Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi,akisoma Hutuba ya Kuahirisha Mkutano wa Kumi na Mbili wa Baraza la Tisa la Wawakilishi Zanzibar leo, Tarehe 06 Disemba, 2018
Mheshimiwa Spika,
Awali ya yote napenda
kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mwingi wa Rehma kwa kutujaalia uhai na
afya njema na kutuwezesha kufanikisha Mkutano huu wa Kumi na Mbili wa Baraza la
Tisa ulioanza tarehe 28 Novemba, 2018 hadi leo tarehe 6
Disemba, 2018 tunapouahirisha.
Mheshimiwa Spika, Napenda kutoa pongezi zangu za dhati kabisa kwa Rais wetu
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein kwa
kutekeleza matakwa ya Wazanzibari ya kutia saini mkataba wa mgawanyo wa
uzalishaji wa mafuta na gesi asilia (Production Sharing Agreement) baina ya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Kampuni ya RAKGAS tarehe 23 Oktoba, 2018. Mkataba huo ni halali kama ilivyokuwa
halali boribo siagi kuliwa! Wale wanaodhani Rais wetu amevunja Katiba au
sharia ya nchi ruhsa kwenda Mahakamani kwani nchi yetu inafuata misingi ya
utawala bora.
Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza kwa dhati Mwakilishi wa Jimbo la Jang’ombe,
Mheshimiwa Ramadhan Hamza Chande kwa kuapishwa kuwa Mjumbe wa Baraza lako
Tukufu baada ya ushindi mkubwa wa kishindo alioupata wa uchaguzi mdogo
uliofanyika tarehe 27 Oktoba, 2018.
Aidha, nawapongeza wananchi wa Jimbo la Jang’ombe kwa kuendelea kukiamini
Chama cha Mapinduzi kuwa ndio Chama pekee kinachoweza kusimamia amani, utulivu
na mshikamano wa nchi na kuwaletea maendeleo ndani ya nchi yao.
Mheshimiwa Spika, mkutano huu tumejadili
kwa kina Miswada mitatu ambayo ni:-
i.
Mswada wa Sheria ya Kuweka Masharti Yanayosimamia Utoaji wa Huduma za
Msaada wa Kisheria, Kurahisisha Upatikanaji wa Haki na Kuweka Masharti Mengine
Yanayohusiana na Hayo.
ii. Mswada wa Sheria ya
Kufuta Sheria ya Ukuzaji na Kulinda Uchumi Zanzibar Nam. 11 ya mwaka 2004 na
Kutunga Sheria ya Mamlaka ya Ukuzaji na Kulinda Vitega uchumi Zanzibar na
kuweka Masharti Mengine yanayohusiana na Hayo.
iii.
Mswada wa Sheria ya Kufuta Sheria ya Vyama vya Ushirika Nam. 4 ya Mwaka
1986 na Kutunga Sheria ya Vyama vya Ushirika Zanzibar ya Mwaka 2018 ambayo
inaweka utaratibu wa Uundaji na Uendeshaji ya Vyama vya Ushirika na Mambo
Mengine Yanayohusiana na Hayo.
Mheshimiwa Spika, ni imani yangu Miswada hiyo mitatu (3)
tuliyoipitisha itakapokuwa Sheria itasaidia kuondoa changamoto mbali mbali
tulizozijadili ambazo zilipelekea haja
ya kuwa na Miswada hii. Mbali na Miswada hii Baraza lako Tukufu pia lilipokea taarifa ya Serikali kuhusu hoja ya Mjumbe ya
kuitaka Serikali kuja na mkakati unaotekelezeka kwa kutatua changamoto
zinazowakabili wakulima wa zao la mwani.
Mheshimiwa Spika,
Halikadhalika, Baraza
lilipokea hoja mbili kutoka kwa Waheshimiwa Wajumbe ikiwemo hoja inayotaka
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka Viti Maalum vya Wanawake kufaidika na
fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo, na Hoja ya kutaka kuliomba Baraza lako Tukufu
kutoa maazimio ya kushughulikia tatizo la kuharibika kwa vifaa tiba kwenye Hospitali ya Abdulla Mzee iliyoko
Mkoani, Pemba. Serikali imeichukua hoja
hiyo na kwenda kuifanyia kazi na hatimae itakuja na majibu muafaka yatakayoweza
kuondoa matatizo yaliyokuwepo katika eneo hilo.
Mbali na hayo Waheshimiwa Wajumbe walipata nafasi kuuliza maswali ya
msingi 123 na maswali ya nyongeza ...... ambayo yote yalijibiwa kwa mfasaha na
Waheshimiwa Mawaziri.
Mheshimiwa Spika,
kama tujuavyo tarehe 3
Disemba ya kila mwaka ni Siku ya Watu Wenye Ulemavu Duniani. Zanzibar kama nchi
nyengine tumeadhimisha siku hii na mimi nilibahatika kuwa Mgeni Rasmi. Miongoni
mwa mambo yanayowakwamisha watu wenye ulemavu ambayo yanawapa usumbufu mkubwa
na mara nyengine huwa wanadhalilika ni kutokana na miundombinu isiyokuwa rafiki
kwao. Majengo yetu mengi yamejengwa bila kuzingatia mahitaji ya watu wenye
ulemavu ambayo yanawapa usumbufu mkubwa na mara nyengine huwa wanadhalilika
katika kuzifikia huduma muhimu za kijamii kutokana na miundombinu iliyopo. Kwa
mara nyengine tena, napenda kutoa wito kwa vyombo vyote nchini vinavyohusiana
na ujenzi wa miundombinu yote pamoja na majengo kuzingatia muongozo wa Serikali
wa miundombinu rafiki ambao unaelezea upatikanaji wa haki na fursa za watu
wenye ulemavu kuweza kuzifikia huduma zitolewazo bila ya vikwazo, kwani tuelewe
sisi sote ni walemavu watarajiwa, hivyo tunahitaji kujitengenezea miundombinu
ambayo isiyomkwaza au kumpa shida mwengine katika maisha yake.
Mheshimiwa Spika, mwezi huu wa Disemba
tarehe 1 tuliadhimisha Siku ya Ukimwi Duniani.
Miongoni mwa malengo ya nchi yetu kama zilivyo nchi nyengine duniani
katika kupambana na maradhi haya thakili ya ukimwi ni kuzifikia shabaha za 90
tatu (90-90-90) ifikapo mwaka 2020, ili kumaliza maradhi ya UKIMWI
ifikapo mwaka 2030. Katika kuzifikia shabaha hizo tumefanikiwa kuzifikia 90
mbili za mwanzo. Kwa ufafanuzi Tisini ya mwanzo maana yake ni asilimia 90 ya
watu wanaoishi na VVU wawe wanajitambua.
Hadi kufikia Septemba mwaka huu, asilimia 92 ya watu wanaokisiwa kuishi
na VVU tayari wanajitambua (kwa lugha nyengine watu 5,861 kati ya watu 6,393
wanaoishi na VVU tayari wanajitambua). Tisini ya pili maana yake asilimia 90 ya
wale wanaojitambua wawe wanatumia dawa za kupunguza makali ya VVU umaarufu kama
ARVs. Shabaha hii nayo Zanzibar tayari tumeifikia. Hadi kufikia Septemba
asilimia 98 ya wanaojitambua wanatumia dawa za ARVs (kwa lugha nyengine watu
5,725 kati ya watu 5,861 wanaojitambua kuambukizwa na virusi vya ukimwi
wanatumia ARVs). Bado hatujaifikia shabaha ya 90 ya tatu inayotaka asilimia 90
ya wale wanaotumia dawa za ARVs wawe na kiwango cha chini cha virusi
mwilini. Hadi kufikia Septemba tulifikia
asilimia 76, naamini kwa kushirikiana vizuri na wagonjwa, watoa huduma na jamii
kwa ujumla 90 hiyo nayo ifikapo mwaka 2020 tutaweza kuifikia bila ya matatizo.
Mheshimiwa Spika,
ukimwi bado upo unaathiri
nguvu kazi ya Taifa na bado hauna dawa. Wito wangu kwa wananchi wenzangu
kuchukua juhudi za makusudi kutumia ipasavyo huduma za upimaji ili kuitendea
haki kauli mbiu ya mwaka huu “Pima Virusi vya Ukimwi ujue Afya Yako”.
Mheshimiwa Spika, maradhi
yasiyoambukiza (Non-Communicable Diseases - NCD) hivi sasa yanaongezeka kwa
kasi ya kutisha duniani kote kwa mujibu wa wataalamu wetu wa afya. Maradhi haya
yakiwemo kisukari, shindikizo la damu (pressure), tezi dume na saratani ya
shingo kizazi yapo pia hapa kwetu na ndio maana hata Jumuiya inayohusika na
maradhi yasiyoambukiza imeundwa hapa Zanzibar. Miongoni mwa mambo ambayo
yatasaidia kupambana na maradhi haya ni kupima afya zetu mara kwa mara, kufanya
mazoezi pamoja na kupendelea kula vyakula vya asili badala ya vyakula vya
makopo.
Mheshimiwa Spika, Nawaomba
Waheshimiwa Wajumbe tujitokeze kwenda kupima ili tujue afya zetu mapema. Tupime tezi dume japo mara moja kwa miezi
sita, tusiogope upimaji wake pamoja na saratani ya shingo ya kizazi. Sisi ni Viongozi na Viongozi huongoza kwa
mifano bora. Naamini tukiwa mstari wa
mbele katika kupambana na maradhi haya yasiyoambukiza wananchi wetu watakuwa
nyuma yetu. Kinga ni bora kuliko tiba. Tuutumie usemi
huu kumpambana na maradhi yasiyoambukiza kwa kwenda kupima afya zetu.
Mheshimiwa Spika, Serikali
yetu imejidhatiti kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa wanawake
na watoto kwa nguvu zake zote. Takwimu za mwaka 2017/2018 zinaonyesha kuwa
matukio 1,091 yameripotiwa kutoka Jeshi la Polisi ukilinganisha na matukio
2,449 yaliyoripotiwa mwaka 2016/2017. Takwimu hizi bado hazifurahishi ijapokuwa
kutokana na jitihada mbali mbali matukio haya yamepunguwa kwa mwaka 2017/2018.
Hivyo basi, inaonyesha wazi tukijipanga vizuri tunaweza kabisa kupunguza
vitendo hivi na hatimaye kuvimaliza kabisa.
Uzoefu
unaonyesha kuwa vitendo vya ukatili na udhalilishaji hufanywa na watu wa karibu
na familia na jambo la kusikitisha zaidi pale watu tunaowaamini kama walimu wa
Madrasa na Skuli kushiriki katika vitendo hivi. Matukio ya vitendo hivi zaidi
hufanywa kwa watoto kuliko watu Wazima. Takwimu kutoka jeshi la Polisi
zinaonyesha kwamba asilimia 88.8 ya matukio yaliyopokelewa kwa mwaka 2017/2018
yalikuwa ni ya watoto.
Mheshimiwa Spika,
ukitaka kuiangamiza nchi
kiurahisi basi chezea elimu yake.
Udanganyifu wa mitihani ni miongoni mwa vitendo vya uhalifu vyenye nia
ya kuiangamiza nchi yetu kimaendeleo. Hakuna Serikali makini duniani
itakayokubali kuchezewa elimu yake. Kwa
maana hiyo udanganyifu wa mitihani ya Taifa ya Darasa la 10 au Form II
uliotokea na kulazimisha Serikali kufuta mitihani yote haukubaliki hata kidogo.
Serikali itachukuwa hatua kali dhidi ya wale wote waliohusika na uhalifu huu.
Tutang’oa miti hata kama ni mikubwa kama mbuyu, miche, mizizi na mbegu
zinazosubiri kuchipua ili tukio hili lililotia aibu Serikali yetu lisitokee
tena. Napenda kumpongeza Mhe. Riziki
Pembe Juma, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali kwa umakini wake mkubwa wa
kufuta mara moja mtihani wote wa Darasa la 10 baada ya kugundua kuvuja kwa
mtihani huo.
Nawaomba
wananchi wote wa Zanzibar washirikiane na Serikali katika kupiga vita uhalifu
huu ambao ukiachiwa utaliangamiza Taifa letu. Natoa agizo kwa Wizara ya Elimu
na Mafunzo ya Amali kuchukua tahadhari zote ili udanganyifu wa mitihani
Zanzibar usitokee tena. Aidha, naviomba
vyombo vya ulinzi na usalama kufanya upelelezi wa kina na kuwapeleka Mahakamani
mara moja wale wote waliohusika na udanganyifu wa mitihani hiyo.
Mheshimiwa Spika, Zanzibar ni nchi
inayoongozwa na kuendeshwa katika misingi ya utawala bora na kufuata sharia
ilizojiwekea. Hata hivyo, hivi karibuni
kumekuwa na tabia ya baadhi ya watu kupuuza au kutofuata na kutoheshimu Sheria
zilizowekwa kwa baadhi yao wasio waaminifu kwa sababu wanazozijua wao wenyewe
katika Taasisi mbali mbali za umma na kusababisha madhara makubwa kwa jamii
yetu.
Kwa
mfano, tulitunga sheria ndani ya Baraza hili kuhusu uvaaji wa kofia ngumu
(helmet) kwa vyombo vya maringi mawili, na ukipita njiani utakuta wasimamizi wa
Sheria hiyo na watekelezaji wanapuuza kwa kiasi kikubwa. Hivyo, natoa wito kwa Jeshi la Polisi
kusimamia utekelezaji wa sheria hiyo bila muhali wala upendeleo. Kwani kupuuza
utekelezaji wa Sheria hiyo ni kuhatarisha maisha ya wananchi wetu.
Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia hotuba yangu nakushukuru wewe
Mheshimiwa Spika, Naibu Spika, Katibu wa Baraza na timu yake yote kwa
kuliendesha Baraza hili Tukufu kwa
ueledi wa hali ya juu. Aidha, nawashukuru Waheshimiwa Wajumbe kwa kutumia
nafasi yenu ya kidemokrasia ya kuisimamia, kuishauri na kuihoji Serikali, jambo
ambalo limeonesha nia thabiti mliyonayo ya kuitaka Serikali yenu kuwajibika
ipasavyo kwa wananchi wake. Kadhalika,
napenda kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa kujibu maswali
yote mliyoulizwa; mliweza kuyatolea ufafanuzi vizuri na kwa usahihi yote
maswali yaliyoulizwa kwa lengo la kuwafahamisha wananchi wetu jinsi Serikali
yao inavyowatumikia. Aidha, napenda pia kumpongeza Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu
wa Serikali kwa ufafanuzi alioutoa katika mambo mbali mbali yaliyohitaji
ufafanuzi wa kisheria.
Kwa namna ya pekee
navishukuru vyombo vya habari kwa kazi yao nzuri ya kuwawezesha wananchi
walioko majumbani kufuatilia yaliyokuwa yanatokea ndani humu. Nawaomba Waheshimiwa Wajumbe tuendelee
kupendana, kuvumiliana na kushirikiana katika kuijenga nchi yetu kiuchumi na
kijamii kwani mshikamano na umoja wetu ndio utakaoivusha nchi yetu kuelekea
kwenye maendeleo endelevu.
Mheshimiwa
Spika, nawashukuru wananchi wote wa Zanzibar kwa namna
walivyoutumia vyema mwaka 2018 katika shughuli za uzalishaji na ninawatakia
kheri ya mwaka mpya wa 2019 Mungu atujaalie kheri, salama na mapenzi baina
yetu. Uwe ni mwaka wa mavuno mengine, na
ambao Mwenyezi Mungu atuondoshee maradhi kwa wagonjwa wetu na kuipa nguvu
Serikali yetu ili itekeleze kwa ufanisi wa hali ya juu malengo iliyojiwekea kwa
ajili ya watu wake. Aidha, nawaomba
wananchi wote wajitokeze kwa wingi kusherehekea miaka 55 ya Mapinduzi Matukufu
ya Zanzibar siku itakapowadia katika kiwanja cha Gombani, Pemba kwenye upepo
mwanana wa marashi ya karafuu.
Mwisho, napenda kuwapongeza Wakalimani wetu wa
lugha za alama ambao wamefanya kazi nzuri ya kuwajulisha watazamaji wetu wenye
ulemavu wa kusikia kilichokuwa kinaendelea ndani ya Baraza lako Tukufu.
Mheshimiwa
Spika, Baada ya maelezo hayo, naomba sasa kwa heshima na
taadhima kutoa hoja kwamba Baraza lako Tukufu liakhirishwe hadi siku ya
Jumatano tarehe 06 Februari, 2019, saa 3.00 barabara za asubuhi panapo
majaaliwa.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment