Habari za Punde

Ujumbe wa Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu UAE Wakiendelea na Ziara Yao Kisiwani Pemba Kutembelea Sehemu Mbali Mbali Kuangalia Usehemu za Kuwekeza.


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,Mawasiliano na Usafirishaji Nd.Shomari Omar Shomari (wa pili kulia)pamoja na Viongozi wengine wakimsikiliza Nd.Ali Humaid Alderei(kushoto) kutoka Mfuko wa Maendeleo wa (Abudhabi Fund) katika Ujumbe wa Timu ya Wataalam kutoka Nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ulipofika kutembelea mradi wa Barabara ya Mkoani-Chakechake  Pemba leo kufuatia ziara ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein aliyoifanya (UAE) mwanzoni mwa mwaka huu
Mkurugenzi Idara ya Tiba  DK.Mohamed Dahoma alipokuwa akitoa maelezo kwa ujumbe wa timu ya wataalamu kutoka katika  Serikali ya Umoja wa Nchi za Kiarabu (UAE) wakati ulipofika kutembelea katika Hospitali ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba leo,kufuatia ziara ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika Nchi za UAE Mwanzoni kwa mwaka huo.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba Dk.Omar Issa(kushoto) alipokuwa akitoa maelezo kwa ujumbe wa timu ya wataalamu kutoka katika  Serikali ya Umoja wa Nchi za Kiarabu (UAE) wakati ulipofika kutembelea sehemu mbali mbali katika Hospitali ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba leo,kufuatia ziara ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika Nchi za UAE Mwanzoni kwa mwaka huo.
Afisa Mdhamini katika Wizara ya Kazi,uwezeshaji,Wazee,Wanawake na Watoto Pemba Nd,Khadija Khamis Rajab (kushoto) alipokuwa akitoa maelezo kwaMshauri wa Waziri wa Nchi Ushirikiano wa Kimataifa wa Serikali ya Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu (UAE)  Bibi Najla Al- Kaabi (katikati)akifuatana na ujumbe wa wataalamu kutoka Serikali ya Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu (UAE) uliotembelea kaaika Ushirika wa Wajasiriamali wa Kikundi cha Upendo Group Wete Pemba leo,[Picha na Ikulu.] 10/08/2018.


UJUMBE wa timu ya Wataalamu kutoka Serikali ya Nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) umepongeza mapokezi na ukarimu walioupata kutoka kwa wananchi na viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika ziara zao zote walizofanya Unguja na Pemba.

Akitoa pongezi hizo mara baada ya kumaliza ziara ya kutembelea maeneo mbali mbali kisiwani Pemba yakiwemo Barabara ya Chake Chake hadi Mkoani, Hospitali ya Abdalla Mzee, Bandari ya Mkoani,Hospitali ya Wete, Bandari ya Wete na kikundi cha Wajasiriamali cha Upendo cha mjini Wete, Mshauri wa Waziri wa Nchi Ushirikiano wa Kimataifa wa Serikali ya Nchi za Falme za Kiarabu Najla Al Kaabi aliyasema hayo katika uwanja wa ndege wa Pemba.

Katika maelezo yake Mshauri huyo wa Waziri wa Nchi Ushirikiano wa Kimataifa wa Serikali ya UAE, alieleza kuwa Wazanzibari wameonesha upendo mkubwa kwake pamoja na ujumbe aliofutana nao kutoka UAE, hivyo kuna kila sababu na wao kuonesha upendo wao katika kuhakikisha azma ya ziara yao hiyo inazaa matunda.

Alieleza kuwa ujumbe huo wa Wataalamu kutoka Serikali ya UAE ambao uko nchini umepata fursa nzuri ya kujionea maeneo ambayo yamo katika makubaliano yaliofikiwa kati ya UAE na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika ziara ya Dk. Shein aliyoifanya mwezi Januari mwaka huu katika nchi za Umoja huo.

Najla Al Kaabi, alieleza kuridhishwa kwao na juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta za kiuchumi na kijamii na kusisitiza azma ya Umoja wa nchi za (UAE) katika kuunga mkono juhudi hizo.

Aidha, Najma Al Kaabi alieleza kuvutiwa kwake na wajasiriamali wa kisiwani Pemba kwa jinsi wanavyopambana katika kujiimarisha kiuchumi na kujiendeleza katika maisha yao kwa kujiendeleza katisha shughuli mbali mbali zikiwemo ushoni.


Mkurugenzi Mkuu wa Masuala ya Taaluma katika Idara ya mambo ya Afya ya Abudhabi Dk. Ali AbdulKareem Al Obaidli kwa upande wake alisifu jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya na kueleza jinsi Serikali ilivyoweka mazingira mazuri ya huduma za afya baada ya kutembelea hospitali ya Wete na Hospitali ya Abdalla Mzee na kuwaona wananchi wanavyopata huduma hizo.

Dk. Ali Al Obaidli aliahidi kwamba atahakikisha Serikali ya Umoja wa Falme za Kirabu (UAE) inafanya jitihada za kuhakikisha inashirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya katika nyanja mbali mbali.

Akitoa shukurani kwa Ujumbe huo kwa kukamilisha ziara yao kisiwani Pemba na Unguja, Mshauri wa Rais Masuala ya Ushirikiano wa Kimataifa, Fedha na Uchumi Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa aliupongeza kwa kufanya kazi kubwa ya  kutembelea maeneo mbali mbali yalioanishwa katika ziara hiyo.

Pia, Balozi Ramia alisema kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa taarifa za kutosha juu ya utekelezaji wa miradi iliyoanishwa katika ziara hiyo hatua kwa hatua.

Aliahidi kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuimarisha uhusiano wa kidugu uliopo baina ya watu wa Zanzibar na ndugu zao wa Falme za Kiarabu hasa ikizingatiwa kuwa pande hizo mbili zina uhusiano na ushirikiano wa kihistoria.

Sambamba na hayo, Balozi Ramia alitumia fursa hiyo kuvipongeza vyombo vya habari vya Zanzibar na nje ya Zanzibar kwa kuitangaza vyema ziara ya ujumbe huo wa wataalamu kutoka Serikali ya Umoja wa Nchi za Falme ya Kiarabu (UAE) tokea ulipowasili.

Wataalamu hao wakiwa na wenyeji wao kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar walifanya ziara leo kisiwani Pemba na kupata fursa ya kutembelea maeneo mbali mbali kisiwani humo na kupata maelezo kutoka kwa viongozi husika kutoka sekta walizozitembelea.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.