Habari za Punde

Balozi Seif akagua maendeleo ya Mradi wa Ujenzi wa Makaazi ya Makamu wa Pili wa Rais na Uwanja wa Gombani

 Baadhi ya Majengo ya Mradi wa Makaazi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Pagali Chake Chake Pemba yanayoendelea na Ujenzi wake chini ya Wahandisi wa Kikosi cha Kuzuia Magendo Zanzibar {KMKM}.
 Haiba nzuri ya Muonekano wa Nyumba ya Makaazi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar inayojengwa katika eneo la Pagali Chake Chake Pemba unavyoonekana pichani.
  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akifanya ziara ya kukagua mradi wa ujenzi wa Makaazi yake katika Kijiji cha Pagali Chake Chake Pemba.
 Haiba nzuri ya Uwanja wa Michezo wa Gombani Chake Chake Pemba inavyoonekana ikiwa inaandaliwa kuhudumiwa Maadhimisho ya Sherehe za Maadhimisho ya kutimia Miaka 55 ya Mapinduni ya Zanzibar.
 Balozi Seif akiwa pamoja na Viongozi wa Wizara inayosimamia Michezo Wakuu wa Mikoa na Wilaya za Pemba akifanya ziara ya kukagua sehemu mbali mbali za Uwanja wa Michezo wa Gombani Pemba.
 Baadhi ya Wahandisi wa Ujenzi kutoka Wakala wa  majengo Zanzibar wakiendelea na harakati zao mbali mbali za matengenezo ya Uwanja wa Michezo wa Gombani Kisiwani Pemba.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis Ame, OMPR
Uongozi wa Wakala wa Majengo Zanzibar umeihakikishia Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwamba Mradi wa Ujenzi wa Makaazi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  utawekewa jiwe la Msingi kama ulivyopangiwa katika Ratiba ya Sherehe za Maadhimisho ya Kutimia Miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mshauri Muelekezi wa Ujenzi huo kutoka Wakala wa Majengo Zanzibar Kisiwani Pemba Bwana Mansour  Mohamed Kassim alieleza hayo na kuthibitishwa pia na Kamanda wa Kitengo cha Ufundi wa Kikosi cha Kuzuia Magendo Zanzibar {KMKM} CDR – Hamad Masoud Khamis wakati wa ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  ya kuangalia maendeleo ya Ujenzi wa Mradi huo.
Bwana Mansour alimueleza Balozi Seif  kwanza Mradi huo hivi sasa uko katika hatua nzuri ya ujenzi wa Majengo yote yaliyokusudiwa kujengwa katika eneo hilo kwa hatua ya awamu ya kwanza.
Naye kwa upande mwengine Kamanda wa Kitengo cha Ufundi wa Kikosi cha Kuzuia Magendo Zanzibar {KMKM} CDR – Hamad Masoud Khamis alisema Awamu ya Pili ya Mradi huo itazingatia ujenzi wa Uzio utakaozunguuka Kijiji hicho pamoja na mfumo wa Huduma nyengine muhimu.
CDR – Hamad Masoud alisema Wahandisi wa Ujenzi huo kutoka Vitengo tofauti vya Kikosi hicho wako makini katika kutekeleza kazi hiyo ikiachilia mbali jukumu lao jengine la kusimamia Ulinzi.
Balozi Seif  aliwapongeza Wajenzi wa Mradi huo kwa jitihada kubwa wanazochukuwa za kutekeleza wajibu wao hatua inayoleta faraja kubwa kwa Serikali nzima.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliutembelea Uwanja wa Michezo wa Gombani kuangalia maendeleo ya Matengenezo makubwa ya Uwanja huo utakaobeba kilele cha sherehe za Maadhimisho ya kutimia Miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Katibu Mkuu Wizara ya Vijana, Utamaduni na Sanaa Omar Hassan Omar { King} alisema hatua za matengenezo makubwa ya Uwanja huo zinaendelea vyema chini ya Wahandisi wa Wakala wa Ujenzi Kisiwani Pemba.
Omar Hassan alisema wahandisi hao hivi sasa wanaendelea na kazi ya kuvifanyia Matengenezo Vyoo, Paa pamoja na Majukwaa ya VIP ya Uwanja huo baada ya kumaliza uchimbaji Kisima cha maji safi na salama Uwanjani hapo ili uwahi sherehe hizo kama ulivyopangiwa na Taifa.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliwapongeza Wahandisi hao kwa kazi kubwa na nzito wanayoendelea kuifanya ambayo imeanza kuleta matumaini.
Balozi Seif alisema pamoja na kazi kubwa ya saa 24 kutekeleza jukumu hilo kwa nia ya kuwahi Ratiba lakini bado aliwaagiza kutamuwa muda mwengine wa ziara kwa kuhakikisha kazi hiyo inamalizika kwa wakati uliopangwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.