Habari za Punde

Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Hamad Rashid Azungumza na Mwakilishi wa W H O

Mwakilishi mkaazi wa shirika la afya duniani (WHO) Dk. Andemichael Ghirmy (kushoto)akizungumza na Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohammed kuhusiana na matayarisho ya upokeaji watalii kipindi hichi cha mripuko wa maradhi ya korona huko Wizara ya Afya Mnazimmoja Mjini Zanzibar.


Na. Sabiha Khamis - Maelezo Zanzibar.
Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed amelishukuru Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa juhudi kubwa walizozichukuwa kushirikiano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika Mapambano dhidi ya maradhi ya Corona nchini.
Hayo ameyasema huko Ofisini kwake Mnazi Mmoja wakati akizungumza na Mwakilishi Mkaa wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Dk. Andemichael Ghirmy aliofika Ofisini hapo kujua hatua iliofikia kwa maradhi hayo.
Amesema kwa sasa maradhi hayo yamezibitiwa kwa kiasi kubwa hali ambayo imewapa matumaini mazuri yakuweza kuruhusu shughuli za kikazi kuendelea kama kawaida na kuruhusu Wageni kuingia nchini bila ya pingamizi wakiwemo watalii.
“Tumeruhusu Wageni waingie nchini bila ya wasiwasi wowote kwani tumejipanga vizuri kwa matibabu na kuwashughulikia kwa kuwapima na kujua taarifa zao, kwani Zanzibar maradhi haya yamepungua kwa kiasi kikubwa na ikigundulikana mmoja wao ana maradhi tutahakikisha tunampatia matibabu ipasavyo,” alisema Waziri.
Aidha alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inalipongeza Shirika hilo kwani mafanikio hayo yametokana na juhudi ya pamoja kwa kutoa misaada yao na kupeana taarifa za kitaalamu.
Hata hivyo aliwataka wananchi kuchukua tahadhari kwa wageni wanaoingia kwani bado zipo nchi za jirani zinasumbuliwa na maradhi hayo.
Aliwataka washirika wa kimaendeleo kuendelea kuwaunga mkono mara tu inapotokea mripuko wa maradhi ya aina yoyote ikiwemo Kipindupindu, Malaria na mengineyo ili kuweza kuyadhibiti kwa haraka sana.
Hata hivyo, Waziri huyo alifanya ziara kutembelea katika maabara akiwa na mwakilishi mkaazi huyo wa (WHO) katika Hospital ya Rufaa Mnazi Mmoja kuona kifaa cha kupimia Corona.
Nae Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Dk. Andemichael Ghirmy amesema ataendelea kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya afya na kuhakikisha wanakwenda sambamba na maradhi ya miripuko ambayo yataweza kujitokeza.
Alisema licha kupungua kwa maambuizi ya Corona nchini pia wanajipanga kutokomeza Kipindupindu Zanzibar kupitia Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa ili kuhakikisha maradhi hayo yanaondoka kabisa kwa Unguja na Pemba.
Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohammed (katikati) akizungumza na Mwakilishi  mkaazi wa shirika la afya duniani (WHO) Dk. Andemichael Ghirmy (kushoto) kuhusiana na matayarisho ya upokeaji wa watalii  kipindi hichi cha mripuko wa maradhi ya korona huko Wizara ya Afya Mnazimmoja Mjini Zanzibar. 
Mwakilishi mkaazi wa shirika la afya duniani (WHO) Dk. Andemichael Ghirmy akitoa maelekezo kwa mkuu wa maabara Fauzia Ameir huko Ofisi ya maabara ya Hospital ya Rufaa ya Mnazimmoja.
Mkuu wa maabara ya Hospital ya Rufaa ya Mnazimmoja Fauzia Ameir akifafanua juu ya maandalizi ya utumikaji wa mashine mpya ya kupimia virusi vya Corona huko  Ofisi ya maabara ya Hospital ya Rufaa ya Mnazimmoja.
PICHA NA FAUZIA MUSSA/MAELEZO ZANZIBAR.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.