Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein Azungumza na Ujumbe wa Benki ya CRDB Ikulu Jijini Zanzibar leo.13-2-2020.


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein akizungumza na Uongozi wa Benki ya CRDB ukiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa CRDB Ndg. Ally Hussein Laay ( kulia kwa Rais) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benk ya CRDB Ndg.Abdulmajid Mussa Nsekela, walipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kumtambulisha Mkurugenzi Mtendaji mpya wa benki hiyo, hafla hiyo imefanyika leo 13-2-2020.Ikulu Zanzibar

RAIS  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza haja kwa Benki ya CRDB kuendelea kutoa huduma zake kwa pande zote mbili za  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili wananchi  wote wafaidike na matunda ya benki hiyo.

Dk. Shein aliyasema hayo leo, Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Benki ya CRDB Abdulmajid Mussa Nsekela aliyefika Ikulu kwa ajili ya kujitambulisha akiwa amefuatana na uongozi wa Benki hiyo ulioongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Ally Hussein Laay.

Katika maelezo yake Rais Dk. Shein aliipongeza Benki hiyo kwa kuendelea kutoa huduma zake hapa Zanzibar sambamba na mikakati na malengo yake iliyoyaweka katika kutoa huduma kwa wananchi pamoja na kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Rais Dk. Shein alisisitiza haja kwa Benki hiyo kuongeza matawi yake hapa Zanzibar pamoja na kuipongeza azma yake ya kushirikiana na Serikali katika kuendeleza na kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo.

Pia, Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuupongeza uongozi wa Benki hiyo kwa mipango waliyoipanga ya kuhakikisha Benki hiyo inaleta tija kwa nchi na wananchi wake huku akieleza matarajio yake makubwa katika uongozi wa Mkurugenzi huyo mpya wa Benki hiyo ya CRDB.

Alisisitiza kuwa iwapo Benki hiyo itaendelea  kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi Benki nyengine hapa nchini zitaweza kupanua wigo kutoka Benki hiyo hatua ambayo itapelekea kufuatwa ile dhana ya uzalendo kwani wananchi, Makampuni na hata Serikali wataitumia benki hiyo ikiwemo kukopa fedha badala ya kwenda kukopa kwenye benki za nje ya nchi.

Aidha, Rais Dk. Shein alieleza kuwa Benki ni taasisi ya kiuchumi hivyo, kuongezeka kwa benki hapa Zanzibar ambapo hivi sasa zipo Benki 13 kutaendelea kuongeza ushindani wa kibiashara sambamba na kukuza uchumi wa Zanzibar ambao umekuwa ukiimarika kila uchao.

Katika maelezo yake Rais Dk. Shein alieleza uzoefu alionao wa Benki hiyo kutokana na shughuli zake inazozifanya kwa muda mrefu hapa nchini ikiwa ni pamoja na kuunga mkono sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo kilimo, afya, viwanda, biashara, miundombinu ya barabara, wajasiriamali na mambo mengineyo.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein aliuhakikishia uongozi wa Benki hiyo ya CRDB kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Benki hiyo.

Nae Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Benki ya CRDB Abdulmajid Mussa Nsekela alimueleza Rais Dk. Shein kuwa atahakikisha anatekeleza vyema majukumu yake ili benki hiyo iendelee kupata mafanikio zaidi.

Alieleza jinsi Benki hiyo inavyofanya kazi zake hapa Zanzibar pamoja na Tanzania Bara na kueleza azma ya Benki ya CRDB ya kuunga mkono miradi mbali mbali ya maendeleo hapa Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Aliongeza kuwa Benki hiyo inayomilikiwa na Serikali imekwua ikipata mafanikio makubwa katika utoaji wake wa huduma hali ambayo ilitokana na hatua iliyochukuliwa ya kwenda kwa wananchi.

Alieleza kuwa kwa upande wa Zanzibar Benki hiyo ina matawi mawili hapa Zanzibar ambapo tawi moja liko Unguja na jengine liko Pemba na ina wafanyakazi 42 hapa Zanzibar na wateja wapatao 30,062 ikiwa na Mawakala kwa ujumla 145 (128 kwa Unguja na 17 Pemba) sambamba na kutoa huduma za kifedha katika uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume.

Pamoja na hayo, Mkurugenzi huyo alieleza azma ya Benki hiyo ya kufungua tawi lake jipya hapa Zanzibar huku akionesha maeneo ambayo Benki yake imedhamiria kushirikiana na Zanzibar yakiwemo miundombinu, kilimo, utalii na ukusanyaji mapato.   

Mkurugenzi huyo pia, alitumia fursa hiyo kumueleza Rais Dk. Shein jinsi Benki ya CRDB ilivyodhamiria kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika miradi ya kimkakati kwa lengo la kuendelea kuimarisha uchumi wa Zanzibar.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Ally Hussein Laay kwa upande wake alisema kuwa Benki hiyo inayofuata misingi ya Utawala Bora imekuwa na mikakati na Sera madhubuti katika kuhakikisha inabadilishana madaraka huku akieleza namna Benki hiyo inavyochangia uchumi wa Tanzania.

Aidha, alieleza mafanikio makubwa yaliopatikana tokea kuanza kazi kwa Mkurugenzi Mtendaji mpya Abdulmajib Mussa Nsekela ambaye amechukua nafasi ya aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Charles Kimei ambaye amestaafu.

Mapema Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa akiutambulisha uongozi huo kwa Rais Dk. Shein alieleza jinsi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inavyoshirikiana na Benki hiyo ya CRDB katika mambo mbali mbali.

Pamoja na kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya nchi, Benki ya CRDB imeendelea kutumia mfumo wake imara wa kibiashara ili kutekeleza mkakati wa kuimarisha biashara na uendeshaji wa shughuli zake za kibenki.

Hivi karibuni Benki hiyo imepata tuzo ya Mfuko wa Kimataifa wa Mazingira ambapo ikidhihirisha utekelezaji wa falsafa yake, imekuwa ikiendelea na dhamira ya kutoa huduma bora zaidi kwa wateja pamoja na bidhaa za kifedha za kisasa kwa wateja binafsi na wakubwa kwa kutumia mifumo imara ya tehama na mtandao wake mpana wa huduma.

Azma na dira ya benki hiyo wakati wote imelenga katika kukidhi mahitaji ya wateja huku ikitumia uwezo wa teknolojia kutoa pato zuri kwa wanahisa pamoja na kujali jamii na jumuiya inayowazunguka ikiwa na kauli mbiu yake isemayo “Benki inayomsikiliza mteja”.

Benki ya CRDB ni taasisi ya kibenki nchini Tanzania iliyo na thamani kubwa ya rasilimali, mikopo na amana za wateja ikiwa na lengo la kujipanua katika ukanda wa Afrika Mashariki ambapo mnamo Julai 29, mwaka 2017 Benki hiyo ilizindua Tawi lake jipya kisiwani Pemba.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.