Na.Grace Semfuko-MAELEZO
Nchi za kiafrika zimeshauriwa
kutafakari kwa mapana zaidi kabla ya kuingia kwenye mkataba wa Mpango wa
Ushirikiano wa Kiuchumi (EPA) baina ya Jumuiya za nchi mbalimbali za Afrika na
Nchi za Ulaya Jumuiya za Ulaya ili kuepuka kujitokeza mikanganyo ya mipango ya uendeshaji wao ya
uchumi, ambapo kila nchi ina vipaumbele
vyake.
Hayo yamebainishwa Jijini Dar Es
Salaam leo na Mtaalamu wa Uchumi, Profesa Daktari Helmut Asche wa Chuo Kikuu
cha Leipzig, nchini Ujerumani, Profesa Asche amekuwa mshauri bingwa wa masuala
ya uchumi mara kadhaa kwa nchi mbalimbali za Afrika.
Akiongea na waandishi wa Habari
katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa
wa Julius Nyerere, alisema baadhi ya nchi za Afrika hadi sasa hazijasaini
mkataba wa EPA kwa kusita na yaliyomo kwenye mkataba kwa kuwa yanakosa manufaa kwa nchi zao. Hata hivyo
baadhi ya nchi za Afrika zimekwishasaini Mkataba huo huku zingine zikiendelea
kuutafakari.
Kwa upande wa Tanzania, bado
haijasaini mkataba huo ingawaje wasomi na Wataalamu wa mambo ya uchumi tayari
wameonyesha kutoukubali mkataba huo.
“Ni muhimu kwa Nchi za Afrika
kuangalia manufaa wanayoweza kuyapata katika mkataba huo, wasikimbilie kuusaini
kwani kila nchi ya Afrika ni bora kuutathmini mkataba huo ili kuepuka migongano
baina ya vipaumbele vyao” alisema Profesa Asche.
Akifafanua, Profesa Asche alisema
anatambua sekta binafsi ya Tanzania inavyotegemewa kuinua uchumi wa Taifa kama
ilivyo kwa sekta binafsi kwenye mataifa ya Ulay, lakini ili kila mmoja anufaike
kwa upande wake ana mchakato wa utekelezaji kwa vipaumbele vyake,
“Tanzania kwa
mfano, inahitaji Viwanda, na hivyo viwanda vinahitaji malighafi na kipaumbele
kitakuwa kuuza nchini na ziada nchi za nje, na si
vinginevyo.”
Asche aliongeza kuwa kabla ya
nchi yoyote kuusaini Mkataba wa EPA ni muhimu kuangalia utashi wake wa kisiasa
na vipaumbele vyake ikilinganisha na utashi
wa malengo ya nchi yaliyomo ndani ya Mkataba huo.
Rais Dkt John Pombe Magufuli
mwaka 2017 alihoji kuhusu Mkataba wa EPA na kusema ni chimbuko la ukoloni mamboleo.
Kadhalika Wabunge wa Chama Tawala
na upinzani ndani wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamekuwa wakihoji
manufaa yanayokusudiwa ndani ya mkataba wa EPA bna kuonesha hofu yao.
Kwa Upande wa Tanzania Mkataba
huo wa mpango wa ushirikiano wa kiuchumi baina ya Jumuiya ya Nchi za Ulaya na
Afrika EPA umekuwepo tangia mwaka 2007, na Oktoba 2014 Jumuiya ya Afrika
Mashariki EAC na ile ya Ulaya EU walikamilisha majadiliano baina yao na
walitarajia kufunga mkataba wa makubaliano mwezi Julai 2016.
Hata hivyo mwaka 2017 Wabunge wa
Bunge la Afrika Mashariki wengi wao katika vikao mbalimbali waliukataa mkataba
huo wakiashiria kuweza kukwamisha dhamira ya mikakati kadhaa ukiwemo wa kuinua
viwanda Afrika Mashariki.
No comments:
Post a Comment