Habari za Punde

Serikali kupambana na vitendo vya udhalilishaji dhidi ya watoto na wanawake

 

                                  STATE HOUSE ZANZIBAR

                       OFFICE OF THE PRESS SECRETARY

                                          PRESS RELEASE

Zanzibar                                                                         Januari 03, 202i

 

WAZIRI wa Nchi (OR) Afisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka mikakati maalum kwa kipindi cha mwaka 2017 – 2022 ikiwa ni hatua ya  kupambana na vitendo vya Udhalilishaji dhidi ya watoto na wanawake nchini.

 

 Waziri Haroun amesema hayo wakati akifungua Tamasha la kwanza la pongezi  kwa Wana Sunni Madrasa katika hafla iliyofanyika Ukumbi wa Sunni Madrasa, Mkunazini jijini Zanzibar.

 

Akimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi; Waziri Haroun aliahidi kukutana na wadau wanaoshughulikia vitendo vya Udhalilishaji, ikiwemo Jeshi la Polisi, Mahakama na Ofisi ya Muendesha Mashtaka  kwa lengo la kujenga mikakati ili  kuharakisha usikilizaji  wa kesi za makosa hayo yalioshamiri nchini.

 

Alisema Serikali hairidhishwi na mlundikano uliopo wa kesi za udhalilishaji  na hivyo akaitaka jamii kujenga mashirikiano na vyombo vya sheria ili kufanikisha mchakato wa kesi pamoja na kuondokana na muhali.

 

Alitumia fursa hiyo kuwapongeza walimu wanaofundisha fani hiyo ya ‘Nasheed’ kwa kazi nzuri wanayofanya pamoja  na kuwoamba kuendelea  na juhudi za kuisambaza taaluma hiyo hadi vijijini Unguja na Pemba.

 

Katika hafla hiyo Waziri Haroun alikabidhi zawadi kwa washindi wa Tamasha hilo la ‘Nasheed’ , ambapo mwanafunzi Nasra Abdalla Mohamed alikuwa mshindi wa kwanza na hivyo kuzawadiwa Friji, Mkoba pamoja na Ma-shafu.

 

Aidha mwanafunzi Asiat Ramadhan Jussa alikuwa mshindi wa pili na  kuzawadiwa zawadi za Cherehani, Mkoba na Mas-hafu, huku mwanafunzi Mudrik Msellem Ali akiondoka na ushindi wa tatu na kuzawadiwa Baiskeli, Mkoba na Mas-hafu.

 

Mapema, Katibu mtendaji Idara  ya  Sensa na Sanaa Omar Abdalla Adamu aliwashukuru waandaji wa Tamasha hilo na kusema wamekamilisha taratibu zote za kisheria na kufauta mila, silka na utamaduni wa Mzanzibari.

 

Nae, Sheikh Habibu Othman ‘Mazinge’ aliwata waislamu nchini kote  kumuomba Mwenyezi Mungu adumishe amani na umoja miongoni mwa Wazanzibari.

 

Aidha, aliumuomba Mwenyezi Mungu kuilinda Zanzibar ili iendelee kubaki na  amani na usalama pamoja na kuwajaalia viongozi wote wa Serikali amani.

 

Katika tamasha hilo wanafunzi 20 walisoma ‘Nasheed’ mbali mbali zenye maudhui ya kupinga vitendo vya Udhalilishaji kwa watoto na wanawake.

 

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 

 E-mail: abdya062@gmail.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.