Habari za Punde

CORONA ilivyoathiri wanawake, kiuchumi, kijamii na Kisiasa


Na Halima Mohammed
MAISHA ni kutafuta, hivyo inabidi kukubaliana na hali yoyote ile ili uweze kufanikiwa katika jambo lako.Kila siku watu huamka asubuhi na kutoka majumbani kwao kwa ajili ya kutafuta riziki ambapo katika kutafuta huko hukumbana na changamoto nyingi ambazo wakati mwengine inatupasa tukubaliane nazo ilimradi tu
mkono uwende kinywani.

Ninapo tamka haya natoa mwanga kwa wale ambao wamekuwa wakiona kila kitu kigumu na kujikuta wakikaa vjiweni na kufanya mambo yasiyokuwa na maana.

Kutokana na hali ya maisha ilivyo na kila mwanadamu ambae yupo hai na anahitaji mambo mbali mbali ya muhimu ikiwemo chakula hulazimika kuhangaika kwa kujishughulisha ili aweze kupata kipato ambacho kitamsababishia kupata riziki.

Kila inapofika asubuhi mwenye kuajiriwa hufika alipoajiriwa na wale ambao hawajaajiriwa kujishughulisha kwa kutafuta biashara mbali mbali ili aweze kuingiza kipato

Takriban miezi sita sasa dunia imekumbwa na  janga kubwa la maradhi ya Corona ambayo yametowa athari kubwa kiuchumi, Kijamii na Kisiasa.

KIUCHUMI
Mambo mbali mbali ikiwemo biashara katika dunia imeshuka na kusababisha taasisi,maofisi na hata maeneo ya burudani na michezo kufungiwa kutokana na janga hilo.

Zanzibar nayo ni miongoni mwa nchi ambazo janga hili imeikumba na kuonekana watu wake kutetereka katika kazi zao hasa wakiwemo wanawake ambao ni wajasiriamali.

Katika Makala haya mwandishi alipata fursa ya kuzungumza na baadhi ya wajasiriamali wanawake wanaopika vyakula ‘Mama Ntilie’, wanajamii na wanasiasa ambao kwa hakika walieleza namna Corona inavyowapa
changamoto.

Wengi wa wajasiriamali hao walieleza jinsi maradhi hayo yalivyosababisha kuangusha uchumi na kushuka kwa kipato chao ambacho kimepelekea kuwa na hali ngumu ya kimaisha.
Fatma Mohammed ambae anafanya kazi zake hizo darajani anasema kuwa kabla ya hapo mazingira yalikuwa sio magumu sana lakini baada ya kuingia Corona kipato kimekuwa kigumu.

Anasema kuwa wakati huu mazingira ya kufanyia kazi yamekuwa magumu kwa sababu ni lazima uende sambamba na vielelezo vya maradhi hayo.

Hivyo anasema kuwa ile pesa ambayo ambayo walikuwa wakiipata kama faida inabidi waitumie kwa kununulia vifaa ikiwemo vifungashio vya vyakula ambapo hapo awali ilikuwa mteja alikuwa akichukuwa chakula
katika kifungashio inabidi umkate pesa.

“Tofauti na sasa kwa vile mkusanyiko umekatazwa inatupasa sisi ndio tununuwe vifungashio hivyo kwani kama utamlazimisha mteja utamkosa’,anasema.

Anasema kuwa katika kazi yao kuna mahitaji mengi yanahitajika na mengine yameongezeka katika kipindi hichi cha corona jambo ambalo linawafanya wafanye biashara yao katika mazingira magumu.

“Kipato si kama kilikuwa kikubwa  lakini ilikuwa afadhali na bora tunaona ni bora upate faida ndogo kuliko kukosa kabisa”, anasema.

Hata hivyo mama huyo aliwataka wanawake wenzake wasikate tamaa kwani suala hilo la maradhi limetokea na inawapasa waendelee na juhudi zao za kufanya kazi kwa kutambuwa kuwa wao wana majukumu.

“Ni  lazima wanawake tupige kazi kwani tuna majukumu ya kifamilia pia yanatutegemea sisi na unaposema usitoke kwa ajili ya corona mwisho wa siku ndo hali inazidi kuwa ngumu zaidi”, alisema.

Fatma anasema kuwa katika kipindi hichi cha Ramadhan ameacha kazi yake ya mama ntilie na badala yake anajishughulisha na kazi ya biashara ya kukopesha nguo ingawa nayo alisema kuwa nayo inakuwa ngumu kutokana na hali iliyopo ya Corona.

KIJAMII
Kuhusu sherehe za harusi, misiba, kutembeleana, kukagua wagonjwa hospitalini na shughuli nyengine za kijamii wanawake hao wanasema kuwa wameathirika kiasi lakini wakati mwengine inawabidi wakubaliane na
hali halisi inavyotaka.

Nia Juma mkaazi wa Tomondo Uzi anamwambia mwandishi wa Makala haya kwamba harusi ni jambo la sherehe ambalo watu hukusanyika na kufurahi lakini kwa sasa inakuwa ni tofauti na vile walivyozoea kutokana na
kupangiwa idadi ya watu wa kuweza kuwaalika.

Anasema kuwa kuwa yeye ni miongoni mwa watu ambao waliathirika na hili baada ya kufanya harusi ya mdogo wake na kutakiwa watu ambao atawaalika wasizidi saba na waume ambao wanakuja kuoa nao idadi iwe
ndo hiyo hiyo.

“Kwa kweli ni maradhi ambayo mungu ametuletea lakini kiukweli yametuathiri maana sasa hivi hatuaminiani hata kidogo kila mtu yupo kwake na familia yake”, anasema.

Hata hivyo aliwataka wanawake na jamii kwa ujumla waendelee kufata maelekezo ya Serikali na wataalamu wa afya ili kujikinga na janga hili.

Madina Ali wa Fuoni anasema kuwa Corona haikuathiri tu wanawake bali hata watoto wameathirika kutokana na kutokwenda shule na badala yake kuzagaa mitaani na kucheza gololi.

“Kusema kweli hili jana ni hatari pamoja na kuwa Serikali imepiga marufuku mkusanyiko na kufunga shule lakini watoto wamekuwa wakaidi na unapopita unawakuta wamekusanyana wanacheza gololi hata ukiwakataza
wanaondoka sehemu moja kwenda nyengine”, anasema.

Anafahamisha kwamba kwa binafsi yake amekuwa akiwaambia kuhusu madhara ya mikusanyiko lakini huwa wanamjibu mikusanyiko hiyo imepigwa marufuku kwa mjini tu na sio huku vijijini.

Warda Nassor Omar wa Mwera anasema kuwa kitendo cha kufungwa shule kumewaathiri sana wazazi na hata watoto ambao wamekuwa hawasomi na unapomsomesha anakuwa hakusikilizi.

Anasema kuwa mwalimu ni tofauti na mzazi maana watoto wengine ukiwasomesha na wakikosea ukamfahamisha mara hukugeukia na kukuambia kuwa wewe ndio hujui.

Aidha anafahamisha kwamba Serikali kupitia Wizara ya Elimu wameanzisha vipindi vya redio na TV vya masomo kwa madarasa yote lakini hii kwa watoto wengine haiawasaidii kutokana na kuwa watoto hao wanashindwa
kufatilia .

Anasema kuwa wakati vipindi hivyo vinafanyika inakuwa wazazi wapo makazini na wengine kama kule vijijini wapo mshamba sasa na mtoto hata kama utamfungulia utamkuta kashabadilisha chanal na kuweka katuni.

Kwa hivyo anasema kuwa inakuwa ni ngumu kwa watoto kuweza kuwadhibiti kwa hilo na wengine hata hizo TV na redio hawana majumbani mwao.

Jengine ambalo anasema wameathirika kama wazazi ni kuongeza mtafaruku wa vurugu na utundu kwa watoto wao hasa wanapokuwa pamoja kwa muda mrefu.

“Tumezowea mtoto anaamka asubuhi anakwenda shule na mchana anakwenda madrasa lakini sasa hivi muda wote wapo nyuumbani utakuta kesi hazipungui kwa kila baada ya muda huyu kampiga huyu na yule kampiga
huyu, kwa kweli corona imeathiri sana shughuli za mwanamke katika utafutaji wake wa riziki na kuongeza kipato.
SIASA
Kwa pande wa siasa ingawa sio kipindi chake lakini wapo ambao wameathirika na hilo kutokana na kurudi nyuma katika juhudi zao za kupambana na kampeni zao za chini kwa chini baada ya kupigwa marufuku mikusanyiko.

Wanawake ambao tayari wameshaonesha nia ya kugombea lakini sasa hivi wanashindwa kuwafikia kuwakampeni wapiga kura wao kwa kuhofia maradhi haya.

Wanawake hao ambao wamekataa kutaja majina yao kwa kuhofia kukatwa majina yao muda utakapofika wanasema kuwa hii ni kazi ya mungu lakini kiukweli imewaathiri kisiasa.

Wanasema kuwa wamepata mafunzo mbali mbali kutoka kwa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania TAMWA ZANZIBAR chini ya Ufadhili wa UN WOMEN, lakini sasa hivi wanshindwa kuyafanyia kazi kuwapa wanawake wenzao ambao bado wanasuasua kuonesha nia zao za kugombea uongozi katika uchaguzi Mkuu ujao.

Bahati Issa mkaazi wa Kikungwi Wilaya ya Kati Unguja anaeleza kuwa hapo awali alikuwa na nafasi kubwa kuwapitia wanawake wenzake kuwashajiisha kujitokeza kuwania nafasi mbali mbali za uongozi lakini
sasa hivi amesita.

Anasema kuwa pamoja na kuwa yeye sio mgombea lakini amekuwa mstari wa mbele katika kuwahamasisha wanawake juu ya kujitokeza kugombea nafasi za uongozi ili waweze kuingia katika vyombo vya maamuzi na kuwatetea wanawake wenzake.

Nae Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Nchini Tanzania (TAMWA),Zanzibar,  Dkt Mzuri Issa alisema kwamba TAMWA Zanzibar inahuzunika kwa kuzuka kwa ugonjwa huo unaosababishwa na
virusi vy Corona ambapo imeleta athari kwa maisha ya watu  katika kipindi hichi cha mwaka huu wa uchuguzi nchini.

Alisema TAMWA  kwa kushirikiana na wadau mbambali kwa mwaka huu tayari wameshaandaa program maalum ya kuwaunga mkono wanawake kushika nafasi  za uongozi katika uchaguzi.

“Mripuko wa maradhi ya Corona umeibuka wakati tukiwa katika hatua ya awali ya kuhamasisha jamii za Unguja na Pemba ili kuwakubali wanawake kama wagombea halali katika siasa za ushindani kama wanaume”alisema
Dkt.  Issa.

Sambamba na hayo Mkurugenzi huyo  alitoa wito kwa jamii hasa Wanawake, Wanume, Viongozi wa Dini na wanachama wa vyama vya Siasa kuwaunga mkono wanawake hao ili kufikia matarajio yao ya kisiaa katika hali
yoyote inayowezekana hasa kwa wakati huu wanawanchi wanapohimizwa kuepuka mikusanyiko.

Aidha alisema kuwa mwanamke ni muhimu katika kila nyanja ya maendeleo, na kuwataka waendelee na shughuli za kujikomboa kiuchumi, kwa kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalam wa afya  ikiwemo kuepuka  mikusanyiko isio ya lazima.

“kujitenga na watu kwa masafa ya mita mbili, kuosha mikono kila inapobidi, kujihifadhi wakati wa kukohoa na kwenda chafya, na ukiona dalili za covid -19 wasiliana na mamlaka husika”, alisisitiza Mkurugenzi huyo.

Hivyo aliwataka wanawake na jamii kwa ujumla kujikinga na  kuuwakinga na wengine na maradhi hayo ambayo kwa hakika corona inaepukika lakini pia inauwa.

Jumla ya wanajamii 4,069 kutoka wadi 55 Unguja na Pemba wamefikiwa na program hiyo yakuwashajihisha wanawake kushika nafasi za uongozi katika kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.