Habari za Punde

Wanawake Wilaya ya Siha Vinara wa Urejeshaji wa Mikopo.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel akimpongeza mmoja wa akina mama wa Wilaya ya Siha kwa kupata mkopo wa Sh.Mil. 3 kutokana na fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Siha.
Baadhi ya wanufaika wa mkopo wa Sh. Mil. 72 zilizotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Siha wakimsikiliza Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel (hayupo pichani) kabla ya kukabidhiwa mkopo huo.

Na Mwandishi wetu, Siha

Halmashauri ya Wilaya ya Siha, Mkoani Kilimanjaro imekabidhi jumla ya kiasi cha shilingi milioni 72 kwa ajili ya mkopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, Wilayani humo ikiwa ni fedha zinazotokana asilimia 10 mapato ya Halmashauri hiyo.

 

Akikabidhi fedha hizo, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel amewapongeza wanavikundi kwa kurejesha mikopo yao kwa wakati ili fedha hizo ziweze kuwanufaisha walengwa wengi zaidi.

 

Aidha, amewataka walengwa hao kuendelea kushikamana na kufanya kazi kwa bidii ili kujiinua kiuchumi na hatimaye kufanikisha Maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

 

Amesema Serikali itaendelea kuwashika mkono ili kuhakikisha wanaimarika zaidi katika vikundi vyao pamoja na mtu mmoja mmoja.

 

Dkt. Mollel pia ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Siha kwa kubuni vyanzo zaidi vya mapato na kuweza kuhakikisha inatenga zaidi ya Sh.Mil.48 kila mwaka kwa ajili ya kuwawezesha wanawake kiuchumi.

 

" Tunapoelekea sasa tutaangalia zaidi sheria hii ili wanufaika hawa waweze kupewa mmoja badala ya vikundi, tumetembea maeneo mengi lakini Wilaya ya Siha mnafanya vizuri" alisema Dkt.Mollel.

 

Mkuu wa Wilaya ya Siha, Onesmo Buswela alisema mikopo hiyo imechangia kupungua kwa vitendo vya unyanyanyasaji wa kijinsia katika Wilaya hiyo kutokana na wanawake wengi kujikwamua kiuchumi.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Ndaki Stephano alisema hakuna vikundi ambavyo ni sugu kulipa na kuongeza kuwa, mikopo hiyo inawasaidia hasa wanawake na kuwa Halmashauri inaendelea kuwatembelea vikundi hivyo na kuwapatia elimu ya mikopo.

 

Ndaki aliongeza kuwa Halmashauri ina mpango wa kutenga fedha zaidi ili vikundi hivyo viweze kuanzisha viwanda vidogo vidogo vitakavyosaidia kutoa ajira nma kukuza uchumi.

 

Awali akitoa taarifa ya mikopo hiyo, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha Marco Masue alisema kiasi cha Sh.Mil. 48.5 ni mapato ya ndani ya Halmashauri na Sh.Mil 23.7 ni marejesho ya mikopo hivyo imesaidia katika kuwafikia wanufaika wengi zaidi kupata mikopo .

 

Kwa upande wao baadhi ya wanufaika Penina Maduhu na  Michael Nko wameishukuru Serikali kwa kuwawezesha kupata mikopo hiyo na kueleza kuwa inawasaidia kuinua uchumi wa familia zao na kuongeza wigo wa shughuli wanazozifanya. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.