BODI ya korosho Mkoa Tanga imeshauriwa kuzitumia taasisi za Kijeshi za
JKT Mgambo na JKT Maramba ili ziweze kusaidia katika mchakato wa
uzalishaji wa miche ya mimea hiyo ya korosho.
Hayo yamezungumzwa na Mkuu wa Mkoa Tanga Martin Shigella kwenye mkutano
wa wadau wa zao la korosho uliokuwa na lengo la kujadili maendeleo ya
Tasnia ya zao la korosho kwa kipindi cha msimu wa miaka mitatu.
Shigella alisema ili bodi hiyo iweza kukabiliana na uhaba wa miche
katika Halmashauri zinazolima zao hilo lazima ifike wakati taasisi hizo
ziweze kutumika kukabidhiwa mbegu kwa ajili ya kuzalisha miche hiyo.
“Jaribuni kuwasiliana na taasisi hizio za kijeshi ambazo wanawataalamu
wa kuandaa vitalu wanaweza kuwasaidia kuzalisha miche mingi na iliyo na
ubora unaotakiwa”Alisema Shigella.
Mbali na hilo pia alizitaka Halmashauri zote zinazolima zao hilo
kuhakikisha zinatenga bajeti mapema ndani ya mwezi huu wa Sept kwa ajili
ya ununuzi wa mbegu toka katika Taasisi ya Utafiti wa
kilimo(Naliendele) kwa ajili ya uzalishaji wa miche ambayo inatarajiwa
kusambazwa mwakani kwa wakulima wote
Awali akizungumzi suala hilo Meneja Bodi ya korosho Kanda ya Kaskazini
Mashariki Ugumba Kilasa alikiri umuhimu wa kuzitumia taasisi hizo
kutokana na na uhaba wa fedha zilizokuwa zinatumika kuvilipa vikundi
vinavyozalisha miche hiyo.
Kilasa alisema lengo ni mjadala wa kuongeza uzalishaji wa zao hilo
Mkoani hapa na ongezeko hilo lazima liendende sambamba na uwepo wa miche
mipya,bora na ya kisasa jambo ambalo ikiwa kutaanzishwa vitalu vya
kukuzia miche na taasisi hizo hali ya uzalishaji inaweza kubadilika.
“Awali tulikuwa na vikundi vya vijana tuliokuwa tunawatumia kuzalisha
miche hiyo na tulikuwa tunawalipa lakini kutokana na ufinyu wa fedha ni
bora tutumie taasisi hizo za JKT zitatusaidia”Alisema Kilasa.
Alisema mikakati endelevu ifanyike ili kuhakikisha ongezeko la
uzalishaji linakuwepo hasa kwa kupanda miche mipya itakayoweza kuzaa kwa
wingi na kuongeza uchumi wa mkulima mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla
Nae Mrajisi Msaidizi vyama vya Ushirika Mkoa Tanga Jacklin Senzige
alisema kweli lipo tatizo la upatikanaji wa pembejeo kwa wakati jambo
ambalo linaweza kukwamisha usambazaji wake kwa wakulima na kuathiri
uzalishaji kwa ujumla.
Alisema uzalishaji wa Korosho mkoani
Tanga umeshuka kutoka tani 1712 mwaka 2016/2017 hadi kufikia tani 1381
mwaka 2017/2018 hali iliyosababishwa na mvua za mfululizo zilizonyesha
kwa kipindi kirefu na kusababisha maua kudondoka na kuozesha matunda.
No comments:
Post a Comment