Habari za Punde

MAKALA- MIEZI ISHIRINI KWA WANAHABARI WASIO NA SIFA KUPIGWA STOP!


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe akiwasilisha bajeti ya Wizara hiyo Bungeni jijini Dodoma ambapo imetengewa kiasi cha sh. bilioni zaidi ya 40.1 kwa mwaka huu wa fedha 2020/2021.

Na Eleuteri Mangi, WHUSM-Dodoma
Ni miaka minne tangu Sheria ya Huduma za Habari Namba 12 ya Mwaka 2016 imepitishwa nchini na Bunge mnamo Novemba 5, 2016 na kusainiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli Novemba 16 mwaka huo huo.

Miongoni mwa matakwa ya sheria hiyo ambayo yameainishwa kuisimamia na kuiboresha tasnia ya habari na kuifanya kuwa taaluma kamili ili iheshimike kama taaluma nyingine ni hatua kuingiza kipengele cha kiwango cha elimu, hatua itakayowasidia kuongeza weledi katika utendaji kazi wanataaluma hao.

Kifungu cha 67(b) cha Sheria ya Huduma za Habari Namba 12 ya Mwaka 2016 kikisomwa kwa pamoja na Kanuni ya 17(20(a) ya Kanuni za Sheria ya Huduma za Habari, 2017 vinawataka wanahabari wote kujiendeleza na kuwa na sifa ya kitaaluma ya angalau Stashahada (Diploma) ndani ya kipindi cha miaka mitano baada ya kuanza kwa Sheria hiyo iliyoanza kutumika rasmi nchini Desemba 31, 2016.

Akiwasilisha Bungeni Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka 2020/2021 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amesema kuwa kipindi cha miaka mitano cha mpito kinakwisha mwezi Desemba 2021 ni vema wanataaluma hao wajiendeleze wapate sifa za kitaaluma kwa kiwango kilichoainishwa kisheria ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria hiyo.

“Natumia nafasi hii kuwapongeza wengi walioitikia wito na ambao kwa sasa wanajiendeleza au wameshamaliza masomo yao, natoa wito kwa waandishi wa habari nchini ambao bado hawajajiendeleza kielimu kukidhi matakwa ya sheria wafanye hivyo ili waweze kuendelea na kazi ya uandishi wa habari baada ya muda huu wa mpito kuisha” alisisitiza Dkt. Mwakyembe.

Hakika imebaki miezi 20 kwa wanataaluma ambao bado hawajaanza kujiendeleza kielimu, sasa ni muda muafaka kufanya hivyo ili kupata sifa za kuwa mwanataaluma kamili wa habari.

Sheria ya Huduma za Habari imekuja wakati muafaka ambapo imekuwa ni hatua muhimu kwa tasnia ya habari kwa kuihamisha taaluma ya hiyo kutoka fani ambayo mtu yeyote anaweza kujinasibu nayo hadi kuwa taaluma kamili yenye sifa mahsusi, maadili yanayojulikana pamoja na vyombo vya kusaidia kusimamia utekelezaji wake ikiwemo Bodi ya Ithibati na Baraza Huru la Vyombo vya Habari.

Idara ya Habari (MAELEZO), inasimamia na kuratibu shughuli za Serikali upande wa habari. Katika kutekeleza majukumu yake, Idara hiyo imegawanyika katika sehemu tatu ambazo ni Sehemu ya Ukusanyaji na Usambazaji wa Habari, Usajili wa Magazeti na Mawasiliano Serikalini ambapo kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari Namba 12 ya Mwaka 2016 kifungu cha 4 (1) Mkurugenzi wa Idara ya Habari ndiye msimamizi mkuu wa Idara hiyo.

Mkurugenzi Msaidizi wa Idara hiyo, sehemu ya Usajili wa Magazeti, Patrick Kipangula   amebainisha kuwa utekelezaji wa sheria hiyo unaenda vizuri hatua inayoonesha kuwa kuna mwitikio mkubwa wa waandishi wa habari kujiendeleza kielimu.

Aidha, amesema kuwa sehemu hiyo ya Idara ndiyo yenye mamlaka ya kutoa vitambulisho vya waandishi wa habari (Press Card) ambapo kuanzia mwezi Januari hadi Aprili 2020 vitambulisho vya wanahabari 638 vimetolewa na kati yao takribani asilimia 80 ya vitambulisho hivyo vya waaandishi wana sifa na wana kiwango cha elimu kinachotakiwa kwa mujibu wa sheria yaani Stashahada katika tasnia ya habari.

Aidha, Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA-TAN) ikiwa mdau muhimu wa tasnia ya habari nchini ambayo miongoni mwa malengo yake makuu ni kukuza, kuboresha na kuleta utofauti wa utendaji kazi wa vyombo vya habari vikiongozwa na weledi katika utendaji kazi wao kwa kuzingatia taaluma ya habari ikiwemo kiwango cha elimu.

Akizungumzia hotuba ya Waziri mwenye dhamana ya habari aliyoitoa Bungeni jijini Dodoma hivi karibuni, Mwenyekiti wa MISA-TAN nchini Salome Kitomari amesema kuwa tangu sheria hiyo imepitishwa na kufanya kazi nchini, taasisi hiyo imekuwa ikitoa mafunzo na kuwasisitiza waandishi wa habari kujiendeleza kielimu ambapo kwa upande wao wamekuwa wakitoa mafunzo mbalimbali kuhusu sheria zinazosimamia taaluma hiyo.

“Wapo ambao walitusikia na kufuata matakwa hayo ya kisheria na sasa wamemaliza vyuo vikuu na wengine wamemaliza diploma, lakini kuna ambao wapo katika hatua mbalimbali ikiwemo kumalizia masomo yao katika vyuo walivyojiunga kusoma” alisema Kitomari.

Aidha, Mwenyekiti huyo ametoa wito kwa waandishi wa habari nchini kutimiza takwa hilo la kisheria kwani imeshakuwa sheria tayari na haina mbadala, hivyo lazima kila mwandishi wa habari ambaye atapenda kufanya kazi hiyo awe na elimu angalau kiwango cha Stashahada katika tasnia ya habari.

Zaidi ya hayo, amesema kuwa muda ulioainishwa kwa maana ya muda wa mpito uliotolewa kisheria unakaribia kuisha kwani muda huo ulishatolewa tangu Desemba 31, 2016 na ukomo wake ni Desemba 31, 2021.

“Napenda kuwaambia waandishi wa habari wenzangu, kama kweli unaipenda kazi yako ya uandishi wa habari, nenda darasani ukasome ule wakati wa ujanja ujanja na kufanya mambo mbalimbali yaende umekwisha, sasa hivi ni wakati wa kuhakikisha una cheti chako kwa sababu itafikia wakati kama huna cheti hata ‘Press Card’ hutapata” amesisitiza Kitomari.

Kwa upande wa usajili wa wanachama wa MISA-TAN, Mwenyekiti huyo amesema kuwa taasisi hiyo ina wanachama wa zamani ambao wamekuwa wakihimiza kila mara kujiendeleza kielimu na ikitokea kunapata na kupokea wanachama wapya ambao bado wanaendelea na masomo wanawasisitiza kumalizia masomo yao ili waweze kuwa na sifa stahiki zilizoainishwa kisheria.

Kwa mujibu wa Kanuni ya 17 inayofafanua Sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya 2016 imebainisha kuwa mtu mwenye sifa ya kupata ithibati ya kuwa mwandishi wa habari ni pamoja na wahariri wa habari, waandishi wa habari, watangazaji, waandishi wa habari wa kujitegemea, wapiga picha, watayarishaji wa habari na watangazaji wa redio na runinga wanaofanya kazi katika vyumba vya habari, watu waliofanya kazi ya kutukuka katika tasnia ya habari pamoja na mtu mwenye shahada yoyote ambaye lazima awe na stashahada ya tasnia ya habari.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.