Habari za Punde

Serikali haitokuwa na muhali kumchukulia hatua kiongozi yeyote atakaebainika kuingilia uhuru wa Mahakama

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Watendaji wa Sekta ya Sheria pamoja na Wanamichezo mbali mbali baada ya kumalizika kwa Matembezi ya Siku ya Sheria Zanzibar hapo katika Viwanja vya Maisara Suleiman Mjini Zanzibar.

 Baadhi ya Watendaji wa Sekta ya Sheria wakifuatilia Hotuba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman hayupo pichani hapo Viwanja vya Maisara Suleiman.

Picha na – OMPR – ZNZ.


Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haitasita kumchukulia hatua za Nidhamu pamoja na zile za Kisheria Kiongozi ye yote wa Taasisi ya Umma atakayebainika kuingilia uhuru wa Mahakama katika masuala yote yanayohusiana na Kesi ya Udhalilishaji hapa Nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla wakati akizungumza na Watendaji wa Sekta ya Sheria na Wanamichezo mbali mbali baada ya kumalizika kwa Matembezi ya Siku ya Sheria Zanzibar hapo katika Viwanja vya Maisara Suleiman Mjini Zanzibar.

Mheshimiwa Hemed Suleiman ameuagiza Uongozi wa Mahakama kutoa taarifa mara moja pale utakapobaini uwepo wa Kiongozi anayejaribu kuingilia kati mwenendo wa Kesi za udhalilishaji ama kwa kutuhumiwa yeye binafsi au rafiki na hata Jamaa wake wa karibu.

Alisema matendo ya Udhalilishaji yanayooenaka kushamiri kila kukicha na kulitia aibu Taifa ndani ya kipindi hichi lazima yadhibitiwe kwa nguvu zote huku akiwataka Majaji na Mahakimu wanaosimamia Mashauri hayo kuharakisha kesi zote zinazowahusu watuhumiwa wa Udhalilishaji.

Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alibainisha wazi kwamba ili  mapambano dhidi ya vitendo vya udhalilishaji yafanikiwe Wananchi watakaobahatika kushuhudia matendo hayo katika maeneo yao ni vyema wakabeba dhima ya kutoa ushahidi Mahakamani pale watapohitajika kufanya hivyo.

Alifahamisha kwamba kinachohitajika kwa sasa ni Mahakimu na Majaji kuepuka mazingira yanayotengeneza sintofahamu zinazozaa chuki na uhasama hapo baadae kati ya makundi yanayotuhumiwa dhidi ya yale yaliyodhalilishwa.

Siku ya Sheria Zanzibar kuadhimisha ifikapo Tarehe Nane ya kila Mwaka ambapo Mwaka huu wa 2021 Ujumbe mahsusi wa Siku hiyo unaeleza” Wajibu wa Mahkama na Wadau wa Sheria kuendana na Kasi ya Awamu ya Nane katika kushughulikia kesi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.