kuwakopesha wanafunzi wa mwaka wa kwanza wapatao 40,000 na wanaoendelea na masomo zaidi ya 80,000.

Aidha, HESLB inakamilisha taratibu za kuanza kutoa mikopo kwa wanafunzi wa stashahada (Diploma) mbalimbali katika utaratibu ambao utatangazwa mwishoni mwa mwezi Juni, 2018.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Dkt. Dalmas Nyaoro, Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya HESLB, Menejimenti na wawakilishi wa Idara na Vitengo vya HESLB.

HESLB ilianzishwa mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi mwezi Julai 2005 ili kutoa mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi watanzania wasio na uwezo na pia kukusanya mikopo iliyoiva iliyotolewa na Serikali tangu mwaka 1994/1995.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.