Habari za Punde

Waandishi Watakiwa Kuripoti Habari za Miradi ya Maendeleo Kuwahabarisha Wananchi.

Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu Hassan Khatibu Hassan akiwasisitiza Waandishi wa Habari kufuatilia Miradi ya Maendeleo  katika Mkutano uliofanyika Ukumbi wa Sanaa Rahaleo (kulia) Mkuu wa Ufuatiliaji Kisekta kutoka Tume ya Mipango Hamad Abdalla Haji.

Baadhi ya waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali wakimsikiliza Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu Hassan Khatibu Hassan (hayupo pichani) wakati wa Mkutano wa Ufuatiliaji wa Miradi ya Maendeleo uliofanyika Ukumbi wa Sanaa Rahaleo.

(Picha na  Ramadhan Ali –Maelezo)

Na Kijakazi Abdalla - Maelezo  Zanzibar.

Waandishi wa Habari wametakiwa kufuatilia miradi inayoanzishwa ili kujua maendeleo yake na kusikiliza matatizo yanayowakabili wananchi na kuyawasilisha Serikalini kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi.

Akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu ufuatiliaji wa Miradi ya Maendeleo katika Ukumbi wa Sanaa Rahaleo, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu Hassan Khatibu Hassan aliwashauri waandishi kuwa tayari kubadilika na kuisaidia Serikali katika juhudi zake za kuwatumikia wananchi.

Amesema waandishi wa Habari wanawajibu wa kufuatilia miradi  iliyoazishwa na Serikali kujua inavyotekelezwa na kasoro zitakazojitokeza ili wananchi waweze kufaidika na miradi hiyo.

Mkurugenzi Hassan amesisitiza kuwa Serikali ya awamu ya nane imekusudia kuwapatia wananchi huduma zote zinazostahiki kwa lengo la kuwapunguzia ugumu wa maisha.

 “Serikali hii ya awamu ya nane ni ya wananchi hivyo taarifa zenu ziwe na lengo la kuwasaidia wananchi,” Alisisitiza Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu.

Mkuu wa Ufuatiliaji Kisekta kutoka Tume ya Mipango Hamad Abdalla Haji amesema Serikali itaendeleza miundo mbinu ya barabara mbali mbali za Mkoa wa Kusini na Kaskazini Unguja na barabara za Pemba ili kuwaondoshea wananchi tatizo la usafiri.

Aidha amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendeleza lengo lake la kuwapatia wananchi huduma ya maji safi na salama mijini na vijijini katika mikoa yote ya Zanzibar.

Mkuu huyo wa ufuatiliaji kutoka Tume ya Mipango ameeleza kuwa kuibuka kwa maradhi ya covid 19 kumepelekea baadhi ya miradi kutofanyika kama ilivyopangwa lakini hivi sasa juhudi zinachukuliwa kuhakikisha inatekelezwa.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.