Habari za Punde

Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Kuzindua Mwongozo wa Wawekezaji Mkoani Tanga.

Na Hamida Kamchalla, KOROGWE.

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema pamoja na kuzindua miradi ya maendeleo katika ziara yake mkoani Tanga, pia atazindua Mwongozo wa wawekezaji ambapo amesisitiza wawekezaji kuja kuwekeza kwa wingi mkoani hapa.

Aliyasema hayo jana alipokuwa wilayani Korogwe na kueleza kipaumbele cha mkoa huo kuwa ni uwekezaji wa viwanda na biashara pamoja na kilimo kutokana na kuwepo kwa viwanda vingi miaka ya nyuma na kipaumbele hicho kitapelekea kuleta chachu ya uwekezaji kuongezeka na vilivyokufa kufufuliwa.

Suluhu alibainisha kwamba ukizungumziwa mkoa huo unaleta taswira ya viwanda vingi ambavyo vinazalisha bidhaa pamoja na kuzalisha mazao ya biashara kwa wingi jambo linaloisukuma serikali kutafuta wawekezaji kwa wingi hata kwa viwanda vya usindikaji wa matunda na uchakataji wa mazao ya nafaka.

"Serikali inatafuta wawekezaji kwa nguvu kuja kuwekeza katika sekta ya viwanda katka mkoa wa Tanga kwa kuona una viwanda vingi, zamani mkoa ulikuwa na viwanda vingi vingine vimekufa, tunataka wawekezaji waje wawekeze na vilivyokufa vifufuliwe ili kuinua uchumi wa Taifa letu katika sekta ya viwanda" alisema.

Alisema mazao ya kimkakati yalikuwa ni mkonge na pamba lakini kwa mkoa lakini kuna mazao mengi kama matunda (machungwa) na mahindi nayo yawekwe kwenye orodha ya mazao ya kimkakati kutokana na kuwepo kwa viwanda karibu vya mazao hayo.

"Awali mliweka mazao ya mkonge na pamba yawe ya kimkakati ndani ya mkoa lakini kwa sasa naona mazao ya mahindi na hata machungwa yanazaliwa kwa wingi, itabidi nayo yawe mazao ya kimkakati" aliongeza.

Aidha aliongelea kilimo kingine kinachoweza kubadilisha kipato cha mkulima wa kawaida kuwa ni zao la muhogo ambalo wawekezaji tayari wako kwenye mchakato wa kujenga kiwanda cha kuchakata huku soko lake likiwa nje ya nchi na tayari wawekezaji wa masoko wanahitaji kwa wingi zao hilo.

Aliwasisitiza wakulima kuzalisha kwa wingi zao hilo ili kuweza kuwafanya wawekezaji kuongezeka na kwamba haitakuwa busara na rahisi kutangazia wawekezaji nafasi za masoko bila kuwa na bidhaa inayojitosheleza.

"Kwa upande wa zao la muhogo wwtu walikuwa wanaogopa kulima kwakuwa masoko hayakuwepo lakini niwaambie kwamba mlime kwa wingi muhogo sasa masoko yapo na karibuni muwekezaji atakuja kujenga kiwanda cha kuchakata, tumeshatangaza soko la zao hilo inabidi muongeze juhudi katika uzalishaji, zao lisikosekane" alisema.

Alisema kupitia viwanda hivyo wakinamama na vijana wengi wanapata ajira katika viwanda lakini pia wawekezaji hao wanaleta manaleta mafanikio kwa kusaidia kuunga mkono juhudi za serikali kwa kujenga miradi ya maendeleo katika maeneo yanayozuwazunguka.

Hata hivyo aliwataka wananchi wanaozunguka maeneo ya wawekezaji kuchangamkia fursa ya ajira pindi zinapotokea huku akitoa pongeza kwa vijana kuwa watiifu katika ujenzi mbalimbali wa miradi kwa kujiyolea na kutunza mazingira pamoja na vifaa vinavyohofadhiwa.

Makamu wa Rais atafanya uzinduzi wa Mwongozo wa Wawekezaji siku ya alhamisi tarehe 18 katika Hotel ya Regal Naivera jijini Tanga ambapo wadau wakubwa watakuwa ni wawekezaji wakubwa na wadogo kutoka ndani na nje ya nchi pamoja na wafanyabiashara.

Vilevile Suluhu alitoa salamu kutoka kwa Rais kwa wananchi na kusema amesisitiza kudumisha mshikamano, amani, umoja na upendo kwa kufanya kazi kwa bidii na kuleta maendeleo kwa Taifa na kupuuza watu wanaosambaza maneno kwenye mitandao ya kijamii.

"Nitoe salamu za muheshimiwa Rais, ameniagiza niwape salamu zake, muendelee kudumisha mshikamano, umoja, amani na upendi kwa kila mmoja na kufanya kazi kwa bidii badala yake muwapuuzie wanaotaka kuvuruga amani ya nchi kwa kusambaza maneno yatakayoleta mtafaruku" alisisitiza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.