Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe.
Dkt. Harrison Mwakyembe (wa tatu Kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mabondia
na Viongozi wa Ngumi walipotembelea Bunge Aprili 2019 Jijini Dodoma. Wa tano
kulia ni Naibu Spika
Mhe. Dkt Tulia Ackson wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
NGUMI
ni miongoni mwa michezo ambayo imeitangaza na kuipa heshima Tanzania duniani kutokana
na mabondia wake kuonyesha uwezo mkubwa na kushinda katika mapambano mbalimbali
ya Kimataifa. Kutokana na sababu mbalimbali za kiutendaji wa viongozi wa mchezo
huu, ulipoteza sifa yake Kitaifa na Kimataifa na kudidimiza maendeleo yake hapa
nchini. Eleuteri Mangi wa Wizara ya
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dodoma anaelezea jinsi mchezo huo
unavyorejesha heshima iliyokuwa nayo Tanzania Kitaifa na Kimataifa katika miaka
ya 1970.
Mchezo wa ngumi ni
miongoni mwa michezo inayofahamika na kupendwa sana na watu wengi duniani. Kama
ilivyo kwa michezo mingine kama vile mpira wa miguu, mchezo huu umekuwa ni
chanzo cha ajira na hivyo kujipatia umaarufu mkubwa ambapo vijana wengi wanajiunga
kwa lengo la kujipatia kipato. Ndiyo kusema, michezo ni kiwanda kikubwa
kinachobeba ajira lukuki kwa vijana na wataalam wa michezo mbalimbali nchini na
duniani kote.
Mchezo wa ngumi nchini
Tanzania ulianza kufahamika katika miaka ya 1950 ambapo miaka ya 1970 mabondia
wake walianza kufahamika katika mashindando mbalimbali ya Kimataifa. Medali ya
kwanza ya Kimataifa ililetwa na Titus Simba mwaka 1974 katika michezo ya Jumuiya
ya Madola iliyofanyika nchini Uingereza na mwaka 1998 bondia mwingine Michael
Yombayomba aliiletea Tanzania medali nyingine katika mashindano hayo ya Jumuiya
ya Madola yaliyofanyika nchini Malasia.
Huo ndio ulikuwa mwanzo
wa Tanzania kufahamika Kimataifa katika medani ya mchezo wa ngumi ambapo
wanamasumbwi wengine kama vile akina Makoye Isangula, Stanrey Mabesi, Benjamin
Mwangata, Shaaban Matumla na wengine walitamba na kuiletea Tanzania medali
mbalimbali. Hata hivyo, kuzuka kwa vyama vingi vya ngumi nchini kumekuwa chanzo
cha kushuka kwa mchezo huo katika kipindi cha muongo mmoja uliopita kutokana na
viongozi wake kutoelewana kiutendaji kutokana na sababu mbalimbali.
Kwa kulitambua hili, Serikali
ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
Johh Pombe Magufuli kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
imeanza kuchukua hatua kadhaa kuweza kurejesha heshima ya Tanzania Kitaifa na
Kimataifa kupitia mchezo wa ngumi.
Kuundwa kwa Kamisheni
ya Kusimamia Ngumi za Kulipwa nchini (TPBRC) ni mwanzo mpya unaodhihirisha nia
ya dhati ya Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe (Mb). Utekelezaji wa agizo la kuanzisha TPBRC
nchini umeanza kuleta manufaa kutokana na shabaha ya Ilani ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015-2020 katika kukuza michezo.
Ilani hiyo katika
ukurasa wake wa 218 Ibara ya 161 imetamka “Katika kipindi cha miaka mitano ya
utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2015-2020 imebainisha CCM itaielekeza Serikali
kuimarisha sekta ya michezo ili kuinua kiwango cha michezo
nchini ikiwa ni pamoja kuifanya sekta ya michezo kutoa fursa
za ajira hususani kwa vijana”.
Kama michezo mingine, mchezo
wa ngumi za kulipwa unaendeshwa kwa mujibu wa Sheria ya Baraza la Michezo la
Taifa Na. 12 ya mwaka 1967 na marekebisho yake Na. 6 ya mwaka 1971 pamoja na
kanuni za Usajili Na. 442 za mwaka1999.
Sheria hiyo iliyofanyiwa
marekebisho ya Sheria Na. 3 kifungu cha 18 ya mwaka 2018 kwa mamlaka aliyonayo
Waziri mwenye dhamana ya michezo nchini yameongeza wigo na kutambua michezo ya
ridhaa na michezo mingine ambayo yamepelekea kuundwa kwa Kamisheni ya Ngumi za
kulipwa nchini.
Chombo hicho kimeleta
mafanikio katika mchezo wa ngumi za kulipwa nchini na umekuwa na mchango mkubwa
katika kuajiri vijana ambao wamekuwa na mafanikio kwa mtu mmoja mmoja akiwa
mchezaji na taifa kwa ujumla.
Katika kuthamini michezo
nchini ikiwemo masumbwi, Rais Dkt. Magufuli ni mpenda michezo amekuwa mstari wa
mbele katika kutambua na kuwatuza wanamichezo wanapofanya vizuri katika
mashindano mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Mapema mwezi Machi
mwaka 2019, Rais alidhihirisha uzalendo wake kwa michezo nchini kwa kuwapa wachezaji,
viongozi wao na bondia Hassan Mwakinyo zawadi ya viwanja vya kujengea nyumba mkoani
Dodoma kama ishara ya kuonyesha alivyofurahishwa kwa juhudi za wachezaji na
viongozi wao kuipa Tanzania ushindi.
“Nimeamua niwape zawadi kidogo kwa niaba ya
watanzania, nitawapatia viwanja vya kujenga nyumba wachezaji wote wa Taifa
Stars na viongozi wao, bondia Hassan Mwakinyo pamoja na mwalimu wako, zawadi
hiyo pia kwa Peter Tino na Leodegar Tenga” alisema Rais Dkt. Magufuli.
Bondia Hassan Mwakinyo anapongezwa
kwa kazi nzuri anayoendelea kuliwakilisha taifa vema katika mashindano
mbalimbali duniani ikiwemo kumtwanga Amel Tinampay raia wa Ufilipino kwa point
katika mchezo uliofanyika jijini Dar es Salaam mwezi Novemba, 2019.
Hakika mchezo wa ngumi
za kulipwa umekuwa mwanzo mpya wa mabondia nchini kufanya vizuri katika
mapambano waliyoshiriki. Bondia Abdallah
Paziwapazi alimchapa Zulipikaer
Maimaitiali raia wa China kwa Knock Out katika pambano
la WBO Asia
Pacific Super
Middle Title lililofanyika
nchini China mwezi Agosti, 2019 wakati Hamis Maya alimtwanga Piergiulia
Ruhe raia wa Ujerumani kwa Knock Out katika pambano la Global Boxing Council
Intercontinental Welter lililofanyika nchini Ujerumani mwezi Novemba, 2019.
Mabondia wengine
waliofanya vizuri na kuliletea Taifa sifa nzuri ni pamoja na Bondia Bruno
Melkiory Tarimo (Vifua Viwili) ambaye alimpiga Nathaniel May raia wa Australia
kwa point katika pambano la Boxing Federation International Super Feather Title
lililofanyika nchini Australia mwezi Desemba, 2019 na Bondia Salimu Jengo aliyemchapa
Suriya Tatakhun raia wa Thailand kwa KO katika pambano la Universal Boxing
Organization World Light Title lililofanyika Jijini Tanga mwezi Januari, 2020.
Akiwasilisha
Bajeti ya Wizara yake ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka
2020/2021 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt.
Harrison Mwakyembe amewapongeza wachezaji wa Kitanzania wanaozidi kuongezeka na
kufuzu vigezo vya kimataifa na kucheza
michezo ya kulipwa katika nchi
mbalimbali na kupeperusha vyema bendera ya Tanzania.
“Nawapongeza
wanamichezo wote nchini kwa kupeperusha vyema bendera ya nchi yetu katika
mashindano mbalimbali ya kimataifa na hivyo kuitangaza na kuiletea heshima
kubwa nchi yetu” alisema Dkt. Mwakyembe.
Waziri Mwakyembe
aliendelea kusema “Namshukuru sana Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kwa uongozi wake thabiti na hatua anazochukua kuimarisha michezo nchini.
Nampongeza Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kwa kuipa wizara yangu ushirikiano
mkubwa na msaada katika kuendeleza michezo nchini. Pia niwapongeze watanzania
kwa hamasa na uzalendo wanaouonesha kwa timu zetu”.
Kwa upande wake Promota
Shomari Kimbau ambaye ni mdau wa mchezo wa masumbwi ameipongeza Serikali kwa kwa
nia yake ya dhati ya kusaidia na kusimamia mchezo huo na kuamini usimamizi bora
wa mchezo huo nchini ni mwanzo mpya wa Mchezo wa Ngumi za Kulipwa.
“Lazima yawepo
mazingira mazuri ya kusimamia mchezo huu, ili upendwe na watu wengine pamoja na
kurudisha imani kwa wadau na wawekezaji waweze kuwekeza fedha zao. Hiki
kinachofanywa na Serikali ni kitu kizuri na kinafaa kuungwa mkono na wadau wa
mchezo huu” anasema Kimbau.
Awali Ngumi za Kulipwa
zilisimamiwa na Vyama tofauti tofauti ikiwemo Chama cha Wataalamu wa Mchezo wa
Ngumi Tanzania (TPBO), Pugilistic organization of Tanzania (PST) na Tume ya
Wataalamu wa Mchezo wa Ngumi Tanzania (TPBC).
Mtindo huo wa kuongoza
mchezo wa ngumi za kulipwa ulikuwa na namna ya vionozi na wachezaji kutoelewana
wenyewe kwa wenyewe kabla ya Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuingilia kati mgogoro huo
na kuamua kufanya mabadiliko katika mchezo wa Ngumi za Kulipwa ndipo TPBRC
ilipoanzishwa na kupewa mamlaka ya kusimamia Ngumi za Kulipwa mnamo mwaka 2018.
Kwa mujibu wa BMT, baada
ya kuundwa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa
yapo mafanikio yanayodhihirisha kuimarika
kwa mchezo huo yanayochagizwa kuwepo kwa viongozi waliopatikana kwa uchaguzi uliofanyika
Machi 31, 2019 ambao ni Joe Anea (Rais), Agapita Basil Jambwale (Makamu wa Rais),
Yahya Poli (Katibu Mkuu), Bakari Songoro (Mweka Hazina), Hamisi Kimanga na Nassoro
Chuma (Wajumbe).
Aidha, kuunganishwa kwa
wadau wa ngumi za kulipwa umeibua mwamko mpya kwa wadau hao, mabondia wanafanya
vizuri katika mashindano ya kimataifa ndani na nje ya nchi, kuongezeka kwa
idadi ya wakuzaji wa mchezo wa ngumi, kuongezeka kwa mapambano 35 ambayo yamefanyika kati ya
Aprili, 2019 hadi Machi, 2020.
Fauka ya hayo, wadhamini
kujitokeza kuwekeza katika kusimamia na kuhakikisha haki za mabondia
zinazingatiwa ikiwemo kupitiwa kwa mikataba yao ya mapigano kabla ya pambano
pamoja na kuimarika kwa mahusiano ya vyombo vya kusimamia michezo katika nchi
tofauti pamoja na vyama vinavyoshindanisha mikanda tofauti duniani ikiwemo,
WBO, WBA, WBC, ABU na UBO.
Hatua hiyo imesaidia wanachama
wa Ngumi za kulipwa waliosajiliwa kwa muda wa miaka mitatu kuanzia 2016 hadi
2019 kufikia 22, taswira ambayo inaonesha kuongezeka kwa mwamko wa kuanzisha na
kusajili vikundi vya sanaa na michezo nchini.
Kulingana na takwimu
hiyo, kati ya vikundi 22, vikundi 17 vinajihusisha na mchezo wa ngumi, sanaa na
michezo mingine wakati vikundi vitano tu vilivyoanzishwa na kusajiliwa
vinajihusisha na mchezo wa ngumi pekee.
Kwa hakika jambo hili
linaonesha wazi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imetekeleza agizo la CCM
katika ilani yake iliyotolewa wakati wa uchaguzi wa 2015 kwani kwa takwimu hizo ni kweli Serikali kwa
kishirikiana na sekta binafsi imeweza kuanzisha vituo vya kuendeleza vipaji vya
wanamichezo mahiri na kutumika kama vituo vya maandalizi ya wanamichezo
wanaoiwakilisha Tanzania katika michezo ya kimataifa.
Kwa mantiki hiyo,
mwandishi wa makala hii amebainisha kuwa mwamko wa kuanzisha michezo shirikishi
ni mkubwa zaidi kuliko mchezo mmoja mmoja na hatua hii Serikali inapaswa
kupongezwa kwani chanda chema huvishwa pete.
Kwa nafasi mafanikio
haya na nafasi hii, mwanamichezo anayeshriki katika mchezo wa ngumi akiwa
katika kikundi mazoezi (gym) anayonafasi kubwa zaidi ya kuwa mwanamasumbwi bora
zaidi ya yule ambaye yupo kweye masumbwi pekee.
Hatua hiyo inamsaidia
mwanamichezo kuwa bora katika mchezo katika kikundi ambacho kinahusisha mchezo
zaidi ya mmoja ana fursa ya kupata vifaa vinavyomsaidia kufanya mazoezi ya
uhakika, utimamu wa mwili na kupata msaada wa kitaalamu katika mchezo husika kutoka
kwa walimu mbalimbali wanaokuwepo wakati wa mafunzo na mazoezi yanayompa motisha
unaompelekea kuwa mwanamichezo bora.
Hakika Kamisheni ya
Kusimia Ngumi za Kulipwa imekuwa mwarobaini wa mchezo huo ambapo migogoro ya
mara kwa mara imekuwa ni historia ikiwemo mapromota kuvamia tasnia hiyo na
kuharibu mustakabali mzuri wa mchezo huo nchini.
Ni ukweli usiopingika,
kila lenye mafanikio halikosi kuwa na changamoto, mchezo wa ngumi za kulipwa bado
unakabiliwa na changamoto ya kutokuwepo kwa makocha wenye viwango vya kimataifa
wenye nyota zinazotakiwa, vifaa vya kufanyia mazoezi, uhaba wa wadhamini pamoja
na maeneo ya kufanyia mazoezi na ulingo unaotumika wakati wa mashindano. Kwa
hakika Serikalia ya Awamu ya Tano itaendelea kuzitatua changamoto zote
zilizosalia na kwa hakika mambo yatakuwa mazuri hivi punde.
Mafanikio haya
yaliyofikiwa ni makubwa mno kwa mchezo huu ulionza kuchezwa hata kabla nchi
yetu haijatawaliwa na wakoloni katika karne ya 19. Mchezo huu ulichezwa katika
viwanja vikubwa vyenye mikusanyiko mikubwa ya watu (Coliseum) huko Roma na
(Arena) huko Athina, iliyokuwa katika hekalu kubwa la ufalme wa Wayunani
(Ugiriki) la Akropolis. Viwanja hivyo vilikuwa ndio mwanzo wa ulingo wa kisasa
kwani japokuwa ulingo wa kisasa ni wa mraba lakini mwanzo wake ni Arena ya
mduara.
No comments:
Post a Comment