Habari za Punde

Milioni 148 kutumika kupeleka maji safi na salama visiwa vya Uvinje na Fundo

Na Masanja Mabula -Pemba
JUMLA ya shilingi Milioni 148  zinatarajia kutumika kupeleka  huduma ya maji safi na salama katika visiwa vya Uvinje na Fundo Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Mradi huo unatekelezwa kwa pamoja kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na taasisi ya Pemba Foundation yenye makao yake makuu nchini Marekani.
Mkuu wa wilaya ya Wete Abeid Juma Ali akizungumza baada ya kukagua mradi huo , amewataka wananchi watakaonufaika na huduma hiyo, kuitunza miundo mbinu iliyowekwa.
Amesema kuwapatia maji wananchi wa maeneo ya visiwa ni moja ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020.
“Mradi huu utatumia fedha nyingi , lakini wananchi ndio ambao mtanufaika, hivyo ni jukumu lenu kuilinda miundo mbinu ambayo iliyowekwa”alisisitiza Mkuu wa Wilaya.
Aidha Mkuu wa Wilaya aliongeza kwamba”Kazi ya kuwapelekea wananchi  wa maeneo ya visiwa huduma muhimu za kijamii , ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ambayo imeagiza huduma za kijamii ziwafikie wananchi popote walipo”alisema.
Mkurugenzi wa Pemba Foundation Nassor Ahmed Marhun amesema mradi huo unataraji kukamilika baada ya miezi mitatu.
Nassor amesema kwa sasa mradi huu umeshagharimu shilingi milioni 76, na umekamilika kwa zaidi ya asilimia 80.
“Tunahitaji kiasi cha shilingi milioni 72 kukamilisha mradi huu wa maji katika visiwa vya Uvinje , Fundo pamoja na Ukunjwi”alifahamisha.
Ameeleza kwamba taasisi ya Pemba Foundation wanakusudia kujenga kituo cha afya Uvinje , lakini wameona ni bora kufikisha huduma ya maji ili waanze kutekeleza mradi wa kituo cha afya.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar –ZAWA-kisiwani Pemba ,Omar Mshindo Bakar amesema kisima kilichochimbwa na ambacho kitakuwa kinasambaza maji katika maeneo hayo kinauweza kuzalisha lita 40,000, kwa sasa.
Nao baadhi ya wananchi watakaonufaika na huduma hiyo, wamepongeza taasisi ya Pemba Foundation kwa kuwasaidia kuliondoa tatizo la maji lililokuwa linawakabili kwa muda mrefu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.