Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) akiwasilisha bungeni mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na ya Kiwango na ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2020/21, Dodoma, ambapo Serikali inatarajia kukusanya na kutumia jumla ya shilingi trilioni 34.88.
MAELEZO YA MHESHIMIWA DKT. PHILIP I. MPANGO (MB), WAZIRI
WA FEDHA NA MIPANGO, AKIWASILISHA
MAPENDEKEZO YA
SERIKALI YA MPANGO WA MAENDELEO WA
TAIFA
NA YA KIWANGO NA UKOMO WA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2020/21
UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi
Mungu, kwa kuendelea kutujalia uhai na afya njema na kutuwezesha wote kukutana
tena hapa Jijini Dodoma, kupokea Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo
wa Taifa na Kiwango cha Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2020/21.
Wasilisho hili ni kwa mujibu wa Kanuni ya 97 (1) na (2) ya Kanuni za Kudumu za
Bunge Toleo la Januari 2016. Aidha, tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea
kuijalia nchi yetu umoja amani na utulivu.
2.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, taarifa hii imegawanyika katika sehemu kuu tatu: Sehemu ya
Kwanza ni Tathmini ya Mwenendo wa Hali ya Uchumi; Sehemu ya Pili ni Mapitio ya
Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2019/20 na Mapendekezo ya Serikali
ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2020/21; na Sehemu ya Tatu ni
Tathmini ya Utekelezaji wa Bajeti kwa Mwaka 2019/20 na Mapendekezo ya Kiwango
cha Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2020/21.
SEHEMU YA KWANZA
TATHMINI YA MWENENDO WA HALI UCHUMI
3.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2020/21 ni ya
mwisho katika utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano
2016/17 – 2020/21 wenye dhima ya kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea
mageuzi ya uchumi na maendeleo ya watu. Aidha, mapendekezo haya yamezingatia
Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015. Katika kipindi hicho cha utekelezaji wa
mpango, mafanikio makubwa yamepatikana kupitia uongozi mahiri wa Mheshimiwa
Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
4.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Katika kipindi cha mwaka 2016 hadi mwaka 2019, Pato la Taifa
lilikua kwa wastani wa asilimia 6.9 kwa mwaka. Ukuaji huu ulichochewa na sekta
ya ujenzi kufuatia kuongezeka kwa uwekezaji hususan katika miundombinu ya
barabara, reli na viwanja vya ndege; kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma za
maji; kuimarika kwa huduma za usafirishaji; kuimarika kwa shughuli za habari na
mawasiliano; kuongezeka kwa uzalishaji wa madini hususan dhahabu na makaa ya
mawe; na kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo. Mwenendo mzuri wa ukuaji
wa Pato la Taifa umechangia kuongezeka kwa ajira 6,032,299, ambapo ajira
1,975,723 ni kutoka sekta rasmi na ajira 4,056,576 ni kutoka katika sekta isiyo
rasmi.
5.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Mojawapo ya malengo ya Serikali ya awamu ya Tano ni
kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu. Moja ya nyenzo za
kutekeleza lengo hilo ni kuzikwamua kaya masikini kutoka katika lindi la
umasikini kupitia utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini Awamu ya Tatu
Kipindi cha Pili kwa Tanzania Bara na Zanzibar, ambapo Serikali imesaini
mkataba na Washirika wa Maendeleo wenye thamani ya dola za Marekani milioni
883.31.
6.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Mfumuko wa bei umeendelea kubaki ndani ya wigo wa tarakimu moja
wa wastani wa asilimia 4.4 kati ya mwaka 2016 na mwaka 2019. Kati ya Julai 2019
hadi Januari 2020 mfumuko wa bei ulifikia wastani wa asilimia 3.7 ambao uko
ndani ya lengo la ukomo la mfumuko wa bei wa nchi za Jumuiya ya Afrika
Mashariki wa asilimia 5. Mwenendo wa mfumuko wa bei nchini kwa mwaka 2019
uliendelea kubaki kwenye wigo wa tarakimu moja kutokana na upatikanaji mzuri wa
chakula, utulivu wa bei za mafuta katika soko la dunia na utekelezaji na usimamizi
madhubuti wa sera za fedha na bajeti.
7.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, ujazi wa fedha umeendelea kukua kwa kasi kulingana na mahitaji
ya shughuli mbalimbali za kiuchumi. Katika mwaka 2019, ujazi wa fedha kwa
tafsiri pana zaidi (M3) uliongezeka na kufikia shilingi bilioni 28,313.1 kutoka
shilingi bilioni 25,823.5 mwaka 2018, ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia
9.6, ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 4.5 mwaka uliotangulia. Ukuaji huo
unadhihirisha kuwepo kwa fedha za kutosha kuendesha shughuli za uchumi na
kuongezeka kwa uwezo wa sekta ya kibenki kutoa mikopo kwa wananchi kwa ajili ya
shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo kilimo, ujenzi na madini.
8.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, mikopo kwa sekta binafsi imeendelea kuongezeka na kufikia
shilingi bilioni 19,695.4 mwaka 2019, kutoka shilingi bilioni 17,726.8 mwaka
2018, sawa na ongezeko la asilimia 11.1, likilinganishwa na ongezeko la
asilimia 4.9 mwaka 2018. Ukuaji huo unaenda sambamba na muendelezo wa
utekelezaji wa sera ya fedha inayolenga kuongeza ukwasi kwenye uchumi, na
utekelezaji wa mpango wa Serikali wa kuboresha mazingira ya biashara nchini.
Aidha, kuimarika huko kwa ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi kumechangiwa na
hatua mbalimbali zilizochukuliwa kupunguza kiwango cha mikopo chechefu, ikiwemo
kuboresha matumizi ya mfumo wa taarifa za wakopaji na kusimamia utekelezaji wa
maadili bora kwa watumishi wa sekta ya kibenki katika kutoa mikopo.
9.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, sekta ya kibenki imeendelea kuwa imara, salama na yenye
kutengeneza faida. Sekta hiyo pia imeendelea kuwa na mtaji na ukwasi wa kutosha
unaowezesha kuendelea kutoa huduma mbalimbali za kibenki kwa ajili ya shughuli
za maendeleo. Katika kipindi kilichoishia Desemba 2019, mtaji wa sekta ya
kibenki uliongezeka na kufikia shilingi bilioni 4,102.7 kutoka shilingi bilioni
3,800.3 mwezi Desemba 2018, ikiwa ni ongezeko la asilimia 8.0. Kiasi hiki cha
mtaji wa msingi ni sawa na asilimia 16.8 ya rasilimali za benki ikilinganishwa
na kiwango cha chini cha kisheria cha asilimia 10.0. Aidha, sekta ya kibenki ilipata
faida ya shilingi bilioni 394.6 ikiwa ni ongezeko la asilimia 221.9 kutoka
faida ya shilingi bilioni 122.6 iliyopatikana mwaka 2018. Amana za sekta ya
kibenki zimekua na kufikia shilingi bilioni 23,807.0 mwaka 2019 kutoka shilingi
bilioni 22,226.5 mwaka 2018, ikiwa ni
ongezeko la asilimia 7.1. Ongezeko hilo linaashiria kuongezeka kwa upatikanaji
wa huduma za kibenki kwa wananchi ikiwemo mikopo.
10.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, ukwasi kwenye sekta ya kibenki umeendelea kuwa katika viwango
vya juu ya kiwango cha kisheria cha asilimia 20 na kufikia asilimia 32.4 mwezi
Desemba 2019. Aidha, rasilimali katika sekta ya kibenki ziliongezeka na kufikia
shilingi bilioni 33,067.4 kutoka shilingi bilioni 30,374.0 mwaka 2018 ikiwa ni
ongezeko la asilimia 8.9. Vile vile, ubora wa rasilimali za sekta ya kibenki
uliimarika kama inavyodhihirishwa na kupungua kwa uwiano wa mikopo chechefu
kutoka asilimia 10.7 Desemba 2018 hadi kufikia asilimia 9.8 ya mikopo yote
Desemba 2019. Serikali kupitia Benki Kuu imeendelea kuchukua hatua mbalimbali
katika kupunguza uwiano wa mikopo chechefu ili kufikia lengo la asilimia 5.
Baadhi ya hatua zilizochukuliwa ni pamoja na, kuzitaka benki na taasisi za
fedha kuboresha usimamizi katika utoaji mikopo; kutekeleza mpango kazi wa
kupunguza uwiano wa mikopo chechefu kwa benki zilizokuwa na uwiano mkubwa; na
matumizi ya lazima ya taarifa za wakopaji zilizo kwenye kanzidata ya wakopaji
kabla ya utoaji wa mikopo.
11.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika kuhakikisha kuwa huduma za kibenki zinawafikia wananchi wengi
wakiwemo waliopo vijijini, Benki Kuu imeruhusu benki kutoa huduma za kibenki
kupitia kwa mawakala. Kumekuwepo na mafanikio makubwa katika utoaji wa huduma
za kibenki kwa njia hii ambapo hadi kufikia Desemba 2019, benki 21 zilikuwa
zinatoka huduma hiyo kwa kutumia mawakala ikilinganishwa na benki 17 zilizokuwa
zinatoa huduma hiyo Desemba 2018. Aidha, Desemba 2019 kulikuwepo na mawakala
28,358 nchi nzima ikilinganishwa na mawakala 18,827 waliokuwepo Desemba 2018,
likiwa ni ongezeko la asilimia 50.6. Kiasi cha amana kilichowekwa kwenye benki
kupitia mawakala wa benki kilifikia shilingi bilioni 5,464.9 Desemba 2019
ikilinganishwa na kiasi cha shilingi bilioni 3,402.7 kilichokuwepo Desemba
2018, ikiwa ni ongezeko la asilimia 60.6 wakati kiasi cha amana kilichochukuliwa
kwenye benki kupitia mawakala kilifikia shilingi bilioni 1,833.1 Desemba 2019
ikilinganishwa na shilingi bilioni 1,051.1 Desemba 2018, ikiwa ni ongezeko la
asilimia 74.4.
12.
Mheshimiwa
Mwenyekiti,kwa mwaka 2019, riba ya amana ya mwaka mmoja ilifikia wastani wa
asilimia 8.78 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 8.80 mwaka 2018. Aidha,
riba za mikopo zilipungua kufikia wastani wa asilimia 16.97 mwaka 2019 kutoka
asilimia 17.43 mwaka 2018. Vile vile, riba ya mikopo ya mwaka mmoja imepungua
na kufikia wastani wa asilimia 16.69 kutoka asilimia 18.25.
13.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka 2019, nakisi kwenye urari wa biashara
ya bidhaa, huduma na uhamisho mali nchi za nje ulipungua hadi kufikia dola za
Marekani milioni 1,623.0, ikilinganishwa na nakisi ya dola za Marekani milioni
2,204.6 mwaka 2018. Kupungua huku kulitokana na kuongezeka kwa mauzo nje ya
nchi, hususan, bidhaa asilia na zisizo asilia kama vile dhahabu na bidhaa za
viwandani. Kwa kiasi kikubwa, nakisi kwenye urari wa biashara ya bidhaa, huduma
na uhamisho mali nchi za nje yalifidiwa na mitaji mikubwa ya moja kwa moja na
mikopo kutoka nje ya nchi.
14.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Mauzo ya bidhaa na huduma nje, yalikuwa dola za Marekani
milioni 9,712.6, ikilinganishwa na dola za Marekani milioni 8,398.3 mwaka 2018.
Thamani ya mauzo ya bidhaa zisizo asilia iliongezeka na kufikia dola za
Marekani milioni 4,236.6 mwaka 2019 ikilinganishwa na dola za Marekani milioni
3,209.3 zilizopatikana mwaka uliotangulia. Matokeo haya yalichangiwa na kuongezeka
kwa uzalishaji dhahabu sambamba na ongezeko la bei katika soko la dunia.
Vilevile, mauzo ya bidhaa asilia yaliongezeka hadi dola za Marekani milioni
829.9 mwaka 2019 kutoka dola za Marekani milioni 772.1 mwaka 2018, kutokana na
kuongezeka kwa thamani ya bidhaa za korosho, kahawa na pamba.
15.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, thamani ya uagizaji bidhaa na huduma kutoka nje ilikuwa dola za
Marekani milioni 10,984.8, sawa na ongezeko la asilimia 7.7 kutoka dola za
Marekani milioni 10,197.8 mwaka 2018.
Ongezeko hili lilichangiwa na uagizaji wa malighafi pamoja na mashine sambamba
na utekelezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu ya reli, barabara na uzalishaji
umeme.
16.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Desemba 2019, akiba ya fedha za
kigeni ilifikia dola za Marekani milioni 5,567.6, kiasi kinachotosheleza kulipia
uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi cha miezi 6.4.
Kiwango hiki ni zaidi ya lengo la nchi la kuwa na akiba ya kutosha kuagiza
bidhaa na huduma nje ya nchi kwa muda wa miezi 4, ikiwa pia ni juu ya lengo
lililokubalika katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki la miezi
isiyopungua 4.5 na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika la miezi isiyopungua
6.
17.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya sarafu nyingine kubwa
duniani imeendelea kuwa tulivu kwa kipindi chote cha mwaka 2019. Hali hii
ilitokana na utekelezaji mzuri wa sera ya fedha na ya kibajeti, pamoja na
kupungua kwa nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamisho mali
nchi za nje. Aidha, utulivu huo wa shilingi ya Tanzania ulichangiwa pia na
hatua zilizotekelezwa na Benki Kuu katika kuhakikisha uwazi na utaratibu mzuri
wa ununuzi na uuzaji wa fedha za kigeni nchini. Utulivu wa thamani ya shilingi
umechangiwa pia na utulivu wa mfumuko wa bei kubaki katika viwango vya chini
hali iliyopelekea kuwa na utofauti mdogo wa mfumuko wa bei kati ya Tanzania na
washirika wake wa biashara. Katika kipindi hicho, dola moja ya Marekani
ilibadilishwa kwa wastani wa shilingi 2,299.8 katika soko la fedha la jumla
ikilinganishwa na wastani wa shilingi 2,275.4 mwaka 2018.
18.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Sheria ya Huduma Ndogo
za Fedha ilipitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo mwezi
Novemba 2018. Pamoja na mambo mengine, Sheria hiyo inaipa Benki Kuu nguvu na
wajibu wa kusimamia watoa huduma ndogo za fedha (Microfinance Service
Providers) waliogawanywa katika madaraja manne yaani benki za huduma ndogo za
fedha (microfinance banks); watoa huduma ndogo za fedha wasiopokea amana
(nondeposit taking microfinance service providers); vyama vya akiba na mikopo
(Savings and Credit Cooperative Societies); na vikundi vya kijamii (community
microfinance groups).
19.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Benki Kuu kwa
kushirikiana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika (Tanzania Cooperative Development
Commission) na Mamlaka ya Serikali za Mitaa (Local Government Authorities)
imeanza utekelezaji wa Sheria na Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha ikiwemo
kusajili watoa huduma ndogo za fedha katika madaraja yote. Aidha, Benki Kuu
inashirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango katika kuutekeleza mpango wa elimu
kwa umma kuhusu Sera, Sheria na Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha (Public
Awareness Programme on Microfinance Policy, Law and Regulations). Sheria na
Kanuni hizi mpya zitasaidia kuimarisha mfumo wa taarifa za wakopaji, kutatua
malalamiko ya watumiaji wa huduma ndogo za fedha ikiwemo riba kubwa na
ukusanyaji wa madeni usiozingatia maadili. Sheria na Kanuni hizi pia zitasaidia
kuongezeka kwa huduma jumuishi za fedha na elimu ya masuala ya fedha kwa
wananchi wanaotumia huduma hizo.
20.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Serikali ya Awamu Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John
Pombe Joseph Magufuli, itaendelea kutekeleza na kusimamia sera madhubuti za
fedha na bajeti ili kuhakikisha uchumi wa nchi yetu unaendelea kuwa imara,
jumuishi na endelevu.
SEHEMU YA PILI
TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MWAKA 2019/20 NA MAPENDEKEZO YA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA
2020/21
A. TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2019/20
21.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika mwaka 2019/20 jumla ya shilingi trilioni 12.25
zilitengwa kugharamia miradi ya maendeleo ambapo shilingi trilioni 9.74
zilikuwa fedha za ndani na shilingi trilioni 2.51 ni fedha za nje. Hadi Januari
2020, jumla ya shilingi trilioni 6.22 zilitolewa kwa ajili ya kugharamia miradi
ya maendeleo sawa na asilimia 71.9 ya lengo la shilingi trilioni 8.67. Aidha,
Serikali imetumia shilingi trilioni 5.80 kulipia deni la Serikali lililotokana
na mikopo iliyotumika kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo. Baadhi ya miradi hiyo ni: mradi wa maji Arusha; mradi
wa maji Ruvu chini; mradi wa kufua umeme wa Kinyerezi, mradi wa njia ya
kusafirisha umeme wa msongo wa Kv 400 kutoka Singida – Arusha – Namanga;
upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Zanzibar; Mradi wa Kuboresha Huduma katika mji
wa Zanzibar; Mradi wa Serikali Mtandao Awamu ya Pili Zanzibar; ujenzi wa Jengo
la tatu la abiria katika kiwanja cha ndege cha Julius Nyerere; ukarabati wa
viwanja vya ndege vya Mtwara, Kigoma, Shinyanga, Sumbawanga na Mwanza;
ukarabati wa reli ya kati; na uboreshaji wa bandari ya Dar es Salaam.
22.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, mafanikio makubwa sana yamepatikana katika utekelezaji wa
miradi ya maendeleo kuanzia mwaka 2016/17 hadi Januari 2020 chini ya utawala wa
Rais Magufuli na Serikali yake ya CCM. Naomba niwaeleze Waheshimiwa Wabunge na
Watanzania kwa ujumla baadhi ya mafanikio ya kujivunia kama ifuatavyo:
(i)
Ujenzi wa
Reli ya Kati kwa kiwango cha Standard Gauge: Ujenzi wa kipande cha Dar es
Salaam – Morogoro (km 300) umefikia asilimia 75 na kwa kipande cha Morogoro –
Makutupora (km 422) asilimia 25. Hadi Septemba 2019, mradi huu umezalisha
takribani ajira 13,117. Aidha, zabuni zenye thamani ya shilingi bilioni 664.7
zimetolewa kwa wazabuni na makandarasi wa ndani 640. Jumla ya shilingi trilioni
2.96 zimetumika kugharamia mradi huu zikijumuisha shilingi bilioni 237.5
zilizotolewa katika kipindi cha Julai 2019 hadi Januari 2020;
(ii)
Ujenzi wa
Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere - Mw 2,115: kazi
zilizokamilika ni pamoja naujenzi wa miundombinu wezeshi ya mradi (njia ya
kusafirisha umeme, barabara kwa kiwango cha changarawe, mfumo wa maji,
mawasiliano ya simu na nyumba za makandarasi); ujenzi wa daraja la muda namba
2; utafiti wa miamba na udongo; na uchimbaji wa mtaro wa chini kwa chini (adit
tunnel) wenye urefu wa mita 147.6 kuelekea kwenye mtaro wa chini kwa chini wa
kuchepua maji na mtambo wa kuchakata kokoto namba moja ambapo utekelezaji wa
mradi wote umefikia asilimia 10.74. Jumla ya shilingi trilioni 1.28 zimetumika
kugharamia mradi huu ikijumuisha shilingi
bilioni 200.7 ambazo zimetolewa katika kipindi cha Julai 2019 hadi Januari
2020. Mradi huu umezalisha ajira zipatazo 3,074 na kutoa fursa kwa makandarasi
wa kampuni 10 za Kitanzania;
(iii)
Kuboresha
Shirika la Ndege Tanzania: Serikai imeendelea kuboresha Shirika la Ndege
Tanzania kwa kununua ndege mpya 11 ambapo ndege nane (8) mpya zenye thamani ya
shilingi trilioni 1.27 zimepokelewa na malipo ya awali ya shilingi bilioni 85.7
kwa ajili ya ununuzi wa ndege nyingine mpya tatu
(3) yamefanyika ambapo ndege
mbili (2) ni aina ya Airbus A220-300 na moja (1) ni aina ya De Havilland Dash
8-400; kuongezeka kwa idadi ya vituo vya safari za ndani kufikia 13 na nje
kufikia sita (6) ambavyo ni Hahaya (Comoro), Entebbe (Uganda), Bujumbura
(Burundi), Mumbai (India), Lusaka (Zambia) na Harare (Zimbabwe). Aidha,
Serikali imekamilisha ukarabati wa karakana ya matengenezo ya ndege katika
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA); na kugharamia mafunzo ya
marubani (110), wahandisi (127) na wahudumu (125). Hadi Septemba 2019, mradi
huu umezalisha ajira 436;
(iv)
Miradi ya
Umeme: Shughuli zilizotekelezwa ni: kukamilika kwa mradi wa njia ya
kusafirisha umeme wa Msongo wa kV 220 kutoka Makambako – Songea ambapo shilingi
bilioni 160.1 zimetumika; kuendelea na
ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa kV 400 kutoka Singida – Arusha – Namanga
ambapo utekelezaji umefikia asilimia 63 na shilingi bilioni 219.4 zimetumika
katika kipindi cha Julai 2016 hadi Januari 2020; kuendelea na utekelezaji wa
miradi ya usambazaji umeme vijijini kupitia REA ambapo jumla ya vijiji 8,641
kati ya vijiji 12,268 vya Tanzania Bara vimeunganishwa umeme, sawa na asilimia
70.4. Katika kipindi cha Julai 2015 hadi Januari 2020, jumla ya shilingi
trilioni 1.53 zimetumika katika utekelezaji wa mradi huu ikijumuisha shilingi
bilioni 207.2 zilizotolewa katika kipindi cha Julai 2019 hadi Januari 2020;
kuendelea na utekelezaji wa mradi wa
Kinyerezi I Extension – (MW 185) ambapo ufungaji wa mitambo yote minne (4)
umeanza; na kuendelea na upanuzi (upgrade) wa njia ya msongo wa KV 132 kutoka
Kinyerezi I hadi kituo cha kupoza umeme cha Gongo la Mboto ambapo utekelezaji
umefikia asilimia 85; na kuendelea na utekelezaji wa mradi wa kufua umeme wa
Rusumo (MW 80) ambao umefikia asilimia 60 na shilingi bilioni 9.4 zimetolewa
kugharamia mradi huu;
(v)
Miradi ya
Maji Mijini na Vijijini: Serikali imeendelea kuboresha huduma ya maji safi
na salama vijijini na mijini ambapo utekelezaji wa miradi 875 unaendelea
ikijumuisha miradi 802 ya maji vijijini na miradi 73 ya maji mijini ambapo
miradi 75 ya maji vijijini imekamilika. Miongoni mwa miradi mikubwa
inayoendelea kutekelezwa ni pamoja na: mradi wa maji Arusha; mradi wa maji wa Same – Mwanga – Korogwe, ambapo katika mji
wa Same utekelezaji umefikia asilimia 73 na Mwanga asilimia 38 na ujenzi wa
mtambo wa kusafisha maji umefikia asilimia 81; na mradi wa kutoa maji kutoka
Ziwa Victoria kwenda katika miji ya Isaka, Tinde, Kagongwa, Tabora, Igunga,
Uyui na Nzega ambapo ujenzi wa matanki 17 na ulazaji wa mabomba makubwa ya
kusafirisha maji kutoka kijiji cha Solwa – Nzega – Tabora – Igunga (km 290.7)
umekamilika. Aidha, ulazaji wa mabomba ya matawi umefikia asilimia 86 na
ulazaji wa mabomba ya usambazaji maji mijini na vijijini umefikia asilimia
98.6. Hivyo, utekelezaji wa miradi ya maji umewezesha kiwango cha upatikanaji
wa maji vijijini kufikia asilimia 64.8, katika miji ya mikoa asilimia 84, Dar
es Salaam asilimia 85 na katika miji midogo asilimia 64. Jumla ya shilingi
bilioni 146.7 zimetolewa katika kipindi cha Julai 2019 hadi Januari 2020;
(vi)
Miradi ya
Afya: Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kuboresha utoaji wa huduma za
afya kwa kugharamia ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya vituo 540 vya
kutolea huduma za afya ikijumuisha vituo vya afya 361, hospitali za halmashauri
za wilaya 71, hospitali za zamani 9 na zahanati 99 ambapo watumishi 477 wameajiriwa na kupangwa kwenye vituo
hivyo. Aidha, Serikali imefanikisha ununuzi wa dawa, chanjo, vifaa, vifaa tiba
na vitendanishi ikijumuisha vifaa tiba vya kisasa katika hospitali ya Moyo ya
Jakaya Kikwete; kujenga na
kuboresha miundombinu ya hospitali za rufaa za Njombe, Simiyu, Mara, Geita,
Songwe, Katavi, Sekou Toure (Mwanza), Burigi - Geita, Mwananyamala – Dar es
Salaam na hospitali za rufaa za kanda ya kusini Mtwara, kanda ya nyanda za juu
kusini Mbeya, hospitali ya Kibong’oto na ujenzi wa Isolation centre katika
hospitali ya Taifa Muhimbili. Vile vile,
madaktari 646 wamegharamiwa mafunzo ya kibingwa kwenye fani mbalimbali
katika vyuo vikuu vya ndani na nje ya nchi; na kukamilika kwa nyumba 320 za
watumishi wa sekta ya afya. Katika mwaka 2019/20 vituo vya afya 133 vimejengwa
kwa gharama ya shilingi bilioni 64.64; na katika kipindi cha Julai 2015 hadi
Januari 2020 jumla ya shilingi trilioni 3.01 zimetumika kugharamia huduma za
afya ikijumuisha shilingi bilioni 14.5 zilizotumika kununua mashine ya Positron
Emmission Tomography (PET scan) kwa ajili ya hospitali ya Ocean Road;
(vii)
Miradi ya
Elimu: mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuendelea na ujenzi na
ukarabati wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia; kukamilika na
kuzinduliwa kwa Maktaba ya Kimataifa yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 2,600
kwa wakati mmoja pamoja na hosteli za wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam; utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu; uimarishaji wa vyuo vya
VETA na kukuza ujuzi kwa vijana nchini ambapo jumla ya shilingi bilioni 371.2
zimetolewa kugharamia shughuli hizo; na shilingi bilioni 9.1 zimetolewa
kugharamia ukamilishaji wa maboma 364 ya nyumba za walimu wa shule za msingi.
Aidha, kupitia programu ya EP4R yamenunuliwa
magari 39 na kusambazwa katika vyuo vyote vya ualimu vya Serikali,
kukamilika kwa taratibu za ununuzi wa magari 65 kwa ajili ya kuimarisha
uthibiti ubora wa shule pamoja na magari matano (5) na Malori mawili (2) kwa
ajili ya Baraza la Mitihani la Taifa. Elimumsingi
Bila Ada: Serikali imeendelea kugharamia posho ya madaraka kwa walimu
wakuu; fidia ya ada kwa wanafunzi 1,874,331 na ruzuku ya uendeshaji wa shule
ambapo shilingi bilioni 145.6 zilitolewa kwa ajili ya kugharamia elimumsingi
bila ada;
(viii)
Mpango wa
Kunusuru Kaya Masikini katika Awamu ya Tatu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii
(TASAF III): Serikali imendelea na utekelezaji wa mkakati wa uwezeshaji wa
kaya maskini kiuchumi, ambapo kwa sasa inatekeleza Awamu ya III ya TASAF. Jumla
ya kaya 1,067,041 zenye wanakaya 5,130,001 zimetambuliwa na kuandikishwa katika
vijiji na mitaa 9,627 kwenye Halmashauri 159 Tanzania Bara na kaya 32,248 zenye
wanakaya 169,999 katika shehia 204 za Zanzibar na ruzuku ya fedha shilingi
bilioni 968.73 imehawilishwa katika kaya hizo. Kati ya hizo, shilingi bilioni
935.94 ni kwa Tanzania Bara na shilingi bilioni 32.79 ni kwa Zanzibar. Kazi
nyingine zilizofanyika ni: kutekelezwa kwa miradi 8,384 ambayo imezalisha ajira
za muda kwa kaya zipatazo 230,738 katika Halmashauri 42 Tanzania Bara na kaya
14,555 katika miradi 251 kwa Zanzibar; kuundwa kwa vikundi vya kuweka akiba
16,366 vyenye wanachama 226,050 kwenye halmashauri 44 Tanzania Bara ambavyo
vimeweka akiba ya shilingi bilioni 2.5
na kutoa
mikopo yenye thamani ya shilingi
bilioni 1.13. Aidha, vikundi 1,957 vyenye wanachama 27,398 Zanzibar vimeweka
akiba ya shilingi bilioni 1.1 na shilingi milioni 628.0 zimekopeshwa. Vile
vile, miradi 47 ya kuendeleza miundombinu katika sekta za elimu, afya na maji Tanzania Bara na miradi 8 katika
sekta za elimu na afya kwa Zanzibar
imekamilika.
(ix)
Kilimo,
Mifugo na Uvuvi: Katika sekta ya Kilimo
zimezalishwa na kusambazwa tani 10 za mbegu mpya za mpunga kwa wakulima 3,050;
kusambazwa mbolea tani 492,394.2 katika mikoa yote ya Tanzania Bara; kununuliwa
na kuhifadhiwa tani 3,841.9 za mahindi kupitia wakala wa Taifa wa Hifadhi ya
Chakula (NFRA); na kuzalisha miche 3,692,780 ya kahawa na kusambaza mbegu bora
za korosho zitakazozalisha miche 6,647,760. Mifugo: baadhi ya mafanikio ni pamoja na kuendelezwa kwa mashamba
matano (5) ya kuzalisha mitamba; kuzalishwa na kusambazwa kwa mitamba 15,097 ya
ng’ombe wa maziwa; kununuliwa na kusambazwa kwa lita 8,823.53 za dawa aina ya
Paranex ya kuogesha mifugo; na kukarabatiwa kwa majosho 1,129 na utoaji wa
chanjo ya ndigana kali (east coast fever) kwa ng’ombe 70,260. Jumla ya shilingi
milioni 892.9 zilitolewa kugharamia miradi hiyo ikijumuisha shilingi milioni
154.7 zilizotolewa katika kipindi cha Julai 2019 hadi Januari 2020. Uvuvi: mafanikio yaliyopatikana ni
pamoja na upandikizaji wa vifaranga 18,700 na uzalishaji wa vifaranga
15,041,401 vya samaki; kukamilika kwa upembuzi yakinifu wa ujenzi wa bandari ya
uvuvi; kupungua kwa uvuvi haramu kwa asilimia 80 kwa maji baridi na asilimia
100 kwa uvuvi wa milipuko katika mwambao wa Bahari ya Hindi; kununuliwa kwa
mtambo wa automatic identification system wenye uwezo wa kuona meli zinazoingia
na kuvua katika ukanda wa uchumi wa bahari kuu; na kuongezeka kwa uvunaji wa
samaki (maji ya asili) kutoka tani 448,400 hadi tani 470,309.23;
(x)
Uendelezaji
wa Viwanda: kazi zilizotekelezwa ni upanuzi wa Kiwanda cha Ngozi na Bidhaa
za Ngozi cha Karanga (Moshi) na kuimarisha Shirika la Nyumbu (Pwani) ili
kuongeza uzalishaji ikiwemo magari ya zimamoto; kufutwa na kupunguzwa kwa ada
na tozo 54 ili kuondoa kero na urasimu kwa wafanyabiashara na wawekezaji;
kuzinduliwa na kuanza uzalishaji katika viwanda saba (7) ambavyo ni kiwanda cha
Pipe Industries Co. Limited (Dar es Salaam), kiwanda cha chai cha Kabambe
(Njombe), kiwanda cha Yalin Cashewnut Company Ltd (Mikindani – Mtwara), kiwanda
cha 21st Century Food and Packaging (Dar es Salaam), kiwanda cha kusaga mahindi
cha kampuni ya Mohamed Enterprises Tanzania Limited – MeTL (Dar es Salaam),
kiwanda cha bidhaa za plastiki cha Plasco Pipelines Co. Ltd (Dar es Salaam),
kiwanda cha kupakia na kuhifadhi parachichi - Rungwe Avocado (Mbeya) na kiwanda
cha kuchakata parachichi kwa ajili ya kutengeneza mafuta (KUZA Afrika). Aidha,
jumla ya tani 4,254.1 za korosho zilibanguliwa kupitia viwanda 17 na kuwezesha
kuzalishwa kwa fursa za ajira za moja kwa moja 4,066.
Kwa kipindi cha mwaka
2016/17 - 2019/20, jumla ya viwanda vikubwa 201,
vya kati 460, vidogo 3,406 na
vidogo sana 4,410 vilianzishwa.
(xi)
Madini:
Serikali imepitia na kurekebisha sera, sheria na mikataba ya uwekezaji katika
sekta ya madini ambapo marekebisho hayo yamewezesha kuanzishwa kwa Kampuni mpya
ya Twiga Minerals Corporation inayomilikiwa kwa ubia kati ya Serikali (hisa
asilimia 16) na Kampuni ya Barrick (hisa asilimia 84); kuanzishwa kwa masoko 28
na vituo 25 vya ununuzi wa madini; na kukamilika kwa ujenzi wa vituo vinne (4)
vya umahiri katika maeneo ya Bariadi, Musoma, Bukoba na Handeni na kuendelea na
ujenzi wa vituo vya Songea, Mpanda na Chunya; na kukamilisha uandaaji wa
Mwongozo wa Mpango wa Utunzaji wa Mazingira. Katika kipindi cha mwaka 2016/17
hadi Februari 2020, jumla ya shilingi
trioni 1.18 zilikusanywa kutokana na maduhuli kwenye sekta ya madini, sawa na
wastani wa shilingi bilioni 294.41 kwa mwaka ikilinganishwa na wastani wa
shilingi bilioni 142.53 tu kwa mwaka katika kipindi cha mwaka 2010/11 hadi
2014/15. Ongezeko hili ni sawa na ukuaji wa asilimia 106.6. Mfaninkio haya ni
matokeo ya hatua madhubuti zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano katika
kuboresha sekta ya madini ili kuwezesha Taifa kunufaika na rasilimali zake;
(xii)
Ujenzi wa
Barabara na Madaraja: Katika ujenzi wa Barabara
shughuli zinazoendelea ni ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami zikiwemo
barabara kuu, barabara za mikoa na wilaya ambapo hadi Desemba 2019 mtandao wa
barabara kuu umefikia km 8,671 na mtandao wa barabara za mikoa km 1,808;
barabara ya njia nane kutoka Kimara hadi Kibaha (km 19) umefikia asilimia 63;
na ujenzi wa Ubungo Interchange ambao umefikia asilimia 65. Madaraja: Serikali imeanza maandalizi
ya ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi (Mwanza) lenye urefu wa mita 3,200 na
upana wa mita 28.45 ambapo malipo ya awali ya shilingi bilioni 61.4
yamefanyika; ujenzi wa daraja jipya la Selander unaendelea na umefikia asilimia
25; ujenzi wa madaraja yafuatayo ya Mfugale na Mlalakuwa (Dar es Salaam),
Magufuli katika mto Kilombero (Morogoro), Momba (Rukwa), Sibiti (Singida), Mara
(Mara), Ruhuhu (Ruvuma), Msingi (Singida), Lukuledi (Lindi) na Kavuu (Katavi).
Aidha, ujenzi unaendelea wa madaraja ya Mangara (Manyara) asilimia 94, New Wami
(Pwani) asilimia 35; na Kitengule (Kagera) asilimia 42. Jumla ya shilingi
trilioni 3.60 zimetolewa katika kipindi cha Novemba 2015 hadi Januari 2020
kugharamia miradi ya barabara na
madaraja ikijumuisha shilingi bilioni 703.6 zilizotolewa katika kipindi cha
Julai 2019 hadi Januari 2020;
(xiii)
Ujenzi wa
Meli na Vivuko: mafanikio yaliyopatikana ni kukamilika kwa ujenzi wa meli
mpya ya MV Mbeya yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na mizigo tani 200 katika
Ziwa Nyasa; kuendelea na ujenzi wa meli mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200
na tani 400 za mizigo katika Ziwa Victoria ambapo utekelezaji umefikia asilimia
52 na ujenzi wa chelezo umefikia asilimia 80; ukarabati wa meli ya MV Victoria
umefikia asilimia 75 na MV Butiama asilimia 70; awamu ya kwanza ya upanuzi wa
maegesho ya Magogoni - Kigamboni imekamilika;
jengo la abiria na ofisi ya kivuko cha Lindi – Kitunda limekamilika na
kukabidhiwa; vivuko vya MV Kigamboni, Kigongo – Busisi na MV Utete pia
vimekamilika na tunaendelea na ujenzi wa vivuko vipya vya Nyamisati - Mafia
(asilimia 28), Bugolora - Ukara (asilimia 40), Chato - Nkome na Kayenze Bezi
(asilimia 98); shughuli nyingine ni kununuliwa kwa kivuko kipya chenye uwezo wa
kubeba tani 170 (Magogoni - Kigamboni); kuendelea na ukarabati wa vivuko vya MV
Sengerema (asilimia 70) na MV Misungwi (asilimia 20). Jumla ya shilingi bilioni
81.5 zimetumika kugharamia ujenzi na ukarabati wa meli na vivuko ikijumuisha
shilingi bilioni 38.8 zilizotolewa katika kipindi cha Julai 2019 hadi Januari
2020;
(xiv)
Viwanja
vya Ndege: Jengo la III la abiria katika kiwanja cha Ndege cha Kimataifa
cha Julius Nyerere lilikamilika na kuanza kutumika ambapo shilingi bilioni 722.1 zimetumika kugharamia
mradi huu; ujenzi na uboreshaji wa kiwanja cha ndege cha Mwanza umefikia
asilimia 99.5; uboreshaji wa kiwanja cha Nachingwea umekamilika; ujenzi na
ukarabati wa viwanja vya Geita (asilimia 78) na Songea (asilimia 34)
unaendelea. Jumla ya shilingi bilioni 10.9 zilitolewa katika kipindi cha Julai
2019 hadi Januari 2020 kugharamia miradi hiyo;
(xv)
Uendelezaji
wa Bandari: ujenzi wa gati Na.1, 2, 3 na gati la kupakia na kupakua magari
(Ro-Ro) katika bandari ya Dar es Salaam umekamilika ambapo meli yenye uwezo wa
kubeba magari 6,000 imehudumiwa; ujenzi wa gati lenye urefu wa mita 300 katika
bandari ya Mtwara umefikia asilimia 60; na ukarabati wa gati namba 2 na
kuongeza kina cha bandari ya Tanga unaendelea ambapo utekelezaji umefikia
asilimia 60;
(xvi)
Ukarabati
wa Reli: Serikali imendeleana ukarabati wa reli ya kati ikijumuisha
njia ya reli, madaraja na ujenzi wa
makalavati kwa vipande vya Dar es Salaam – Ngerengere (km 145) ambapo
utekelezaji umefikia asilimia 89.14, Ngerengere - Kilosa (km 138) asilimia
59.43, Kilosa - Itigi (km 343) asilimia 82.57 na Itigi - Isaka (km 344)
asilimia 82.05; ukarabati wa reli ya Tanga – Arusha (km 439) umeendelea ambapo
ukarabati wa kipande cha reli ya Tanga – Moshi (km 353) umekamilika na kuanza
kusafirisha abiria na mizigo; na ukarabati wa kipande cha Moshi – Arusha (km
86) umeendelea kwa kubadili reli na mataruma, kurejesha madaraja na makalavati,
kukarabati stesheni na kufungua mifereji ya maji ya mvua ambapo utekelezaji
umefikia asilimia 90;
(xvii)
Rada za
Kuongozea Ndege na za Hali ya Hewa: miundombinu ya rada, na ufungaji wa
mitambo umekamilika, majaribio ya mitambo kwa rada za kuongozea ndege za kiraia
yanaendelea katika viwanja vya ndege vya JNIA, KIA na Mwanza; malipo ya ununuzi
wa Rada tatu (3) za hali ya hewa zitakazofungwa Mtwara, Mbeya na Kigoma
yamefanyika kwa asilimia 90. Jumla ya shilingi bilioni 17.8 zimetolewa
kugharamia miradi hiyo kwa kipindi cha mwaka 2016/17 hadi Januari 2020;
(xviii)
Miradi ya
Mahakama: Serikali imekamilishaujenzi wa majengo ya Mahakama Kuu Kigoma na
Mara, majengo ya Mahakama za Hakimu Mkazi Manyara, Simiyu na Geita na majengo
ya mahakama za wilaya za Longido, Chato, Bukombe, Bariadi, Njombe, Ruangwa,
Kilwa, Chunya na Kondoa; ujenzi wa nyumba nne (4) za Majaji (Kigoma 2 na Musoma
2) umekamilika; na tunaendelea na ukarabati mkubwa wa Mahakama Kuu Sumbawanga.
Jumla ya shilingi bilioni 28.6 zimetolewa kugharamia miradi hiyo ikijumuisha
shilingi bilioni 3.5 zilizotolewa katika kipindi cha Julai 2019 hadi Januari
2020;
(xix)
Udhibiti
wa Uhalifu na Utoaji Haki: Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa kushirikiana na
wadau, imeendesha kesi na kufanikiwa kupata amri ya Mahakama kutaifisha jumla
ya kilo 398.145 za Dhahabu zenye thamani ya shilingi bilioni 32.30 zilizokuwa
zinatoroshwa. Madini mengine yaliyotaifishwa ni madini ya bati na madini vito aina ya Almasi, Tanzanite, Amethyst,
Rhodolite, Blue Sapphire, grossularite, Tsavorite, Green Garnet, Spessartite,
Cintrine, Grossular, Supphire,
Spinel, Ruby, Tourmaline na Acuamarine.
Jumla ya thamani ya madini yote pamoja na faini zilizolipwa na washitakiwa
ni shilingi bilioni 42.27. Aidha,
shilingi bilioni 17.22 zimetaifishwa kutoka kwa wahalifu mbalimbali na kuwekwa
kwenye akaunti ya Asset Forfeiture Recovery iliyoko Benki Kuu ya Tanzania. Vile vile, jumla ya shilingi bilioni 13.52
zimelipwa kutoka kwa washitakiwa
waliokiri makosa yao (plea bargain) ya ukwepaji kodi. Hivyo, hadi Januari 2020
jumla ya shilingi bilioni 73.0 zililipwa kutokana na makosa mbalimbali. Pamoja
na fedha hizo, Serikali imepata amri ya kutaifisha nyumba 24 , magari 65, viwanja 9,
mashamba 2, mbao 6,894, Jahazi 1, XRF mashine mbili (2) za kupima
ubora wa madini.
Kadhalika, katika kusimamia
utawala wa sheria, washtakiwa (mahabusu) 2,812 wamefutiwa kesi na Mkurugenzi wa
Mashtaka (DPP) katika zoezi la ukaguzi wa magereza na kusikiliza changamoto za wafungwa na mahabusu.
(xx)
Kanda
Maalum za Kiuchumi:Eneo Maalumu la Uwekezaji Bagamoyo (SEZ): kumefanyika
uwekezaji wa viwanda 11 ambavyo ni Seif for Tobacco Trade Limited, Fujian
Hexingwang Industry Company Limited, Siparcoci International Limited, Hua Teng
Metalugical Company Limited, Wegmar Paking Limited, Jambo Food Products
Limited, Phiss Tannery Limited, Tube Limited, Ramky Tanzania Limited, Tanfroz
Limited, na Africa Dragon Enterprises Limited. Kati ya viwanda hivyo, viwanda
viwili (Africa Dragon Enterprises Limited na Phiss Tannery Limited)
vimekamilika na kuanza uzalishaji na kutoa ajira 120 za moja kwa moja na ujenzi
wa viwanda 9 unaendelea. Vile vile, andiko la uendelezaji na makisio ya gharama
za kuweka miundombinu wezeshi katika eneo lililolipiwa fidia limekamilika. Eneo Maalum la Uwekezaji Kigoma: shughuli
zilizotekelezwa ni kukamilika kwa upembuzi yakinifu na Mpango Kabambe wa
uendelezaji wa eneo (Master Plan) na ugawaji wa viwanja kwa ajili ya
wawekezaji; kazi nyingine ni kuendeleza miundombinu kwa kufungua barabara zenye
jumla ya km 28.46 na kuweka alama za mipaka 106; kupatikana kwa kampuni tatu
zitakazowekeza katika ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme wa jua (Next Gen
Solowazi Limited), ujenzi wa kiwanda cha kuchakata mazao ya nyuki
(Third Man Limited) na ujenzi wa
ghala na kiwanda cha kuchakata zao la michikichi (SGC Investment Limited);
(xxi)
Kuhamia
Dodoma: Watumishi 15,361 wa Wizara na Taasisi za Serikali wamehamia Makao
Makuu ya Serikali, Dodoma; ujenzi wa awali wa Ofisi za Serikali katika mji wa
Serikali, Mtumba umekamilika; maandalizi ya ujenzi wa majengo ya ofisi awamu ya
pili na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami (km 40) katika mji wa Serikali
Mtumba unaendelea;
(xxii)
Biashara
Ndogo: Serikali imesajili wajasiriamali wadogo milioni 1.55 ambapo jumla ya
shilingi bilioni 31.02 zimepatikana. Mikoa iliyokuwa na idadi kubwa ya
wajasiriamali waliosajiliwa ni pamoja na Dar es Salaam (asilimia 11.6), Arusha
(asilimia 6.4), Mwanza (asilimia 5.3) na Mbeya (asilimia 5.2); na
(xxiii)
Mafunzo
kwa Vitendo: yametolewa mafunzo ya uanagenzi (miezi sita) kwa vijana 5,875
katika vyuo 17 nchini; mafunzo ya vitendo kwa wahitimu wa elimu ya juu 2,297
mahali pa kazi katika fani mbalimbali ambapo kati ya hao wahitimu 890
wameajiriwa katika kampuni na taasisi mbalimbali na wengine kujiajiri;
kuwagharamia vijana 100 mafunzo kuhusu kilimo cha kisasa nchini Israeli; na
kutolewa mafunzo ya kurasimisha ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa
mafunzo kupitia watathmini kutoka vyuo vya ufundi visivyomilikiwa na VETA
(asilimia 65), watathmini kutoka vyuo vya VETA (asilimia 31) na watathmini
kutoka maeneo ya kazi hususan Viwandani (asilimia 3). katika kipindi cha Julai 2019 hadi Januari
2020 shilingi bilioni 10.5 zimetolewa kugharamia mafunzo hayo.
23.Mheshimiwa
Mwenyekiti, haya ni mafanikio ya kishindo yanayoonekana nchini kote na
yamepatikana chini ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Chama cha Mapinduzi . Hivyo,
napenda kumpongeza sana Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli, Waheshimiwa Wabunge wote
waliopigia kura ya NDIYO bajeti ya Serikali na Watanzania wote kwa kufanya kazi
kwa bidii na kulipa kodi kulikopelekea mafanikio haya ya kihistoria kwa kipindi
kifupi cha miaka minne tu. Asiye na mwana aeleke jiwe!
B. MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2020/21
24.Mheshimiwa
Mwenyekiti, Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa
Mwaka 2020/21 yanatekeleza vipaumbele vilivyoainishwa katika Mpango wa
Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21 ambavyo ni:
(i)
Viwanda
vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda: Miradi
itakayotekelezwa katika eneo hili inalenga kujenga viwanda vinavyotumia kwa wingi
malighafi zinazopatikana nchini zikiwemo za kilimo, madini na gesi asilia ili
kukuza mnyororo wa thamani. Miradi hiyo ni pamoja na Ujenzi wa Kiwanda cha
Kuchakata Gesi Asilia, Uanzishwaji na Uendelezaji wa Kanda Maalum za Kiuchumi
na Kongane za Viwanda, viwanda vya kuongeza thamani mazao ya kilimo, mifugo na
uvuvi, kuongeza thamani ya madini na usimamizi endelevu wa rasilimali za
misitu. Aidha, Mpango utaweka mkazo kuimarisha upatikanaji wa mbegu bora,
pembejeo na zana za kilimo na uvuvi, huduma za ugani na utafiti, uimarishaji wa
malambo na majosho, ujenzi wa maghala na upatikanaji wa masoko ya mazao na
mifugo ndani na nje ya nchi;
(ii)
Kufungamanisha
Ukuaji wa Uchumi na Maendeleo ya Watu: Miradi itakayotekelezwa katika eneo
hili inalenga kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, elimu na ujuzi na huduma
za maji safi na salama. Shughuli za miradi zitakazotekelezwa ni pamoja na
kugharamia utoaji wa elimumsingi bila ada, utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa
elimu ya juu, kuboresha huduma ya maji, elimu ya afya na usafi wa mazingira
shuleni, kuimarisha elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, ununuzi na
usambazaji wa dawa, ujenzi wa hospitali za wilaya na vituo vya afya, kupunguza
vifo vya akina mama vinavyotokana na uzazi, kusimamia na kuendeleza rasilimali
za maji nchini, kuimarisha huduma za ubora wa maabara za maji, kuboresha huduma
za maji mijini na vijijini na kuimarisha usimamizi wa mazingira na mabadiliko
ya tabianchi;
Vile vile, katika Awamu ya Tatu,
kipindi cha pili cha TASAF (2020-2023) itakayotekelezwa kwenye Halmashauri zote
185 na Wilaya zote 11 za Zanzibar itatumia kiasi cha shilingi trilioni
2.032. Asilimia 60 ya fedha hizo sawa na
shilingi trilioni 1.22 zitatumika kutekeleza miradi ya maendeleo takriban
30,000 kwenye vijiji na mitaa 16,596 Tanzania bara na shehia 388 Zanzibar.
Miradi hiyo itahusu sekta za afya
(sh. bilioni 121.736), elimu (sh. bilioni 365.209), maji (sh. bilioni 585.937),
barabara (sh. bilioni 49.668) na mazingira (sh. bilioni 96.416). Kipaumbele kitatolewa kwa watu wenye nguvu
wanaotoka kwenye kaya maskini ambapo ajira milioni 1.2 zitazalishwa na
kuwapatia walengwa ujuzi pamoja na stadi za kazi.
(iii) Uboreshaji wa Mazingira Wezeshi kwa Uendeshaji Biashara na
Uwekezaji: Miradi itakayotekelezwa inalenga kuendeleza ujenzi na
ukarabati wa miundombinu, ikijumuisha miundombinu ya nishati, usafirishaji
(reli, barabara, madaraja, viwanja vya ndege na bandari) na ununuzi na
ukarabati wa ndege, meli na vivuko pamoja na
uanzishwaji wa Kanda Maalumu za Kiuchumi. Miradi hiyo ni pamoja na Mradi
wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere - MW 2,115; Kuboresha Shirika la Ndege
Tanzania; Ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Standard Gauge; na kuendelea
na utekelezaji wa
Mkakati wa Mpango wa Kuboresha
Mazingira ya Biashara na Uwekezaji
Nchini; na
(iv) Kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa
Mpango: Eneo hili linalenga kuboresha ufuatiliaji, tathmini na utoaji
taarifa za utekelezaji wa Mpango, ikiwa ni pamoja na kuimarisha mifumo na
taasisi za utekelezaji wa Mpango; kuweka mfumo utakaowezesha upatikanaji wa
uhakika wa rasilimali fedha
kwa maandalizi, utekelezaji,
ufuatiliaji na tathmini ya miradi; na kuweka vigezo vya upimaji wa mafanikio ya
utekelezaji. Vile vile, Serikali itaendelea kuimarisha mapambano dhidi ya
rushwa na kuimarisha utawala bora katika usimamizi wa miradi ya maendeleo.
SEHEMU YA TATU
TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2019/20 NA
MAPENDEKEZO YA KIWANGO NA UKOMO WA BAJETI YA SERIKALI KWA
MWAKA 2020/21
A. TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2019/20
25.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2019/20, iliyoidhinishiwa ina
jumla ya shilingi trilioni 33.11, ikijumuisha shilingi trilioni 20.86 kwa ajili
ya matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 12.25 kwa ajili ya matumizi ya
maendeleo.
26.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, jumla ya mapato ya ndani yalitarajiwa kuwa shilingi trilioni
23.05. Kati ya mapato hayo, Serikali ililenga kukusanya mapato ya kodi ya jumla
ya shilingi trilioni 19.10, mapato yasiyo ya kodi ya jumla ya shilingi trilioni
3.18, na mapato kutoka vyanzo vya Halmashauri shilingi bilioni 765.5. Katika
kipindi cha Julai 2019 hadi Januari 2020, mapato ya ndani yalifikia kiasi cha
shilingi trilioni 11.87, sawa na asilimia 92.3 ya lengo la kukusanya shilingi
trilioni 12.86 katika kipindi hicho. Kati ya makusanyo hayo, mapato
yanayokusanywa kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), yalikuwa ni shilingi
trilioni 10.62, sawa na asilimia 96.9 ya makadirio ya shilingi trilioni 10.96
katika kipindi hicho.
27.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika kipindi cha Julai 2019 hadi Januari 2020, ufanisi wa
kukusanya mapato ya kodi umeimarika na kufikia asilimia 96.9 ya lengo
ikilinganishwa na ufanisi wa asilimia 88.6 katika kipindi cha Julai 2018 hadi
Januari 2019, sawa na ukuaji wa asilimia 16.6. Sababu za ongezeko la mapato
yaliyokusanywa na TRA ni pamoja na: kuongezeka kwa utoaji wa elimu ya
walipakodi; wananchi kuhamasika kulipa kodi kutokana na kuimarika kwa utoaji wa
huduma za kiuchumi na kijamii ikijumuisha maji, elimu, afya, miundombinu
wezeshi ya barabara na umeme. Sababu nyingine ni kuendelea kuongezeka kwa uwazi
katika usimamizi wa sheria za kodi, maboresho ya huduma kwa mlipakodi,
usimamizi wa matumizi ya mashine za kutolea risiti za kielektroniki hususan
kwenye sekta ya usafirishaji wa bidhaa mbalimbali, kuendelea kuziba mianya ya
ukwepaji kodi kwa kuwashirikisha kikamilifu na kuwaelimisha ipasavyo wale wote
ambao wamekuwa wakibainika kukwepa kodi.
28.
Mheshimiwa
Mwenyekiti,pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika ukusanyaji wa
mapato ya kodi, Serikali imeendelea
kuchukua hatua mbalimbali ili kuongeza makusanyo zaidi. Miongoni mwa hatua hizo
ni pamoja na: kuendelea kusimamia utekelezaji wa sheria, kanuni na taratibu za
kodi; kuhakikisha mfumo wa usimamizi wa mashine za kielektroniki za kutolea
risiti unatumika ipasavyo; kuendelea na utoaji wa elimu kwa mlipakodi na dhana
ya “Ukinunua Dai Risiti na Ukiuza Toa
Risiti”; kuendelea kuongeza kasi katika utatuzi wa pingamizi za kodi;
kuendelea kusimamia matumizi ya stempu za kodi za kielektroniki (ETS) katika
bidhaa zinazotozwa ushuru wa bidhaa, na kupitia nyaraka za walipakodi kwa lengo
la kufanya usuluhishi wa kodi walizolipa kwa kujikadiria wao wenyewe
ikilinganishwa kiasi halisi walichopaswa kulipa kwa mujibu wa Sheria.
29.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, mapato yasiyo ya kodi yaliyokusanywa na
Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala wa Serikali
yalikuwa shilingi bilioni 835.3. Aidha, Mamlaka za Serikali za Mitaa
zilikusanya shilingi bilioni 412.6, sawa na asilimia 90.2 ya makadirio ya
shilingi bilioni 457.4 kwa kipindi hicho.
30.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika kipindi cha Julai 2019 hadi Januari 2020, Washirika wa
Maendeleo walitoa jumla ya shilingi trilioni 1.58, sawa na asilimia 95.2 ya
makadirio ya shilingi trilioni 1.66. Kiasi hicho kimeongezeka kwa asilimia 46.6
ikilinganishwa na kiasi kilichopokelewa Julai 2018 hadi Januari 2019. Ongezeko
hilo linatokana na utekelezaji madhubuti wa Mwongozo wa Ushirikiano wa Maendeleo -
DCF pamoja na kuongezeka kwa ufanisi katika utekelezaji wa
miradi ya maendeleo.
31.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, hadi Januari 2020,
Serikali imefanikiwa kukopa shilingi trilioni 3.04 kutoka soko la ndani
sawa na asilimia 100.9 ya lengo la shilingi trilioni 3.01. Kati ya kiasi hicho,
shilingi trilioni 2.23 zilitumika kulipia mikopo ya ndani iliyoiva na shilingi
bilioni 806.8 zilitumika kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo. Mwenendo wa
upatikanaji wa fedha kutoka soko la ndani umeimarika kutokana na: Kuongezeka
kwa ukwasi kwenye benki za kibiashara; Serikali kuendelea kutoa matangazo ya
minada ya dhamana za Serikali katika Soko la Hisa la Dar es Salaam; na kutoa elimu kwa umma ili
kuhamasisha ushiriki katika kuwekeza kwenye Dhamana za Serikali.
32.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, hadi Januari 2020, kiasi cha shilingi trilioni 1.82 sawa na
dola za Marekani milioni 800 kimepatikana kutoka Benki ya Biashara na Maendeleo
(Trade and Development Bank-TDB) kiasi hicho ni asilimia 98.3 ya lengo la
kukopa shilingi trilioni 1.85 kutoka soko la nje kwa masharti ya kibiashara.
Aidha, kiasi kilichobaki cha dola za Marekani milioni 200 kinatarajiwa
kupatikana kutoka benki hiyo. Vile vile, Serikali imesaini mikataba minne (4)
ya mkopo wa dola za Marekani milioni 1,460.0 (takribani shilingi trilioni 3.33)
ambao unaratibiwa na Standard Chartered Bank
ambapo asilimia 68.0 ya mkopo huo ni kwa utaratibu wa udhamini kutoka
taasisi za udhamini wa mikopo (Export Credit Agency - ECA).
33.
Mheshimiwa
Mwenyekiti,kwa upande wa matumizi kwa mwaka 2019/20, Serikali imepanga
kutumia jumla ya shilingi trilioni 33.11 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo.
Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 20.86 kwa ajili ya matumizi ya kawaida
na shilingi trilioni 12.25 ni matumizi ya maendeleo. Katika kipindi cha Julai
2019 hadi Januari 2020, Serikali ilitoa ridhaa ya matumizi yenye jumla ya
shilingi trilioni 18.27 (ikijumuisha fedha za Washirika wa Maendeleo
zilizopelekwa moja kwa moja kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo kiasi cha
shilingi trilioni 1.20), sawa na asilimia 94.1 ya lengo la shilingi trilioni
19.41. Kati ya kiasi kilichotolewa, shilingi trilioni 12.05 ni kwa ajili ya
matumizi ya kawaida sawa na asilimia 97.6 ya lengo la shilingi trilioni 12.34
na shilingi trilioni 6.22 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo sawa na
asilimia 71.9 ya lengo la shilingi trilioni 8.67. Aidha, Serikali imetumia
shilingi trilioni 5.80 kulipia deni la Serikali lililotokana na mikopo
iliyotumika kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo. Baadhi ya miradi hiyo ni: mradi wa maji Arusha; mradi
wa maji Ruvu chini; mradi wa kufua umeme wa Kinyerezi, mradi wa njia ya
kusafirisha umeme wa msongo wa Kv 400 kutoka Singida – Arusha – Namanga;
upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Zanzibar; Mradi wa Kuboresha Huduma katika mji
wa Zanzibar; Mradi wa Serikali Mtandao Awamu ya Pili Zanzibar; ujenzi wa Jengo
la tatu la abiria katika kiwanja cha ndege cha Julius Nyerere; ukarabati wa
viwanja vya ndege vya Mtwara, Kigoma, Shinyanga, Sumbawanga na Mwanza;
ukarabati wa reli ya kati; na uboreshaji wa bandari ya Dar es Salaam.
34.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, utekelezaji wa bajeti katika kipindi kilichobakia unatarajiwa
kufikia malengo yaliyopangwa. Katika kufikia azma hiyo, Serikali itahakikisha
kuwa mfumo wa usimamizi wa Mashine za Kielektroniki za kutolea risiti unatumika
ipasavyo ili kuziba mianya ya uwezekano wa kugushi risiti; na kuendelea na
kampeni za kuhamasisha utumiaji sahihi wa mashine hizo na dhana ya “Ukinunua
dai risiti na ukiuza toa risiti”. Vile vile, Serikali itaendelea kutoa fedha
kwa Mafungu yote kwa kuwianisha mapato na matumizi na kipaumbele kitakuwa
katika mahitaji yasiyoepukika pamoja na miradi mikubwa ya kimkakati.
B. SERA ZA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2020/21
35.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika mwaka 2020/21, mapato ya Serikali yanatarajiwa
kuongezeka na hivyo kuweza kugharamia miradi mikubwa ya kimkakati. Katika
kufanikisha azma hii, sera za mapato kwa mwaka 2020/21 zitajielekeza kwenye
maeneo yafuatayo: kuendelea kuboresha mazingira ya uendeshaji biashara na
uwekezaji kwa kutekeleza Mpango Kazi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara nchini
ili kukuza biashara ndogo na za kati kwa ukuaji endelevu wa uchumi; kuboresha
mazingira ya ulipaji kodi kwa hiari pamoja na
upanuzi wa wigo wa kodi; kuimarisha usimamizi wa sheria za kodi ili
kutatua changamoto za ukwepaji kodi na kupunguza upotevu wa mapato; kuimarisha
usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani yakijumuisha mapato ya Mamlaka za
Serikali za Mitaa kwa kuhimiza matumizi sahihi ya mifumo ya TEHAMA; kuwianisha
na kupunguza tozo na ada mbalimbali ili kuboresha mazingira ya kufanya biashara
na uwekezaji; kuendelea kutekeleza Mwongozo wa Ushirikiano wa Maendeleo
Tanzania – DCF; na kuendelea kukopa kutoka katika vyanzo vyenye masharti nafuu
na mikopo inayotolewa kwa utaratibu wa udhamini kutoka taasisi za udhamini wa
mikopo.
36.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika mwaka 2020/21, Serikali itaendelea kusimamia nidhamu ya
matumizi ya fedha za umma kwa kuzingatia Sheria ya Bajeti Sura 439, Sheria ya
Fedha za Umma Sura 348, Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa Sura 290 na Sheria
ya Ununuzi wa Umma Sura 410. Lengo kuu ni kuziba mianya ya uvujaji wa fedha za
umma na kuelekeza kiasi kikubwa cha fedha kwenye miradi mikubwa ya kimkakati na
miradi mingine muhimu. Aidha, Serikali itaendelea kuhakiki, kulipa na kuzuia
ongezeko la uzalishaji wa madeni ya Serikali.
C. Kiwango na Ukomo wa Bajeti kwa Mwaka 2020/21
37.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, kwa kuzingatia sera za bajeti kwa mwaka 2020/21, jumla ya
shilingi trilioni 34.88 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika. Mapendekezo ya
kiwango na ukomo wa bajeti ya mwaka 2020/21 yamezingatia mahitaji halisi ya
ugharamiaji wa miradi mikubwa ya kimkakati, ulipaji wa mishahara na deni la
Serikali pamoja na utekelezaji wa vipaumbele vingine vya Taifa. Mapendekezo ya
kiwango na ukomo yanajumuisha: mapato ya ndani ya shilingi trilioni 24.07 sawa,
na asilimia 69.0 ya bajeti yote; mikopo ya ndani shilingi trilioni 4.90; mikopo
ya nje yenye masharti ya kibiashara shilingi trilioni 3.04 na misaada na mikopo
nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo shilingi trilioni 2.87, sawa na
asilimia 8.2 ya bajeti yote.
38.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika mwaka 2020/21, Serikali inapanga kutumia jumla ya
shilingi trilioni 34.88 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo. Kati ya fedha
hizo, shilingi trilioni 21.98 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na
shilingi trilioni 12.90 za matumizi ya maendeleo sawa na asilimia 37.0 ya
bajeti yote. Bajeti ya maendeleo inajumuisha shilingi trilioni 10.16 fedha za
ndani, sawa na asilimia 78.8 ya bajeti ya maendeleo na shilingi trilioni 2.74
fedha za nje. Matumizi haya yanajumuisha gharama za Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2020.
39.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, kwa kuzingatia maelezo hayo, kiwango na ukomo wa bajeti kwa mwaka 2020/21 ni kama ilivyo
katika Jedwali lifuatalo:
Mapendekezo ya Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka

HITIMISHO
40.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Mpango na Bajeti ya mwaka 2020/21 unazingatia azma ya Serikali
ya Awamu ya Tano chini na uongozi thabiti wa Mheshimwa Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ya kujenga uchumi wa viwanda
na kuboresha ustawi wa jamii. Aidha,
bajeti ya mwaka 2020/21 ni ya mwisho katika utekelezajiwa Ilani ya CCM ya mwaka
2015. Hivyo, bajeti hii itaendelea na utekelezaji wa maeneo makuu manne
yaliyoainishwa katika Ilani ambayo ni: Kuondoa umaskini; kupunguza tatizo la
ukosefu wa ajira kwa vijana; kuendeleza vita dhidi ya rushwa na ubadhirifu wa
mali za umma; na kuendelea kudumisha amani, ulinzi na usalama wa maisha ya
wananchi na mali zao.
41.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, ili kufikia malengo hayo, Serikali itaendelea kuongeza na
kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kugharamia shughuli za Serikali
ikiwemo utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati na uboreshaji wa huduma za
kijamii kwa lengo la kuleta maendeleo ya haraka. Aidha, Serikali itaendelea kusimamia nidhamu katika matumizi
ya fedha za umma na kufanya ufuatiliaji na tathmini ya matumizi hususan katika
miradi ya maendeleo. Lengo kuu ni kupata thamani halisi ya fedha katika
utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
42.
Mheshimiwa
Mwenyekiti,kama mnavyofahamu, mwezi Oktoba mwaka huu tutafanya Uchaguzi
Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani. Kwa upande wa Serikali, tumejipanga
kikamilifu katika maandalizi ikijumuisha mahitaji ya kibajeti kwa ajili ya
kufanikisha uchaguzi huo. Napenda kuchukua nafasi hii kuwasihi Watanzania wote
washiriki uchanguzi huu muhimuna wazingatie umuhimu wa kuendelea kudumisha
amani ya nchi yetu. Kila anayehusika atekeleze wajibu wake kulingana na nafasi
yake tukianzia kwa viongozi wa madhehebu ya dini, wagombea wa nafasi
mbalimbali, wapiga kura, Tume ya Taifa ya Uchaguzi, vyombo vya ulinzi na
usalama, wasimamizi wa uchaguzi, vyombo vya habari na hata waangalizi wa
kimataifa watakaokuwepo nchini wakati huo. Napenda kuwahakikishia Watanzania na
jumuiya ya kimataifa kuwa uchaguzi utazingatia haki na utafanyika kwa usalama,
amani na utulivu wa hali ya juu.
43.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
No comments:
Post a Comment