Habari za Punde

Kamati ya Kukabiliana na Maafa Yafanya Ukaguzi Skuli ya Sekondari ya Lumumba.

SGT.Halima Ameir Makame kutoka Kikosi cha Zima Moto na Uokozi Zanzibar akitikicha chupa ya kuzimia moto (fire extinguisher) iliopo lebo ya Skuli ya Sekondari ya Lumumba wakati wa ukaguzi wa kutizama mazingira hatarishi katika maeneo mbalimbali ya skuli hiyo , uliofanya na Kamati ya kukabiliana na  Maafa Zanzibar.

Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya kukabiliana na maafa wakichunguza sehemu  hatarishi katika lebo ya Skuli ya Sekondari ya Lumumba  wakati wa ukaguzi wa mazingira hatarishi katika maeneo mbalimbali ya skuli hiyo .

Picha na Khadija Khamis -Maelezo Zanzibar.

Na Khadija Khamis Maelezo Zanzibar 02/04/2021.

Kamati ya Kukabiliana na Maafa  Zanzibar imewataka walimu wa Skuli ya Sekondari ya Lumumba kuzidisha juhudi ya kuzuwia matumizi ya umeme kwa wanafunzi waliopo kambini jambo ambalo litasaidia kuepukana  na majanga ya moto .

Hayo aliyasema SGT.Halima Ameir Makame kutoka Kikosi cha Zimamoto na Uokozi walipofanya ukaguzi katika Skuli hiyo kwa lengo la kuchunguza mazingira hatarishi na kupatiwa ufumbuzi.

 Amesema kawaida ya wanafunzi huwa wajanja hivyo jitihada za makusudi zinahitajika kudhibiti  matumizi  ya umeme ikiwemo pasi ili kuepusha athari za miripuko ya moto katika vyumba vyao .

Nae Mfanyakazi wa Shirika la Umeme Zanzibar  (ZECCO) Yussuf Hamad Omar amesema hakuridhika na mpangilio wa waya za umeme zilizopo katika chumba cha kusalia  wanafunzi, hivyo aliwataka wahusika kuzifanyia matengenezo ya haraka  ili kuepusha madhara kwa wanafunzi .

Mkuu wa Divisheni  ya Operesheni na Huduma za Kibinaadamu Jabu Sharif Haji alisema elimu ya kengele ya dharura itolewe kwa wanafunzi kutokana na muamko mdogo uliopo.

Pia alisema usimamizi wa vyoo unahitaji kuimarishwa zaidi kwa kusafishwa mara kwa mara jambo ambalo litasaidia kuepukana na maradhi ya mripuko.

Amesema ameridhishwa na mapokezi na mashirikiano ya walimu wa skuli hiyo kwa kutoonyesha hofu kwa ujio huo ambao ni wa kushtukiza .

Kwa upande wa Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari ya Lumumba, Mussa Hassan Mussa ametoa malalamiko kwa Wafanyakazi wa Shirika la Umeme (ZECCO)  kutoonyesha mashirikiano zinapotokea kesi  jambo ambalo linachangia hofu kwa Walimu .

Aidha alisema tayari wamesharipoti kesi ya kuanguka kwa waya katika jumba bovu lililopo pembeni ya Skuli hiyo lakini bado hatua haijachukuliwa  .

Mwalimu huyo alitoa wito kwa wazazi na walezi wa wanafunzi hao kutoa mashirikiano ya pamoja ili kudhibiti adhari zitazoweza kujitokeza.

Kamati ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar imehusisha Idara mbali mbali zinazohusika na maafa ikiwemo Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa, Kikosi cha Zimamoto na Uokozi pamoja na Shirika la Umeme Zanzibar .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.