Habari za Punde

Pori la Akiba la Selous Kueuzwa Kuwa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere


Baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kuagiza sehemu ya Pori la Akiba la Selous kugeuzwa kuwa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere, mchakato wa kutekeleza agizo hili umekamilika. Tarehe 9 Septemba, 2019, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Azimio la Bunge la kuanzisha Hifadhi ya Taifa ya Nyerere. Tarehe 19 Novemba, 2019, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, aliweka sahihi kwenye Tangazo la kuanzisha rasmi Hifadhi ya Taifa ya Nyerere. Kwa hivyo, Hifadhi ya Taifa ya Nyerere imeanza rasmi tarehe 19 Novemba, 2019.

Hifadhi ya Taifa ya Nyerere ina ukubwa wa kilometa za mraba 30,893 na kuifanya kuwa moja ya hifadhi kubwa sana duniani yenye vivutio vingi vya asili na wanyamapori wengi.

Kadhalika, kufuatia Azimio la Bunge la tarehe 10 Septemba, 2019 la kuanzisha Hifadhi ya Taifa ya Kigosi na Hifadhi ya Taifa ya Mto Ugalla, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, ameweka sahihi matangazo ya kisheria ya kuanzisha rasmi Hifadhi ya Taifa ya Kigosi na Hifadhi ya Taifa ya Mto Ugalla.  Hifadhi hizi mpya sasa zinatambuliwa rasmi kisheria kuanzia tarehe 19 Novemba, 2019.

Hifadhi ya Taifa ya Kigosi ina ukubwa wa kilometa za mraba 7,460. Kadhalika, Hifadhi ya Taifa ya Mto Ugalla ina ukubwa wa kilomita za mraba 3,865.

Kufuatia hatua hii, Tanzania sasa inakuwa na jumla ya hifadhi za taifa ishirini na mbili.
  
Prof. Adolf F. Mkenda
KATIBU MKUU
22 Novemba, 2019

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.