Habari za Punde

China Kudumisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo

Naibu Waziri Mkuu wa China Bwana Han Zheing Kulia akimkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na Ujumbe wake katika Makaazi ya Wageni mashururi wa Kimataifa  {Villa 7} Mjini Nanning Jimbo la Guangxi kabla ya kuanza mazungumzo yao.
Ujumbe wa Tanzania kushoto ukifanya mazungumzo na Ujumbe wa Serikali ya China katika Makaazi ya Wageni mashururi wa Kimataifa  {Villa 7 }Mjini Nanning Jimbo la Guangxi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kulia akisalimiana na Katibu wa Chama cha Kikoministi cha China  { CCCP} Jimbo la Guangxi Bwana Lu Xinshe kulia kabla ya kuanza mazungumzo yao Mjini Nanning.
Katibu wa Chama cha Kikoministi cha China  { CCCP} Jimbo la Guangxi Bwana Lu Xinshe akisisitiza umuhimu wa China kuendelea kuiunga mkono Tanzania kutoka na Historia ya Nchi hizo mbili.  Picha na – OMPR – ZNZ.


 Na.Othman Khamis OMPR.
 Jamuhuri ya Watu wa China itaendelea  kuzingatia nafasi ya Tanzania katika kudumisha uhusiano wake wa Kiuchumi, Maendeleo na Ustawi wa Kijamii kutokana na ushirikiano wa pande hizo mbili  uliolenga kusaidia Nchi changa katika Mpango wake wa Kushirikiana kwa karibu zaidi na Mataifa ya Bara la Afrika.

 Naibu Waziri Mkuu wa China Bwana Han Zheing alitoa kauli hiyo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na Ujumbe wake hapo katika Makaazi ya Wageni mashururi wa Kimataifa      {Villa 7 }Mjini Nanning  katika Jimbo la Guangxi.

Bwana Han Zheng alisema uhusiano wa Bara la Afrika  na China, ambapo Tanzania ikipewa nafasi na fursa maalum unazidi kuimarika kila siku lengo likizingatiwa katika mafungamano ya Kiuchumi yatayoweza kuboresha Maisha na ustawi wa Watu wake.

Naibu Waziri Mkuu huyo wa China alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Kiongozi wa Taifa hilo Bwana Xi Jimping alifanya ziara maalum na ya upendeleo Nchini Tanzania mara tu baada ya kuchaguliwa kuliongoza Taifa hilo kubwa Barani Asia Mwaka 2013 kufuatia Historia ndefu ya pande hizo mbili.

Alisema Wananchi na hasa watu wa Mataifa hayo wameanza kushirikiana katika masuala mbali mbali akitolea mfano muingiliano wa Kibiashara, Utamaduni na hata harakati za ujenzi wa Miundombinu kasi inayokwenda kwa haraka sana.

Naye kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Tanzania sambamba na Zanzibar kwa ujumla zimekuwa zikipiga hatua kubwa na ya haraka ya Maendeleo ya Kiuchumi na Ustawi wa Jamii kutokana na nguvu kubwa ya kuungwa mkono na ndgugu zao wa China.

Balozi Seif alisema China bado itabakia kuwa rafiki wa kweli wa Tanzania kutokana na kitendo cha Nchi hiyo kujitolewa kwa nguvu zake kusaidia Miradi ya Kiuchumi ikionyesha uthibitisho wa mapenzi yake thabiti kwa Tanzania.

Alisema jumuia za Kimataifa wakiwemo pia Wananchi wa kawaida wamekuwa wakishuhudia kasi hiyo ya China iliyoelekeza Tanzania ambaye ni mshirika wake mkuu aliyetokana na Waasisi wa Mataifa hayo Mawili.

Alieleza kwamba Miradi ya Ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar, matayarisho ya Ujenzi wa Bandari Kuu ya Mizigo katika eneo la Mpiga Duri ni miongoni mwa Miradi hiyo inayosukumwa na Serikali ya China kupitia mfumo wa Mikopo nafuu na misaada.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliendelea kuipongeza na Kuishukuru Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China na Wananchi wake kwa juhudi wanazochukuwa za kuiunga mkono Tanzania iliyojitayarisha kuingia katika uchumi wa kati ifikapo Mwaka 2025.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikutana kwa mazungumzo na Katibu wa Chama cha Kikoministi cha China{ CCCP} Jimbo la Guangxi Bwana Lu Xinshe kwenye Ukumbi wa Nyumba ya Watu mashuhuri aliyofikia ya Villa 7 Mjini Nanning.

Katika mazungumzo yao Bwana Lu Xinshe alimueleza Balozi Seif  kwamba upo umuhimu wa Mataifa hayo rafiki kuangalia zaidi maeneo mengine ya ushirikiano katika nyanja za Kiuchumi ili kunawirisha uhusiano wa Kihistoria uliopo kati ya Tanzania na China.

Alisema licha ya uhusiano huo kwa sasa kujikita zaidi katika masuala ya Siasa na Utawala lakini bado ipo nafasi ya kuongeza kasi ya pamoja katika Sekta za Utamaduni, Elimu,, Utalii sambamba na Miundombinu kwa kuzingatia zaidi malengo ya baadae.

Naye kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliipongeza Serikali na Wananchi wa Taifa la China kwa hatua kubwa waliyopiga kuelekea kwenye Maendeleo ya Kiuchumi na Teknolojia ya Kisasa.

Balozi Seif alisema  yapo mabadiliko makubwa ya Kiuchumi ndani ya Majimbo ya Taifa hilo akalitolea mfano hili la Guangxi  ambalo limebobea katika Sekta ya Kilimo na Mazingira kwa kutumia mfumo wa Teknolojia ya Kisasa.

Alisema Jimbo la Guangxi lililobeba Mji wa Nanning uliozunguukwa na kijani ambalo Wananchi wake wanaweza kuelekeza nguvu na Taaluma zao katika kuwasaidia Ndugu zao Watanzania na Zanzibar kwa ujumla.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimfahamisha Katibu huyo wa Chama cha Kikoministi cha China Jimbo la Guangxi kwamba Wataalamu na Wawekezaji wa Jimbo hilo wana fursa ya kulitumia soko la Tanzania katika uwekezaji kwenye Sekta na miradi ya Utalii, Kilimo, Uvuvi na Vyuo Vikuu.

Alisema Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilmali nyingi za kuvutia Wawekezaji akazitolea mfano Fukwe mwanyanya za kuvutia, mbuga za Wanyama, Kilimo cha Miwa  pamoja na misitu ya asili.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.