Habari za Punde

Miradi 56 kuzinduliwa katika shamra shamra za Maadhimisho ya Sherehe za kutimia Miaka 55 ya Mapinduzi

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kulia akiongoza Kikao cha Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa kilichochukuwa siku nzima kupanga ratiba nzima ya Sherehe za Maadhimisho ya kutimia Miaka 55 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964.
Kikao hicho kilifanyika katika Ukumbi wa Majengo ya Jumba la Kumbukumbu ya Kifalme Mtaa wa Mizingani Mjini Zanzibar.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis Ame, OMPR

Jumla ya Miradi 56 ya Maendeleo,Uchumi na Ustawi wa Jamii inatarajiwa kuzinduliwa na kuwekewa Mawe ya Msingi ndani ya Kumi la shamra shamra za Maadhimisho ya Sherehe za kutimia Miaka 55 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964.
Miongoni mwa Miradi hiyo, 39 itazinduliwa baada ya kukamilika kwake, wakati Miradi 17 inaratajiwa kuwekewa Mawe ya Msingi ikijumisha pamoja na ile ya Taasisi za Umma, Miradi ya Kijamii sambamba na ile ya Uwekezaji Vitega Uchumi.
Hayo yalibainika wakati wa Kikao cha Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa kilichokutana chini ya Mwenyekiti wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na kufanyika katika Ukumbi wa Jengo la Makumbusho ya Kifalme liliopo Mizingani Mjini Zanzibar.
Wajumbe wa Kikao hicho cha Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa katika majadiliano yao walifikia maamuzi ya kuitoa Baadhi ya Miradi iliyoainishwa kuingizwa katika Ratiba ya Sherehe hizo baada ya kubaini kutotofikia kiwango kinachokubalika katika kiwango cha uzinduzi au uwekaji wa Mawe ya Msingi.
Hata hivyo baadhi ya Wajumbe wa Kikao hicho walipendekeza kubadilishwa kwa nyakati na siku za Uzinduzi na uwekaji wa Mawe ya msingi kwa kuzingatia ratiba za Viongozi Wakuu kuepuka kusafiri zaidi ya mara moja wakati wanaposhiriki kwenye matukio mbali mbali ndani ya Kumia la Sherehe hizo.
Mabadiliko hayo pia yaligusa kwa baadhi ya miradi kutia mashata kwenye uwekaji wa mawe ya msingi au uzunduzi  kutokana na utekelezaji wake kuwa na mashaka kufuatia mabadiliko ya usimamizi wa majukumu uliotokana na muongozo wa Serikali wa kukasimu madaraka Mikoani katika Mfumo wa Ugatuzi.
Mapema Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Shaaban Seif Mohamed alisema Miradi yote iliyopendekezwa kuingizwa katika Maadhimisho ya sherehe za Miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar imekaguliwa.
Nd. Shaaban alisema ukaguzi huo ulifanywa na Wajumbe wa Kamati ya Sekritarieti ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa kujiridhisha na hatua iliyokidhi hali halisi ya Ufunguzi ama kuwekewa mawe ya Msingi Miradi iliyoainishwa kwenye mpango huo.
Alisema yapo marekebisho yaliyofanywa na Kamti hiyo katika kupembua Miradi inayostahiki kuingizwa ndani ya Ratiba ya Sherehe na kufikia maamuzi ya kuitoa ile Miradi iliyoshindwa kufiki kiwango kinachohitajika kuingizwa kwenye mtiririko.
Katika uzinduzi na uwekaji wa Mawe ya Msingi ya Miradi iliyomo ndani ya Sherehe hizo Viongozi wa Kitaifa wa Serikali zote mbili ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi ya Zanzibar wamejumuishwa katika ratiba hizo wakiwemo Marais, Mawaziri pamoja na Viongozi Wastaafu wa pande zote mbili.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.