Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Ali Mohamed Shein Akizungumza na Wananchi wa Ole na Kengeja Pemba.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein akizungumkza na Wananchi wa Ole Kengeja na Kengeja wakati wa hafla ya ufunguzi wa barabara hiyo,mkutano huo umefanyika katika uwanja wa mpira Kengeja Wilaya ya Mkoani Pemba. 
 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa barabara zinafungua milango na kuleta manufaa katika ukuaji na maendeleo ya uchumi na kijamii.

Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo katika ufunguzi wa barabara ya Ole hadi Kengeja yenye urefu wa kilomita 35, hafla iliyofanyika huko katika viwanja vya skuli ya Kengeja, Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba.

Viongozi mbali mbali walihudhuria katika hafla hiyoakiwemo Mama Mwanamwema Shein, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Naibu Katibu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Mabodi, Mawaziri pamoja na viongozi wa vyama vya siasa, Serikali na wananchi,

Alisema kuwa ujenzi wa barabara unaimarisha makaazi ya wananchi kwani walio wengi huvutika kujenga karibu na maeneo ya barabara ambapo pia shughuli za maendeleo ya biashara, kilimo, uvuvi na nyenginezo nazo huimarika.

Serikali ya Awamu ya Saba imejitahidi kuweka mfumo wa barabara katika hali nzuri hivyo, ni wajibu wa Taasisi nyengine zinazohusika na usafiri na usafirishaji pamoja na usalama wa abiria na mizigo kushirikiana pamoja kuona kuwa ajali za barabarani zinapungua.

Alitumia fursa hiyo kuziagiza Mamlaka zinazohusika kuweka alama za usalama barabarani ili ziwaongoze madereva na wapita njia katika kuzitumia barabara vizuri kwa usalama wao na vyombo vinavyoendeshwa.

Alisema kuwa kujenga barabara ni gharama lakini ikiwa zitatumika vyema na kupata matunzo mazuri gharama hizo zinafidiwa na ukuaji wa wa uchumi kwa mtu mmoja mmoja, jamii na nchi kwa jumla.

“Tumeweza, hatimae tumejenga sisi wenyewe  na mkopo wa Benki ya Kimataifa ya Nchi zinazotoa Mafuta kwa wingi (OFID) haukutosha tukaongezea wenyewe hivyo, wajue kama na sisi wenyewe tuna uwezo mkubwa”, alisisitiza Rais Dk. Shein.

Aidha, Rais Dk. Shein alisema kuwa barabara hiyo ni barabara ya watu wote wa Unguja na Pemba huku akitumia fursa hiyo kuipongeza Mamlaka ya UUB kwa kutengeneza barabara hiyo pamoja na kuwapongeza viongozi na wafanyakazi wa Wizara hiyo.

Rais Dk. Shein alisema kwamba njia nyengine  ya kuzitunza barabara ni kujiepusha na ajali za barabarani ambapo takwimu kutoka Idara ya Usalama Barabarani zinaeleza kwamba  ajali nyingi zimekuwa zikitokea hivyo, kuna kila sababu ya kuziepuka.

Aidha, alisema kuwa kwa upande wa barabara  hiyo iliyofunguliwa leo yenye urefu wa kilomita 35 ndio ndefu zaidi kuliko barabara zote hapa Zanzibar.

Rais Dk. Shein aliwataka wananchi kuitunza barabara hiyo iliyotoka Ole hadi Kengeja hasa ikizingatiwa kwamba hilo si jukumu la Serikali peke yake kwani Serikali ni watu.  

Akieleza historia fupi ya barabara kisiwani Pemba , Rais Dk. Shein alisema kuwa barabara hiyo inatokana na lengo na mawazo yaliyowekwa na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume katika kuhakikisha mtandao wa barabara unaimarika kati ya Kusini hadi Kaskazini mwa visiwa vya Unguja na Pemba.

Alisema kuwa ujenzi wa barabara unagharimu fedha nyingi ambapo kilomita moja ya barabara inagharimu TZS bilioni moja kuijenga mpaka ikafikia kiwango cha lami.

Hivyo, alieleza kuwa unapofanywa uharibifu wa barabara ijulikane kwamba gharama za kuzitengeneza zina athari kubwa kwa uchumi na wananchi  kwa jumla kwa sababu barabara ni miongoni mwa vitega uchumi kwa maendeleo ya jamii na nchi nzima.

Rais Dk. Shein pia, alikemea tabia ya kujenga pembezoni mwa barabara bila ya kuhojiwa na kuitaka Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati kufuatilia ili kuondosha madhara ya hapo baadae huku akisisitiza haja ya kujengwa misingi pembezoni mwa barabara ili kuepuka athari kwa makaazi ya wananchi.

Katika hafla hiyo pia, Rais Dk. Shein alimpongeza Waziri wa Wizara hiyo Dk Sira Ubwa Mamboya kwa kutekeleza maagizo yote aliyopewa na Serikali ikiwa ni pamoja na kuijenga barabara hiyo ya Ole hadi Kengeja pamoja na ukamilishaji wa jengo la abiria la Terminal III na maandalizi ya Bandari kuu ya Mpigaduri.

Mapema mara baada ya kuifungua barabara hiyo wakati akiwasilimia wananchi huko Ole, Rais Dk. Shein aliwaeleza wananchi hao waliofika katika eneo hilo kutambua kwamba barabara hiyo ni yao hivyo wanatakiwa kuitunza.

Aidha, aliwataka madereva kutoendesha gari zao kwa mwendo wa kasi ili kuepuka ajali hasa kwa watoto ambao ndio viongozi wa kesho.

Nae Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Dk. Sira Ubwa Mamboya alitoa pongezi wka Rais Dk. Shein kwa ukamilishaji wa barabara hiyo ambayo hatua hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020.

Alisema kuwa ujenzi wa barabara hiyo ni sehemu ya SMZ kuimarisha miundombinu ya barabara kwa lengo la kuimarisha uchumi na maendeleo hapa nchini ambapo pia utaondosha msongamano wa barabara katika mji wa Chake Chake pamoja na kuunganisha Wilaya ya Chake na Mkoani.

Akitoa maelezo Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Mustafa Aboud Jumbe alisema kuwa ujenzi wa barabara hiyo yenye kilomita 35 unajumuisha Wilaya mbili za Chake Chake na Mkoani na kupita katika Shehia 15.

Pia, alisema kuwa barabara hiyo ina upana wa mita 7.5 na imejengwa kwa kiwango cha lami ya moto na ina uwezo wa kutumiwa na gari yenye uzito wa tani 10 ambayo ina madaraja 16 na culvert ndogo ndogo 118 pamoja na miundombinu ya kupitishia huduma za kijamii ikiwemo mabomba ya maji.

Alieleza kuwa ujenzi wa barabara hiyo umefanywa na Wizara ya Ujenzi, mawasiliano na Usafirishaji kupitia Idara yake ya UUB ambayo sasa ni Wakala wa Barabara chini ya Usimamiazi wa Kampuni ya Kizalendo ya KAPSEL kutoka Dar es Salaam.

Alisema Ujenzi huo umefanywa kupitia mkopo wa Benki ya Wanachama wa Nchi zinazotoa mafuata kwa wingi Duniani (OFID) ikishirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo hadi kukamilika kwake mradi huo umegharimu TZS Bilioni 30.935.

Alisisitiza kuwa kati ya fedha hizo mkopo kutoka OFID umechangia TZS Bilioni 24.2 na SMZ imechangia TZS Bilioni 6.735.

Nao wananachi walimpongeza Rais Dk. Shein kwa kuijenga barabara hiyo ambayo itakuwa ni kichocheo cha uchumi na maendeleo yao.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.