Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi Akiweka Jiwe la Msingi Skuli ya Maandalizi Maziwang’ombe Mkoa wa Kaskazini Pemba

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi akifungua pazia kuashiria kuweka jiwe la msingi la Skuli ya Maandalizi ya Maziwang’ombe iliyopo Micheweni Mkoa Kaskazini Pemba.(Picha na OMPR) 

Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Jamii inalazimika kuwaandaliwa Elimu ya Maandalizi Watoto kwa lengo la kuwajengea msingi mzuri utakaowawezesha kuingia kwa kujiamini katika elimu ya sekondari na vyuo hatimae kuwa Watumishi bofa walioelimika vyema.
Alisema Taifa linahitaji Wataalamu Wazalendo watakaoivusha Nchi hii katika mpito wa kuingia katika mabadiliko makubwa ya Sayansi na Teknolojia yaliyoukumba ulimwengu katika Miaka ya sasa.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akisalimiana na Wananchi, Walimu na Wanafunzi wa Mazinwang’ombe baada ya kuweka Jiwe la Msingi la Skuli ya Maandalizi ya Maziwang’ombe Mkoa wa Kaskazini Pemba akiwa katika ziara ya siku Tano Kisiwani humo.
Alisema vitendo vya baadhi ya Wazazi kwa kushirikiana na wadau wa Elimu kuwajengea mazingira bora watoto wao ikuwemo Majengo ya Kisasa kinapaswa kuungwa mkono na kila mkereketwa wa Sekta ya Elimu Nchini na hata washirika wa maendeleo wa Kimataifa.
Balozi Seif  alieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepania kuwasaidia Vijana wake ndio maana ikaweka Elimu bila ya malipo kulikotangazwa na Rais wa kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Aman Karume Mnamo Tarehe 23 Septemba 1967.
Aliwatahadharisha Walimu Maskulini kuacha kuwachangisha fedha Wanafunzi kwa Vile Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imesharejea tena kubeba mzigo wa kugharamia Elimu Maskulini.
Alisema kazi iliopo kwa Wanafunzi ni kusoma kwa bidii ili zile jitihada zinazochukuliwa na Viongozi, Wazazi na Taasisi za Kijamii katika kuunga mkono Sekta ya Elimu zinaleta matunda.
Balozi Seif  alieleza kwamba Serikali imetoa fursa kwa Wanafunzi wasome hadi upeo wa uwezo wao iwe sekondari au chuo kikuu na utaratibu umeshaandaliwa wa kuongeza nafasi ya udhamini kwa wanafunzi wanaoendelea na masomo yao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar katika ziara yake hiyo aliwaomba Wananchi wa Micheweni wanaoishi pembezoni mwa chuo cha  Kiisalmu kuacha ubabe wa kuzuia ujenzi wa uzio wa Chuo hicho.
Alisema ni vyema kwa Wananchi hao wakaridhia Maamuzi ya Serikali yaliyopelekea  kujenga Chuo hicho katika kuwajengea uwezo wa Kielimu watoto wa Taifa hili ili ukuta huo usaidie kuzuia uharibifu wa Mali za Chuo.
Balozi Seif alitahadharisha kwamba Ardhi ni mali ya Serikali kama ilivyoainishwa katika  Sheria sita zinazosimamia Ardhi ambapo pale inapohitaji kuitumia kwa shughuli za Kijamii ina wajibu wa kufanya hivyo.
“ Mwananchi hapaswi kung’ang’ania Ardhi mahali popote pale ambapo Serikali imeshaamua na kupanga kuitumia kwa shughuli za Kijamii”. Alisisitiza Balozi Seif.
Mapema Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Riziki Pembe Juma  aliipongeza Jumuiya ya Pemba Foundation kwa kushirikiana na Mwakilishi wa Jimba la Micheweni Mh. Shamata kwa uzalendo wao uliopelekea kuunga mkono Sekta ya Elimu.
Mh. Riziki alisema jitihada zao za kuongeza ujenzi wa  madarasa ya Skuli zimesaidia kupunguza ufinyu wa Madarasa wakizingatia uwekezaji katika Sekta ya Elimu ambao ni jambo la msingi katika kujenga Taifa litaloelimika.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali aliwaomba na kuwahimiza Wafanyabiashara wengine Nchini kuiga mfano ulioonyeshwa na Pemba Foundation na Mwakilishi wa Jimbo la Micheweni wa kuekeza katika Sekta hiyo muhimu.
Balozi Seif katika ziara hiyo alipata fursa ya kukagua maendeleo ya Ujenzi wa Madarasa Sita ya Chuo cha Kiislamu Micheweni na kuridhika na hatua iliyofikiwa na baadae kutoa zawadi kwa Wanafunzi wa Skuli ya Msingi ya Micheweni pamoja na Vifaa vya Afya kwa Hospitali ya Wilaya ya Micheweni ulitolewa na Mfanyabiashara Mzalendo Said Naaser Boopar.
Akizungumza na Walimu, Wamanchi na Wanafunzi wa Wilaya hiyo Balozi Seif  alimshukuru na kumpongeza Mfanyabiashara Said Naaser Boopar kwa uzalendo wake uliomshawishi kuunga mkono Sekta ya Elimu na Afya ambayo ni Sekta pacha.
Akitoa salamu Mfanyabiashara Mzalendo Said Naaser Boopar alisema amehamasika kuendelea kutoa misaada ya Kijamii kutokana na ushirikiano mkubwa anaoupata kutoka kwa Viongozi wa Serikali pamoja na wale wa Kijamii.
Boopar alisema hatua hiyo kwa vile imetokana na nguvu ya Jamii iliyopmzunguuka ameahidi kuiendeleza kadri ya hali na nguvu za Kibiashara zitakavyoongezeka zaidi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar katika ziara hiyo alipata fursa ya kukabidhi zawadi kwa Wanafunzi wa skuli ya Msingi ya Micheweni zilizotolewa na Mfanyabiashara Mzalendo Said Naaser Boopar.
Zawadi hizo ambazo ni pamoja na mikoba, Mashungi, Penseli na Kampasi zinatokana na ahadi aliyoitoa karibu Miezi Mitatu iliyopita wakati wa Haflya ya kukabidhi mchango wa Vikalio kwa madarasa ya Skuli hiyo ya Msingi iliopo ndani ya Wilaya ya Micheweni Mkoa Kaskazini Pemba.
Msaada huo ulikwenda sambamba na utolewaji wa Vifaa mbali mbali ya Afya kwa ajili ya kuhudumia Wagonjwa wa Hospitali ya Wilaya ya Micheweni .
Baadae Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akatoa zawadi za Kompyuta kwa Skuli Nane zambazo wanafunzi wake wamefanya vyema katika Mitihani yao ya Taifa ya Darasa la 14 Mwaka 2017.
Hafla hiyo fupi ailiyohudhuria pia na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya  Amali Zanzibar Mh. Riziki Pembe Juma ilifanyika katika Ukumbi wa Kiwanda cha Makonyo Wawi Chake chake Pemba.
Skuli zilizofanikiwa kupata zawadi hizo ni pamoja na Chuo cha Kiislamu cha Micheweni, Utaani,, Chasasa na Mchangamdogo kwa Mkoa wa Kaskazini Opemba na Skuli za Castro, Shamiani, Uweleni na Madungu kwa Mkoa wa Kusini Pemba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.