Habari za Punde

Serikali Kujenga Nyumba 400 za Askari Polisi








Na Mwandishi Wetu
Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni kumi kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za askari polisi kote nchini, ikiwa ni kukabiliana na changamoto ya makaazi ya askari na uchakavu wa vituo vya polisi ili kuwawezesha askari hao kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Hayo yamesemwa   na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni alipotembelea kijiji cha Makongoro wilaya ya Bunda mkoani Mara kuona changamoto wanazokutana nazo askari polisi katika kutekeleza majukumu yao ya ulinzi na usalama.
Alisema wizara iko katika mpango maalumu wa kuboresha makazi ya askari polisi nchini huku akitoa wito na nafasi kwa wadau wa maendeleo pia kujitokeza na kuunga mkono juhudi za Rais  Dk.John Magufuli kuboresha makazi ya askari polisi
“Katika kukabiliana na changamoto ya askari nchi nzima tayari tushaanza kujenga makazi ya askari wetu tukianza na nyumba za polisi Kusini Pemba na tutaendelea na ujenzi huo wa nyumba 400 katika mikoa mingine nchini na kutokana na hali niliyoiona hapa Bunda basi tutatoa kipaumbele hapa”Alisema Naibu Waziri Masauni
Akizungumza wakati wa ziara hiyo Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili, ametoa rai kwa wananchi kuhakikisha wanashirikiana na serikali katika ujenzi wa makazi ya askari polisi wilayani humo huku Mwenyekiti wa Kijiji hicho Mussa Masilu aliongeza  kuwa nyumba hizo ni chakavu na zinashusha hadhi ya Askari Polisi
Hadi sasa serikali imeshaanza taratibu za awali ikiwemo tathmini ya ujenzi wa nyumba hizo mia nne za askari polisi nchini ambapo mikoa mbalimbali itanufaika na  ujenzi huo utakaotekelezwa kwa awamu tofauti ukienda sambamba na ujenzi na ukarabati wa vituo vya polisi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.