Habari za Punde


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan akifunga Jukwaa la Nishati Tanzania katika Ukumbi wa Varde Zanzibar leo March 11,2020.

HOTUBA YA MHESHIMIWA SAMIA SULUHU HASSAN,
MAKAMU WA RAIS WA JAMUHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA UFUNGAJI WA JUKWAA LA NISHATI TANZANIA, KATIKA UKUMBI WA HOTEL VARDE - ZANZIBAR
TAREHE 11 MACHI, 2020

Mheshimiwa Simai Mohammed Said, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Zanzibar ambaye anamwakilisha Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Zanzibar;

Mheshimiwa Dk. Medard Kalemani, Waziri wa Nishati – Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

Mheshimiwa Salama Aboud Talib, Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati, Zanzibar;

Mheshimiwa Hassan Khatib Hassan, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharib Unguja;

Mheshimiwa Jeroen Verheul, Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania;

Mwenyekiti wa Jukwaa la Nishati ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia;

Waheshimiwa Wabunge na Wawakilishi;
Waheshimiwa Mabalozi wa Nchi mbalimbali mliopo;

Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu wa Wizara mbalimbali za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano ya Tanzania;

Waheshimiwa Mabalozi Wadogo mliopo Zanzibar;

Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa;

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam;

Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam;

Wawakilishi wa Vyuo Vikuu na Taasisi za Utafiti wa Masuala ya Teknolojia vya Uholanzi;

Wakuu wa Taasisi za Umma na Maafisa Wengine wa Serikali;

Wawakilishi wa Makampuni ya Nishati ya Sekta Binafsi na Mashirika yasiyo ya Kiserikali;

Washiriki wa maonyesho;

Waandishi wa Habari;

Wageni Waalikwa;

Mabibi na Mabwana;
Habari za Asubuhi (Mchana),

Kwanza kabisa, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujaalia afya njema na kuweza kujumuika katika tukio hili muhimu.   Pili, napenda kumshukuru Mheshimiwa Riziki Pembe Juma, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali  - Zanzibar, kwa kunipa heshima ya kuwa mfungaji wa Mkutano wa Tatu wa Kimataifa kuhusu Jukwaa la Nishati Tanzania, ambao umefanyika kwa siku tatu hapa Zanzibar. Aidha, nimejulishwa kwamba mkutano wenu ulitanguliwa na maonesho ya nishati na nishati mbadala kutoka Taasisi za Elimu ya Juu, Mashirika ya Umma, Makampuni ya Nishati na Mashirika yasiyo ya Kiserikali yanayojishughulisha na upatikanaji na usambazaji wa nishati mbali mbali.
Nina taarifa pia kwamba katika siku mlizokuwa hapa, zimewasilishwa mada mbalimbali kuhusu masuala yahusuyo Nishati na washiriki wamepata nafasi ya kubadilishana ujuzi na uzoefu kuhusu maendeleo ya nishati ulimwenguni. Nakupongezeni sana kwa kuandaa maonesho na vile vile, kuwasilisha mada zenye mawanda mapana kuhusu nishati ambazo bila shaka washiriki wamenufaika si tu na elimu kupitia mada hizo, lakini pia kuona vitu na mambo mbalimbali yahusuyo nishati kwa ujumla.  Hongereni sana Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia ambayo ndiyo Mwenyekiti wa Mkutano huu, kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam, kwa uratibu na mpangilio mzuri wa uendeshaji wa mkutano huu mkubwa wenye maslahi makubwa kwa wananchi na Taifa letu.
Washiriki na Wageni Waalikwa;
Madhumuni ya Mkutano huu pamoja na mambo mengine, ni kujadili upatikanaji wa nishati hususan nishati endelevu itakayowezesha ujenzi wa uchumi wa viwanda katika nchi yetu. Nimefurahishwa na Kaulimbiu ya Mkutano huu inayosema ENERGY TRANSITION IN SUB SAHARAN AFRICA, ADVANCES IN EDUCATION, INNOVATION AND RESEARCH FOR A NEW GENERATION OF ENERGY PROFESSIONALS. 

Kaulimbiu hii ni mahsusi kabisa na imekuja wakati ambapo nchi yetu inaweka mkazo mkubwa katika elimu hususan masomo ya sayansi na ufundi, uvumbuzi na utafiti.  Nafahamu wataalamu wameijadili kwa kina kaulimbiu hii lakini niseme tu kuwa utekelezaji wake utahitaji utashi wa kisiasa, mipango madhubuti na mikakati ya dhati ambayo itawianishwa na mipango ya Serikali ili kuharakisha upatikanaji wa matokeo tunayoyatarajia.  

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, zimeweka mikakati mbalimbali ya kuwezesha kupatikana kwa nishati safi, yenye gharama nafuu na ya uhakika, katika maeneo yote ya nchi yetu.  Nishati hii itachochea kwa kiasi kikubwa uanzishwaji na uendelezaji wa viwanda nchini na kuiwezesha nchi yetu kufikia Malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya kuwa nchi ya uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.  Kwa dhati kabisa nampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuanzisha na kusimamia miradi mikubwa ya Nishati endelevu ambayo haijawahi kutekelezwa tangu nchi yetu ipate uhuru. Miradi hiyo itakapomalizika itazalisha umeme utakaoifanya Tanzania kujitegemea katika nishati na hata kuwa na ziada ya kuuza kwa nchi za jirani.

Ndugu Washiriki wa Kongamano,
Tunapoliangalia suala la upatikanaji wa nishaji endelevu, hatuna budi kulinasibisha na Mabadiliko ya Tabianchi.  Serikali zetu zinatambua umuhimu wa matumizi ya nishati endelevu siyo tu kutokana na unafuu wa gharama kwa wananchi, lakini pia ni nishati rafiki kwa mazingira. Suala la uharibifu wa mazingira hususan katika nchi za kusini mwa jangwa la Sahara kwa kiasi kikubwa linachangiwa na ukataji wa misitu kwa ajili ya kupata nishati.  Tafiti zinaonesha kwamba ukataji misitu kwa ajili ya kuchoma mkaa ni chanzo kikubwa cha uharibifu wa mazingira na ekolojia ya nchi yetu.  Ripoti ya Benki ya Dunia ya Hali ya Mazingira Tanzania ya mwaka 2017 imeonesha kuwa Tanzania ni moja kati ya nchi zenye kiwango kikubwa cha ukataji wa miti duniani.  Inakisiwa kuwa kiasi cha hekta 483,859 za miti zimekatwa katika kipindi cha 2002 hadi 2013, hii ni wastani wa hecta 48,389 kwa mwaka. 
  
Kutokana na ukweli huo, ndiyo maana Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (2015 – 2020) inaielekeza Serikali kutoa kipaumbele katika nishati za makaa ya mawe, maji (hydro), gesi asilia na nishati jadidifu (renewable energy) inayojumuisha jua na upepo.

Katika kuitekeleza Ilani, leo hii, miradi mikubwa ya nishati inayotekelezwa katika nchi yetu inalenga vyanzo endelevu nilivyovitaja hapo juu. Hivyo basi, ni jukumu lenu kama wasomi na wataalam kuisadia Serikali kufanya tafiti zitakazowezesha upatikanaji wa nishati endelevu kwa kutumia vyanzo visivyoharibu mazingira yetu.

Hivyo, kwa kuwa Mkutano huu utatoka na maazimio mahsusi, rai yangu kwenu ni kujiwekea muda (timeframe) wenye uhalisia utakaowezesha kujipima na kupata matokeo halisi ya utekelezaji wa maazimio hayo, kwa kutumia vigezo vinavyopimika.  Ni vyema mkaepuka kujiwekea malengo makubwa na yasiyotekelezeka au kujiwekea malengo madogo ambayo utekelezaji wake hautakuwa na tija kwa Taifa letu.
Serikali zetu mbili yaani, Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zinayasubiri kwa hamu maazimio ya Mkutano huu ili kuona namna bora ya kusukuma utetekelezaji  wake kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vizazi vijavyo.

Ndugu Washiriki, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,
Nimefurahi kuona kwamba walengwa wakubwa katika Mkutano huu ni wasomi na wataalam wetu kutoka Vyuo Vikuu na Taasisi za elimu ya juu, ambavyo ndivyo vinavyoandaa wataalamu wanaohusika na masuala haya ya tafiti na uvumbuzi wa teknolojia mbalimbali zihusuzo nishati.  Nafahamu zipo changamoto za uhaba wa fedha katika kuendeleza masuala ya tafiti, ila pamoja na changamoto hiyo bado kazi kubwa inafanyika.   Nitumie fursa hii kupongeza kazi kubwa inayofanywa na Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu hapa nchini katika upande wa nishati.   Aidha, nitoe pongezi na shukurani za dhati kwa Vyuo Vikuu vya nchini Uholanzi kwa utayari wao wa kushirikiana na vyuo na taasisi zetu katika kuvijengea uwezo wa kufanya tafiti zinazohusu nishati mbadala.  Ni imani yangu kuwa ushirikiano huu utakuwa na manufaa makubwa kwa taifa letu.  

Rai yangu ni kwa Jukwaa la Nishati Tanzania kuhakikisha kuwa linaratibu vyema na kwa ufanisi kati Taasisi za Serikali, Taasisi za Kitaaluma, Mashirika ya Kimataifa na Wadau wa Sekta ya Nishati ili kazi zao kwa pamoja zifanikishe malengo tuliyojiwekea kitaifa. 

Ndugu Washiriki, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,
Nimalizie hotuba yangu kwa kuwapongeza watu wote ambao kwa namna moja ama nyingine wameshiriki katika hatua mbalimbali za kuandaa maonesho pamoja na Mkutano huu.  Aidha, kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Watanzania, napenda kuishukuru Serikali ya Uholanzi na Umoja wa Vyuo Vikuu vya Uholanzi kwa kutoa msaada wa fedha za kujenga mahusiano na ushirikiano baina ya Vyuo Vikuu vya Nchi zetu katika utaalamu na tafiti zinazohusu nishati. Ni matumaini yangu kuwa ushirikiano huu utaendelezwa.

Sambamba na hilo, naviagiza Vyuo Vikuu vyetu na Tasisi za Elimu ya Juu zilizoko katika Jukwaa la Nishati Tanzania kutumia taaluma zenu ili kuhakikisha kuwa matokeo ya tafiti mnazofanya yanatumiwa na kuleta tija kwa jamii ya Watanzania hasa walioko vijijini, ili waweze kufaidika na matumizi ya nishati safi na ya gharama nafuu.  

Kazi hiyo ya Vichwa na Mikono yenu itakayofanikiwa  kufikisha nishati mbadala vijijini,  itasaidia sana kuacha kukata miti hovyo, na hivyo, kuachana na uharibifu wa mazingira na kurejeleza ekolojia ya nchi yetu.



Washiriki wa Mkutano, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,
Baada ya kusema hayo sasa naomba kutamka rasmi kuwa MKUTANO WA TATU WA KIMATAIFA KUHUSU JUKWAA LA NISHATI TANZANIA umefungwa rasmi.  Nawatakia safari njema ya kurejea majumbani kwenu na kwa wale waliotenga muda wao vizuri niwatakie utalii mwema katika fukwe nzuri na tulivu hapa Zanzibar.

MUNGU AIBARIKI NCHIN YETU
MUNGU AIBARIKI NCHI YA UHOLANZI
MUNGU ABARIKI USHIRIKIANO WETU
ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.