Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akihutubia katika hafla ya Utiaji wa Saini ya Mkataba wa Mgao wa Uzalishaji wa Mafuta na Gesi Asilia, baada ya utiiji wa saini hiyo pia alihudhuria Mtawala wa Ras Al Rakhaimah Sheikh Saud Bin Saqr Al Qasim na Viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, hafla hiyo imefanyika katika viwanja vya Ikulu Zanzibar.23/10/2018.
MALENGO ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni
kuhakikisha kuwa faida zitakazopatikana kutokana na rasilimali ya mafuta na
gesi asilia zinachangia katika ukuaji wa uchumi na zinawanufaisha wananchi wote
bila ya kuwatenga na kuwabagua wengine.
Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ameyasema hayo leo katika
viwanja vya Ikulu Mjini Zanzibar katika hafla ya Utiaji Saini Mkataba wa
Mgawanyo wa Uzalishaji wa Mafuta na Gesi Asilia, hafla iliyofanyika katika
viwanja vya Ikulu mjini Zanzibar ambayo ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
na viongozi kutoka Ras al Khaimah.
Katika hafla hiyo ambayo
mapema Rais Dk. Shein na mgeni wake Shaikh Saud Bin Saqr Al Qasimi, Mtawala wa
Ras Al Khaimah walishuhudia utiaji saini wa Mkataba huo, aliwahimiza wananchi
waendelee kushirikiana na kuimarisha umoja na mshikamano ili kuweza kupata
mafanikio yanayotarajiwa.
Dk. Shein alisema kuwa
suala la utafutaji wa mafuta na gesi asilia ni jambo linalohusu maendeleo ya
Zanzibar na kamwe halitakiwi lilete mfarakano katika jamii na badala yake
linatakiwa liwaunganishe wananchi.
Aliwataka wananchi
kujiepusha na watu wachache ambao wameamua kulitumia jambo hilo kuwa ajenda ya
kuwagawa watu jambo ambalo ni kinyume na malengo ya Serikali ya kuzishughulikia
rasilimali hizo.
Aidha, Rais Dk. Shein
aliendelea kuwahimiza wananchi wa Zanzibar wawe na subira kwa kutambua kwamba
suala la utafutaji wa mafuta na gesi asilia ni kazi inayochukua muda mrefu.
Rais Dk. Shein alitoa
shukurani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Joseph
Magufuli kwa kushirikiana nae vyema pamoja na mashirikiano mazuri yaliopo baina
ya Serikali zao mbili hatua ambayo imepelekea Mkataba huo umeweza kutiwa saini.
Dk. Shein alisema kuwa
Rais Magufuli ametimiza wajibu wake yeye na wasadizi wake kwa manufaa ya ndugu
zao wa Zanzibar kwa kuhakikisha kwamba shughuli hiyo inafanikiwa “Nampongeza
kwa dhati”, aliongeza Rais Dk. Shein.
Dk. Shein alitoa
shukurani kwa Mtawala wa Ras Al Khaimah Shaikh Saud Bin Saqr Al Qasimi pamoja
na ujumbe aliofuatana nao kwa kujumuika pamoja katika hafla hiyo huku akitoa shukurani
maalum kwa viongozi wa Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kwa
kushirikiana kwa kufanya kazi pamoja kwa lengo la kuimarisha sekta za kiuchumi
na kijamii.
Alisema kuwa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar na wananchi wake wanathamini sana jitihada za Serikali ya
(UAE) katika kuimarisha maendeleo ya sekta zote muhimu ikiwemo maji,elimu,
biashara, usafiri wa anga na maendeleo ya sekta ya mafuta na gesi asilia kwa
kuendelea kushirikiana vizuri baina yao ppamoja na wananchi wote kwa jumla.
Dk. Shein alisema kuwa
Serikali zote mbili zina dhamira ya dhati ya kuendeleza suala hilo ambapo zililazimika kufanya marekebisho ya
sheria muhimu na kutunga sheria mpya zilizo bora zaidi, madhubuti na zenye
kuzingatia maslahi ya pande zote mbili za Muungano.
Alitumia fursa hiyo
kutoa shukurani kwa Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya
Mrisho Kikwete kwa hatua alizozichukua ili kuhakikisha kuwa kabla ya kustaafu
kwake suala hilo linapatiwa ufunbuzi na kuondoa kero ya muda mrefu.
Rais Dk. Shein alisema
kuwa tukio la utiaji saini Mkataba wa Mgawanyo wa Uzalishaji wa Mafuta na Gesi
Asilia linathibitisha jinsi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba
inavyotekeleza kwa mafanikio Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM, Sera zake na ahadi
ambazo ziliahidiwa wakati wa kampeni mwaka 2015.
Aliongeza kuwa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar inajivunia hatua hiyo muhimu kwa maendeleo na
utekelezaji wa dhamira ya kuiendeleza sekta ya Mafuta na Gesi Asili hapa
Zanzibar “Tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutufikisha hapa hivi sasa tuendelee
kuomba dua njema ili Mwenye Mungu atupe Baraka zaidi na aturahisishie
utekelezaji wa hatua zinazofuata”.
Alisema kuwa Mkataba huo
uliotiwa saini hivi leo unahusisha kitalu cha Pemba-Zanzibar tu ambacho
kinajumuisha maeneo yaliyopo nchi kavu na baharini hivyo, viko vitalu ambavyo
havimo katika makubaliano hayo yaliosainiwa hivi leo.
Dk. Shein alitumia fursa
hiyo kwa kutoa nasaha kwa wananchi waendelee kushirikiana katika kuimarisha na kuiendeleza sekta ya mafuta na
gesi asilia kwani ana imani kwamba matokeo ya juhudi hizo yatakuwa na manufaa
na mchango mkubwa katika kuendeleza uchumi wa Zanzibar.
Alisema kuwa kuimarika
kwa uchumi ni kunawiri kwa hali na maisha ya watu wa Zanzibar hali ambayo
itapelekea kuongezeka kwa Pato la Taifa na Pato la kila mwananchi jambo ambalo
litanyanyua hali ya maisha yao ya kila siku.
“Hapana shaka shughuli
za kiuchumi na ustawi wa jamii zitaimarika jambo hili faida yake ni mfano wa
afya na kiwiliwili yaani afya inapoimarika na kiwiliwili huimarika na
hunawiri….hata hivyo bado ni mapema mno kuelezea faida zote zitakazopatikana
iwapo tutafanikiwa katika suala hili”,alisema Dk. Shein.
Nae Mtawala wa Ras Al
Khaimah Shaikh Saud Bin Saqr Al Qasimi akitoa salamu zake kwa wananchi wa
Zanzibar alitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa jinsi anavyowapenda watu wa
Zanzibar ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji wake na watu kwa kufanikisha jambo hilo
kwa haraka.
Alitoa shukurani kwa
viongozi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jumla kwa kufanya kazi kwa
bidii kwa lengo la kujenga mustakabali na maendeleo ya watu wa Tanzania.
Mtawala huyo wa Ras al
Khaimah alitoa pongezi kwa mapokezi makubwa aliyoyapata huku akipongeza juhudi
kubwa zilizochukuliwa ndani ya mwaka mmoja katika kuhakikisha jambo hilo
linafanikiwa.
“Tuna furaha kubwa
katika nafsi zetu tunafungua ukurasa mpya wa maendeleo na mustakabali mpya wa
maendeleo na tunaona fahatri kubwa sana kujenga maendeleo na mustakabali wa
Zanzibar”,alisema Sheikh Al Qasimi.
Aidha, alisisitiza kuwa
Ras al Khaimah pamoja na nchi zote za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) wana
uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu kwa nchi za Afrika ya Mashariki ikiwemo
Tanzania ambapo kwa Zanzibar wana uhusiano maalum.
Mapema Katibu Mkuu Wizara yaArdhi, Nyumba, Maji na
Nishati Ali Khalil Mirza alisema kuwa Mkataba huo ni wa kwanza wa aina yake
katika historia ya Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar na huo ndio wmanzo wa miradi
mingi ya Mafuta na Gesi Asilia itakayokuja yenye lengo la kuimarisha uchumi wa
Zanzibar.
Alieleza kuwa historia
fupi ya zoezi la utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia kwa Tanzania lilianza
katika miaka 50 ambapo kwa upande wa Zanzibar Kampuni za British Petroleum (BP)
na Shell kwa pamoja zilifanya utafiti huo kwa kuchimba visima vya utafiti
kadhaa katika maeneo ya Unguja na Pemba.
Aliongeza kuwa Mkataba
wa Mgawanyo wa Uzalishaji (PSA) ni Mkataba unaoingiwa baina ya Serikali na
Kampuni za Kimataifa za Utafutaji, Uchimbaji na Uzalishaji wa Mafuta na Gesi
Asilia ambapo hatua hatua hiyo ya leo ya kusaini Mkataba wa Mgawanyo wa
Uzalishaji wa Mafuta na Gesi Asilia umepita katika hatua zote za kisheria na ni
Mkataba halali kwa pande zote mbili.
Alisisitiza kuwa mnamo
mwaka 2015, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania liliridhia Sheria ya
Mafuta Na.21 ya mwaka 2015 ambayo imeipa Serikali ya Ma;pinduzi ya Zanzbar
Mamlaka ya kushughulikia rasilimali za Mafuta na Gesi Asilia wenyewe.
Baada ya hafla hiyo,
Rais Dk. Shein akiwa na mgeni wake walikula chakula cha usikua ambacho Dk.
Shein alimtayarishia mgeni wake huyo na ujumbe wake.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment