Habari za Punde

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa CCM Mhe. Balozi Seif Ali Iddi. Afungua Kongamano la Uporomokaji wa Maadili.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Wanakongamano kuhusu kuporomoka kwa mmong’onyoko wa maadili kwa Watanzania hapo Ofisi ya CCM Mkoa Kaskazini iliyopo Mahonda.
Mapema Katibu waJumuiya ya Wazazi ya Wilaya ya Kaskazini “B” Bibi Salma Shaib akitoa Taarifa ya Kongamano hilo kabla ya kufunguliwa rasmi na Balozi Seif.
Balozi Seif akilifunguwa Kongamano  kuhusu kuporomoka kwa mmong’onyoko wa maadili kwa Watanzania hapo Ofisi ya CCM Mkoa Kaskazini iliyopo Mahonda.
Baadhi ya washiriki wa Kongamano  kuhusu kuporomoka kwa mmong’onyoko wa maadili kwa Watanzania hapo Ofisi ya CCM Mkoa Kaskazini iliyopo Mahonda.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis.OMPR. 
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi alisema Jamii inaweza kuondoa au kupunguza uporomokaji wa maadhili ndani ya Familia na Taifa iwapo Wanajamii wenyewe watakubali kuelimishana na kufuata maadili yaliyotokana na wazazi pamoja na Viongozi wa Dini.
Alisema Serikali kwa upande wake iliamua kwa makusudi kutoa fursa kwa Vijana wanapomaliza Elimu yao kujiunga na Jeshi la Kujenga Uchumi {JKU} na Jeshi la Kujenga Taifa {JKT} ili kujenga misingi imara ya maadili ya Taifa kwa Vijana hapa Nchini.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akilifungua Kongamano la siku moja kuhusu uporomokaji wa Maadili katika Jamii ya Watanzania lililoandaliwa na Jumuiya ya Wazazi ya CCM Wilaya ya Kaskazini “B” na kufanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa CCM Mkoa uliopo Mahonda Mkoa Kaskazini Unguja.
Alisema ni jambo la kusikitisha kuona kwamba malezi ya sasa yamevamiwa na Virusi vya maendeleo ya sayansi na Teknolojia, usawa, propaganda za Matafa ya Magharibi pamoja na kupungua kwa Imani za Dini katika Jamii.
Balozi Seif alisema maendeleo haya yamemuwezesha Mtanzania kuwa na uwezo  mkubwa wa kuona na kufuatilia matukio mbali mbali yanayotokea  Ulimwenguni kwa kutumia simu za Viganjani au Kompyuta.
Alisema simu hizo zilizounganishwa na mitandao ya Kijamii kama Face book  na Whatsup hivi sasa zimechukuwa  nafasi kubwa ya kuwafunda vijana badala ya kazi hiyo kuendelea  kufanywa na Wazazi wenyewe.
Alieleza hatua ya mitandao hiyo inamuwezesha Kijana kuangalia mambo mengi ikiwemo vitendo vinavyokwenda kinyume na silka, mila na Tamaduni za Taifa ambazo ni kinyume na Maadili ya Mtanzania badala ya kuangalia yale yanayompasa kumsaidia katika kujipanga Kimaisha zaidi.
Balozi Seif alifahamisha kwamba usawa au kwa lugha nyengine kwenda na wakati kunachangia mmong’onyoko wa maadili ya Mtanzania jambo ambalo hupelekea vijana wengi kujiingiza kwenye vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa Mali za Umma.
Hata hivyo Balozi alieleza pia kwamba Utamaduni wa Mataifa ya Magharibi umechukuwa nafasi kubwa ya kurithisha  Vijana wengi Nchini ambapo hupata muda wa kuiga Mila, Silka na Tamaduni za Nchi hizo na kufikiria ni safi kuliko zile za asili yao.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwakumbusha Wanakongamano hao ni vyema wakaelewa kuwa maadili na uadilifu ni vitu vinavyokwenda sambamba.
Alisema haiwezekani Jamii, Viongozi pamoja na Taasisi za Kijamii zikazungumzia maadili bila ya kugusa suala la uadilifu ili wahusika wafikie pahala pa wao wenyewe kutendeana mema na kukatazama mabaya.
Balozi Sef alisema kwa vile Jamii bado haijaamua kukatazana suala la udhalilishaji pamoja na ubakaji kwa wanawake na watoto, hivyo wakati umefika kila aliyebeba dhima ya malezi kujikita katika kuiandaa Jamii iliyomzunguuka kujaribu kukataza vitendo hivyo ili wahusika waendelee kuishi kwa amani na upendo.
Alionyesha kukerwa kwake na Takwimu  kubwa zinazoonyesha kiwango kisichoridhisha  cha udhalilishaji wa kijinsia ndani ya Wilaya ya Kaskazini “B”  na Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa ujumla ambao unaooongoza kwa vitendo hivyo hivi sasa.
Alisema  hilo ni jambo la hatari linalodhalilisha Wilaya na Mkoa mbele ya Mikoa na Wilaya nyengine hapa Nchini ambapo wakati umefika sasa kwa Wazazi kuwaelekeza njia watoto wao ili kuepuka na changamoto hiyo inayoleta sura mbaya.
Alitahadharisha kwamba licha ya mchango mkubwa unaochukuliwa na Walimu wa Skuli na madrasa katika kuwafinyanga watoto lakini bado nguvu ya wazazi wenyewe zinapaswa kupewa kipaumbele katika malenzi ya maadili kwa watoto wao.
Mapema Katibu waJumuiya ya Wazazi ya Wilaya ya Kaskazini “B” Bibi Salma Shaib alisema Kongamano hilolililoshirikisha Masheha, Madiwani, Walimu wa Wakuu, Viongozi wa Kisiasa na Dini limefanyika kutokana na muongozo wa Jumuia ya Wazazi Ngazi ya Taifa.
Bibi Salma alisema Chama cha Mapinduzi kupitia Jumuiya hiyo kiliamua kuandliwa kwa Makongamano hayo yatakayotoa fursa kwa Kila Mwana Jamii kuchangia mbinu zitakazosaidia kurejesha Maadili ya Mtanzania yanayoonekana kutawaliwa zaidi na Utamaduni wa Kimagharibi.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Wanakongamano hao Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Kaskazini “B”ambae pia ni Mkuu wa Wilaya hiyo Nd. Rajab Ali Rajab alisema kuanzia sasa hakuna kitendo cha usuluhishi kitakachokubaliwa katika vitendo vya udhalilishaji ndani ya Wilaya hiyo.
Nd. Rajab alisema katika kupiga vita janga hilo Uongozi wa Wilaya hiyo umeshakaa na Masheha wa Shehia zilizomo ndani ya Wilaya hiyo na kupanga Mikakati ya kudhibiti wimbi hilo.
Alisema hatua hiyo imekuja kutokana na baadhi ya Masheha hao kuwa Majaji wa kutoa hukumu za matukio ya udhalilishaji wa kijinsia hasa matukio hayo yakiwakumba Watu wa Familia Moja jambo ambalo linachangia kukosesha haki ya Mtendewa.
Alieleza kwamba Taifa kupitia Serikali wakati wote katika mipango yake ya maendeleo inatafuta na kuandaa Jamii iliyo bora na upatikanaji wake unahitaji ushirikiano mkubwa wa pamoja katika ngazi zote kuanzia Familia hadi Taifa kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.