Habari za Punde

Uwajibikaji Kwa Watumishi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA Kupunguza Malalamiko Kwa Wananchi.

Na.Mwanajuma Juma.
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania TCRA imesema kuwa upatikanaji wa habari sahihi bila ya vikwazo itaongeza uwazi na uwajibikaji kwa watumishi wa Mamlaka hiyo na hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa malalamiko.
Akizungumza na Wadau mbalimbali wa huduma za mawasiliano wakiwemo wamiliki wa makampuni ya simu, redio na mafundi wa kompyuta na Simu,  Mkuu wa Mamlaka hiyo Esuvatie Masinga amesema  ukweli na uwazi katika kazi zao ndio kinga muhimu ya kuzuia malalamiko ambayo yanaweza kutafsiriwa na wadau wa sekta ya mawasiliano kuwa ni vitendo vya rushwa.


Hivyo alisema kuwa TCRA inaendelea kuboresha taratibu na kanuni za ndani kwa lengo la upatikanaji wa habari kwa wadau wao wote.

“Sisi TCRA ofisi ya Zanzibar tutaendelea kushirikiana na wadau wa mawasiliano hapa Zanzibar ili kusimamia kwa makini sera, sheria na kanuni hizo ili kuweza kupatikana kwa huduma za mawasiliano”, alisema.

Alifahamisha kwamba katika kuthibitisha hayo Mamlaka yao imeandaa kitabu cha muongozo kwa watumiaji wa huduma na bidhaa za mawasiliano ili kumuwezesha mtumiaji wa huduma za mawasiliano kujiandaa dhidi ya matukio yanayoweza kutokea na kumsababishia athari za kiafya , kiusalama au upotevu wa mali zake.

Aidha alisema kuwa muongozo huo pia una  lengo la kutoa dondoo muhimu kwa wanaotumia huduma za simu  na intenet, huduma za utangazaji na huduma za posta.

“Sote tunatambuwa kwamba katika awamu ya tano kipaombele ni uchumi wa viwanda ambao kasi ya maendeleo yake yanategemea teknolojia ya habari na mawasiliano”, alisema.

Hivyo alisema kuwa shughuli za kiuchumi za Zanzibar zitakuwa na tija kwa taifa lao pale tu zitakapokuwa imara, zitajuulikana na kuweza kuendeshwa kwa kufuata sheriana taratibu zilizopo.

Hata hivyo alisema kuwa kuendelea kuimarika kwa matumizi bora na salama ya mawasiliano  kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali kupitia Mamlak yao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.