Habari za Punde

Mradi Umeme wa Jua Umeweza Kubadilisha Maisha ya Wananchi wa kijiji Mpale

AFISA Msimamizi wa mradi wa nishati ya umeme wa jua katika kijiji cha Mpale kata ya Mpale, Erica Jackson akizungumza na waandishi wa habari ambao wamefika katika kijiji hicho kujuwa maendeleo ya mradi huo.
BAADHI ya vigae vya umeme wa sola vikiwa vimewekwa katika mradi wa umeme wa jua wa 48 KW, ambao unatoa huduma kwa wananchi 250 wa kijiji cha Mpale kata ya Mpale tarafa ya bongo wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga, ambao unamilikiwana kampuni ya ENSOL.(PICHA NA ABDI SULEIMAN.)
NA ABDI SULEIMAN.
UWEPO wa nishati ya Umeme wa Jua kutoka kampuni ya Ensol, katika kijiji cha Mpale kata ya Mpale, tarafa ya Bongo Wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga, umeweza kubadilisha maisha ya wananchi wa kijiji hicho kwenye shuhuli za kiuchumi.
Wananchi wa kijiji hicho walikosa huduma ya Umeme huo, kwa miaka 45 tokea kuasisi kwa kijiji chao mwaka 1972, ambapo wameweza kunufaika nao mwaka 2017 baada ya kampuni ya Ensol kuwekeza mradi wa Bilioni 1 wa nishati ya jua.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi baadhi ya wafanyabiashara, ambao wanatumia nishati ya umeme wa jua, katika shuhuli zao mbali mbali kijijini Mpale, wamesema umeme huo umeweza kubadilisha maisha yao ya kiuchumi.
Walisema hapo mwanzo maduka walikuwa wakifunga saa 12 za jioni, lakini sasa wanafika saa nne usiku bado maduka yako wazi, kutokana na kuwepo kwa umeme wa uhakika kijijini kwao.
Mahunge Mussa Mkande ambaye ni mfanyabiashara wa Duka, alisema matumizi ya umeme kijijini kwao umeweza kuongeza kipato kwa wafanyabiashara, tafauti na walipokuwa wakifanya biashara kwa kutumia taa za vibatari.
“Huu umeme sasa ni wa uhakika na mzuri haukatiki mara kwa mara kama umeme wa REA, umeweza hata kupandisha bishara baada ya kuweka friji dukani kwake”alisema.
Alisema kuwepo kwa friji dukani kwake, kumepelekea mapato kuongezeka kwa siku anauza kati ya elfu 70,000/=hadi 80,000/=, jambo ambalo tafauti na kabalaya kuwepo kwa umeme akiuza shilingi elfu 50,000/= kwa siku.
Aidha Mahunge alisema umeme huo umemfanya kuweka banda la kuonyesha TV kwa wananchi, ambapo kiingilio ni shilingi 300 hadi 500 kwa baadhi ya michezo, huku mpira kwa mtu ni shilingi 1000 kwa mechi moja.
Hata hivyo alisema bei ya huduma ya umeme huo kwa wananchi bado iko juu, kwani kifurushi cha mwezi ni shilingi elfu 11000, wananunua tafauti na umeme wa REA ambao unauzwa kwa uniti.
Mahungo alishauri kampuni ya Ensol kuzirekebisha mita zao kuwa na mita za luku, ili kuondosha tafauti zilizopo baina ya umeme wa Ensol na umeme wa REA ambao unauzwa kwa uniti.
Mohamed Hashim mlale mmiliki wa mtambo wa kujazia upepo katika kijiji cha Mpale, alisema kuwepo kwa umeme huo umeweza kutoa ajira kwa vijana kijijini hapo, kwani vijana wengi wameweza kuingia katika biashara mbali mbali ikiwemo bodaboda.
Alisema baada ya kuja kwa umeme huo, alilazimika kuweka mtambo wa kujazia upepo ili kuwaondoshea usumbufu waendasha bodaboda kijijini hapo, kufuata huduma hiyo masafa ya mbali na wengine kufika mjini, ambapo kwa siku hukusanya kati ya elfu 15,000 hadi 20,000/=.
“Kuwepo kwa mtambo huu nimeweza kuajiri hata vijana wawili kijijini hapa, kwa shuhuli za kujaza upepo pikipiki na baadhi ya magari, pia napata cha kuwalipa vijana hawa kwa siku”alisema.
Philips John Yohana kijana aliekeza katika utoaji wa huduma za saluni, alisema baada ya kuja kwa umeme huo alilazimika kuanzisha saluni, kwa ajili ya kujikwamua na hali ngumu za maisha.
Alisema kazi yake imeweza kumpatia kipato cha kujikimu kimaisha, kwani kwa siku hukusanya kati ya elfu 15000 hadi 20,000/=, jambo ambalo limemuepusha na ukaaji wa vijiweni.
Afisa msimamizi wa mradi wa Ensol kijiji cha Mapale, Erica Jackson alisema umeme huo ulianza 2017 kijijini hapo, ambapo walianza na wananchi 61 kuwaunganishia huduma hiyo, huku malengo yao ni kuwaunganisha wananchi 250 tayari yametimia.
Alisema kuwepo kwa umeme huo umeweza hata kuwanufaisha wanawake kwa kuanzisha biashara zao ndogogo, ikiwemo maandazi na chapiati.
Kwa upande wake Mtendaji wa kata ya Maple Mwanahija Abdalla Nurdin, alishukuru kampuni ya Ensol kuanzisha mradi katika kata ya mpale kijiji cha mpale, ambapo maendeleo mbali mbali yameweza kupatikana kijijini hapo.
Alisema umeme huo umepelekea wananchi kuanzisha biashara mbali mbali, kwa kujiajiri wenyewe ikiwemo kutoka huduma za matibabu hadi muda wa usiku.
Mwenyekiti wa Serikali ya  kijiji cha Mpale, Abdal Mohamed Mdowe alisema kuwepo kwa umeme huo umeweza kuwatoa katika giza la kusubiria umeme wa REA, kitu ambacho umekuwa ni mkombozi mkubwa kwa wananchi wa Mpale.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.