Na Zamaradi Kawawa, Maelezo, Dar Es
Salaam
18.04.2020
Serikali
imehamisha wagonjwa wote waliokuwa wakipata huduma za afya katika hospitali ya Rufaa
ya Mkoa wa Dar es Salaam, Amana iliyopo Manispaa ya Ilala, ili kuanza
kutekeleza jukumu la kutumia hospitali hiyo kutoa huduma za afya kwa wagonjwa
wa Corona (COVID – 19).
Akizungumza na
Watumishi wa hospitali hiyo mara baada ya kutembelea majengo yatakayotumika
kuwalaza wagonjwa wa Corona (COVID-19), Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Zainab Chaula amesema wagonjwa waliokuwa wanapata huduma
katika hospitali hiyo wamehamishiwa katika hospitali nyingine za Serikali jijini
Dar es Salaam.
Amesema
Serikali imetoa kiasi cha Shilingi Milioni Mia Mbili (200m/-=) kwa ajili ya
ukarabati mdogo wa baadhi ya majengo ya hospitali hiyo.
Dkt. Chaula amewataka
watumishi wa sekta ya afya kukumbuka kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo kwa
kuvaa vifaa vya kujikinga na maambukizi wakati wa kuwahudumia wagonjwa wa
COVID-19 hospitalini hapo.
Amewakumbusha
watumishi wa sekta ya afya nchini kutimiza wajibu wao katika kipindi hiki cha
janga la ugonjwa wa Corona huku wakizingatia kiapo cha utii wa majukumu yao ya
utoaji huduma za afya kwa wagonjwa.
Amesema Serikali
ipo tayari kuwezesha huduma za afya kutolewa kikamilifu kwa wagonjwa wa Corona
nchini na kuwa Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imefanya
juhudi mbali mbali za kupunguza maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo nchini
zilizosababisha kuwa na wagonjwa wachache hadi sasa ukilinganisha na nchi
nyingine.
Akizungumzia
uamuzi huo wa Serikali Ijumaa wiki hii,
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bi Ummy Mwalimu
alisema Serikali
imeelekeza Hospitali ya Taifa Muhimbili kuacha kupokea wagonjwa wenye dalili za virusi vya Corona (COVID-19) ili
iweze kutekeleza majukumu yake ya kutoa huduma za kibingwa na huduma bobezi kwa
wagonjwa wa magonjwa mengine nchini.
Alisema, badala yake Serikali imeamua kutumia Hospitali ya
Amana kama kituo maalum cha matibabu ya ugonjwa wa COVID-19. Wananchi wa mkoa
wa Dar es Salaam wanaohitaji kupata huduma za matibabu ya magonjwa mengine
katika Hospitali ya Amana wanatakiwa kutumia hospitali nyingine zilizopo mkoani
humo.
No comments:
Post a Comment