Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa Mhe. Panya Ali Abdallah, akizungumza na Watengaji wa Ofisi ya Rais walipofika kutembelea Ofisi hiyo kupata Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango Kazi wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi..
Na.Abdi Shamna Ikulu Zanzibar.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Baraza la
Wawakilishi Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa Zanzibar Mhe. Panya Ali Abdalla amesema
hatua ya Serikali kufanya sherehe za Mapinduzi kisiwani Pemba mwaka huu,
inaakisi uwiano sawa uliopo kati ya wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba.
Mwenyekiti huyo amesema hayo leo wakati Kamati
hiyo ilipokutana na Uongozi wa Wizara ya Nchi (OR) na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Ikulu mjini hapa, kupitia taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbali
mbali za Wizara kwa kipindi cha Julai hadi Disemba, 2018.
Amesema sherehe hizo zilizoambatana na uzinduzi
wa miradi ya maendeleo, zimepanua wigo wa upatikanaji wa huduma kwa wananchi wa
Pemba pamoja na wafanyabiashara kupata fursa muhimu ya kuendesha shughuli zao.
Alisema ni jambo la faraja kwa wananchi wa kisiwa
hicho kufikiwa na matukio matatu makubwa na muhimu katika kipindi cha mwaka
2018/19, ikiwemo Kongamano la Diaspora, Siku ya Chakula Duniani pamoja na
sherehe za Mapinduzi.
Aliwapongeza wana Diaspora kwa kushiriki
kikamilifu katika mipango ya maendeleo ya nchi, hatua inayolenga kusaidia
ukuaji wa kiuchumi pamoja na upatikanaji wa huduma za kijamii, ikiwemo afya.
Alisema upatikanaji wa vifaa vya tiba, ikiwemo
vile vinavyotumiwa na watu wenye ulemavu, unaunga mkono juhudi za serikali
katika uimarishaji wa afya ya jamii nchini.
Aidha, aliipongeza Wizara hiyo kw ajuhudi kubwa
zilizochukuliwa kuzifanyia matengenezo Ikulu za Chake chake na Micheweni,
ikizingatiwa ugeni mkubwa uliomfikia Rais katika sherehe za Mapinduzi.
Nae, Mjumbe wa Kamati hiyo, Ali Suleiman Ali,
alipongeza juhudi zinazochukuliwa na kitengo cha Habari, Ofisi ya Rais katika
utoaji wa taarifa kuhusiana na miradi mbali mbali inayoendeshwa hapa nchini.
Mjumbe huyo alishauri juhudi zaidi zifanyike ili kupanua wigo wa
utoaji wa taarifa, hususan pale panapokuwepo uzinduzi wa miradi mikubwa ya
kitaifa.
"Ushauri wangu panapokuwa na uzinduzi wa
miradi mbali mbali mikubwa, uzinduzi
wake ufanyike rasmi na vyombo vya habari viwepo ili kumsaidia Mheshimiwa Rais
katika utekelezaji wa Ilani", alisema.
Alisema hali ilivyo hivi sasa, taarifa za matukio
mengi zimekuwa hazivuki mipaka ya Visiwa vya Zanzibar na Pemba.
Aidha, Mjumbe wa Kamati hiyo Mussa Ali Mussa
aliiomba Wizara hiyo kuchukuwa hatua za dharura kuufanyia ukarabati ukuta wa
Ikulu ya Mkoani, unaokabiliwa na mmong'onyoko, ili kuunusuru na mvua zijazo.
Vile vile aliomba Wizara hiyo kuimarisha huduma
za usafiri kwa wafanya kazi wa Wizara hiyo kisiwani Pemba ,kulifanyia
matengenezo jengo la GSO na kupatiwa vifaa vya kisasa wafanyakazi wake.
Mapema, Waziri wa Wizara ya Nchi (OR) na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Issa Haji Ussi, alisema katika kipindi
hicho, Wizara imefanikiwa kupata fedha kutoka Serikali kwa asilimia 94, hivyo
kuwezesha kutekeleza vyema majukumu yaliopangwa.
Alizitaja
miongoni mwa kazi zilizotekelezwa kwa ufanisi na Idara za Wizara
hiyo kuwa ni pamoja na ahadi za Rais,
utoaji wa taarifa, mafunzo, ujenzi wa majengo, kuimarisha usalama wa serikali,
ukaguzi, mikutano na Diaspora, pamoja na
uimarishaji wa huduma za maktaba.
Kazi nyingine zilizotekelezwa katika kipindi
hicho ni pamoja na uimarishaji wa maendeleo ya michezo, uhusiano wa kimatifa,
ukarabati wa nyumba za viongozi, ukaguzi wa majengo na nyenginezo.
Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422
Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822
E-mail: abdya062@gmail.com.
No comments:
Post a Comment