Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itachukua hatua kali kwa watakaohusika na ubadhirifu wa mali za Umma kupitia ripoti ya mdhibiti na mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali iliowasilishwa hivi karibu kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la MapinduziMhe.Hussein Ali Mwinyi.
Mhe. Hemed alitoa kauli hiyo wakati akiakhirisha mkutano wa tatu wa baraza la kumi la wawakiklishi huko chukwan nje kidogo ya jiji la Zanzibar.
Alieleza kuwa, serikali itachukua hatua hizo ili kurejesha nidhamu kwa watumishi wa umma katika suala zima la kuheshimu fedha na mali za Umma na kuahidi katika hatua hizo hakuna mtu yoyote atakaeonewa au kudhulumiwa kwa namna yoyote ile.
Alisema ripoti ya mdhibiti na mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali imebainisha baadhi changamoto mbali mbali zinazohusiana na idara, taasisi pamoja na mashirika hivyo, serikali itachukua hatua kwa kuzingatia sheria za nchi zinavyoelekeza.
Makamu wa Pili wa Rais alisema bajeti ya mwaka 2021/2022 imezingatia malengo ya dira ya maendeleo ya zanzibar 2050, ilani ya uchaguzi ya CCM, ahadi pamoja na maagizo mbali mbali alioyatoa Mhe. Rais DK. Hussein Mwinyi wakati akiomba ridhaa ya kuchaguliwa na wananchi wa Zanzibar hivyo, katika kufikia adhma ya bajeti hiyo kunahitajika nidhamu kwa ajili utekelezaji wake.
“Mafanikio ya bajeti ya serikaili tuliyoipitisha yanategemea sana nidhamu ya ukusanyaji wa mapato pamoja na matumizi ya hicho tulichokikusanya” Alisema Mhe. Hemed
Alieleza kwamba serikali itaweka mkazo Zaidi katika usimiaji wa bajeti iliopitishwa kwa ukamilifu wake kwani endapo kutatokea uzaifu katika usimamiaji mipango na kazi iliopangwa kutekelezwa itakuwa sawa na kazi bure.
Akigusia kuhusu kodi ya majengo (Propert Tax) Makamu wa Pili wa Rais wa Rais amewatoa hofu wananchi kwamba kodi hiyo haipo kwa ajili ya kumkomoa mtu na wala haitowagusa wananchi wanyoge na wale wanaotumia majengo kwa ajili ya makaazi binafsi kwani serikali imedhamiria kusimamia ukusanyaji wa mapato kupitia sheria ya kodi inayohusisha majengo ya kibiashara.
“Napenda niweke wazi kuwa wanaohusika ni wale ambao nyumba zao zinatumika kibiashara tu kwa kulipia kiwango cha shilling elfu Kumi (10,000/) kwa kila ghorofa moja au kwa nyumba ambayo thamani yake inaanzia Millioni hamsini (50,000,000) kwa nyumba ya kibiashara isiokuwa na ghorofa, Nawaomba sana wananchi waliunge Mkono jambo hili” Alieleza Makamu wa Pili
Aidha, Alisema kuwa serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Dk. Hussein Mwinyi itaendelea kulinda maslahi ya wananchi wake kwa kuzingatia uwajibikaji kwa watumishi ambao wamepewa dhamana ya kusimamia makusanyo na matumizi ya serikali.
Akizungumzia suala la Ajira na ukuaji wa uchumi Mhe. Hemed alieleza kuwa serikali itaendelea kufungua fursa mbali mbali za uwekezaji nchini kwa kuwajengea mazingira bora wawekezaji wagaeni na wenyeji kwa kutengeneza mazingira mazuri kwa kuzifanyia marekebisho sheria zote zinazohusiana na masuala uwekezaji ili kuepusha urasimu.
Pia, kupitia sekta ya utalii alisema serikali imekuwa ikitegemea sekta hiyo kwani imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa cha fedha za kigeni hadi kufikia kuchangia (27%) ya pato la Taifa (GDP) lakini kutokana na maradhi ya Covid 19 yaliosambaa duniani nchi nyingi ikiwemo Zanzibar na kupelekea kupokea idadi ndogo ya watalii.
“ Kwa kuwa nchi haikuthariwa sana na ugonjwa wa Covid 19, serikali itaendelea na juhudi zake za kujitangaza ili watalii wengi Zaidi waweze kuingia nchini mwetu” Alisema Makamu wa Pili
Wakati akiakhirisha mkutano wa tatu wa Baraza la kumi Makamu wa Pili wa Rais alitoa wito kwa vyombo vya habari vilivyopo nchini kufanya kazi kwa ushindani ili kuendana na kasi na vyombo vyengine vya habari na kuwavutia wananchi walio wengi.
Alisistiza kuwa lengo la serikali inataka kuviona vyombo vya habari nchini vinafanya kazi zake bila ya vikwazo hivyo serikali itazipitia sheria zote zinazokwamisha uhuru wa vyombo vya habari na kuzianyia marekebisho.
Pamoja na mambo mengine Mhe. Hemed aliuwagiza uongozi wa wizara ya habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kushirikiana pamoja na shirirkisho la mpira wa miguu Zanzibar (ZFF) kueka utaratibu maalum wa kuhakikisha ligi kuu ya Zanzibar pamoja na ligi nyengine zinarejea katika ubora.
“Nataka nizione timu zetu kama vile Malindi, Ujamaa, Small Simba, Kikwajuni na nyenginezo zinakuwa katika kiwango cha ushandani na kuvutia wapenda michezo wote wa Zanzibar. Alisema Mhe. Hemed
Kwa upende wa Sekta ya maja safi na salama Makamu Makamu wa Pili wa Rais alisema serikali kupitia mamlaka ya maji Zanzibar (ZAWA) inaendelea kuchukua hatua za kuondosha kasoro zinazopelekea kutopatikana kwa huduma ya maji safi na salama kwa baadhi ya maneo Unguja na Pemba.
Pia, alieleza serikali ipo katika mkakati wa kutekeleza miradi mikubwa ya maja kwa maslahi ya wananchi wake akitolea mfano kwa mwezi Disemba 2020 hadi mwezi Juni 2021 jumla ya visiama vipya kumi na sita (16) vimechimbwa katika maeneo mbali mbali ili kuwafikishia wananchi huduma hiyo huku akiwataka wananchi kuendelea kuilinda miundombinu kwa lengo la kuiwezesha serikali kufikia malengo ilioyakusudia.
Akigusia suala la makaazi ya wananchi alifafanua kuwa, serikali imedhamiria kujenga nyumba ambazo zitawawezesha wananchi kulipia bei nafuu ikiwa lengo ni kuwawezesha wananchi wa kipato cha chini kumudu bei hiyo.
Alisema pia katika sula la makaazi serikali ya awamu ya nane itaendelea kuzikarabati nyumba zote za serikali sambamba na kujenga nyumba mpya kwa ajili ya makaazi ya viongozi ambapo serikali inaendelea kuzifuatilia nyumba zilizokuwa zinakaliwa na viongozi kwa ngazi ya mawaziri, Makatibu wakuu, wakurugenzi na maafisa wengine ambao ni wastaafu ili kuzirejesha nyumba hizo serikalini.
Kupitia houtuba yake hiyo Mhe. Hemed aliwatanabahisha watumishi wa serikali kuacha mara moja kujihusisha katika masuala yanayopelekea migogoro ya ardhi kwani serikali imekusudia kuchukua hatua za kinidhamu na kisheria dhidi ya wahusika wanaosababisha migogoro hiyo.
“Takwimu zilizopo zinaonesha kwamba kuanzia mwezi Disemba 2020 hadi mwezi Juni 2021 wizara ya ardhi na maendeleo ya makaazi imeskiliza jumla ya migogoro mia mbili na arubaini na mbili (242) kati ya hiyo migogoro (79) imeshapatiwa ufumbuzi.
Makamu wa Pili wa Rais alieleza kuwa, katika kuijenga Zanzibar kupitia uchumi wa Buluu serikali itasimamia na kuunga mkono kwa karibu miradi yote itakayoanzishwa katika sekta hio inayojumuisha uvuvi, utalii, uchimbaji wa mafuta na gesi, michezo ya bahari na usafiri wa baharini kwa lengo la kutoa tija kwa wananchi wake na Taifa kwa ujumla.
Katika kuimarisha huduma za Afya Makamu wa Pili wa Rais alisema serikali itaendelea kuweka miundombinu bora katika sekta ya Afya ikiwemo kuanzisha bima ya Afya, kuongeza vifaa tiba, madawa, kuimarisha mazingira ya kufanyia kazi na kuimarisha maslahi ya wafanyakazi ikijumuisha hospitali ya Mnazi mmoja, Abdalla Mzee na hospitali nyengine pamoja na vituo vya Afya.
Sambamba na hayo, alisisitiza kuwa serikali imeweka mkazo katika suala la tahadhari juu ya mripuko wa maradhi ya Covid 19 ambapo hatua mbali mbali za kudhibiti maradhi hayo zimechukuliwa ikiwemo kuimarisha vituo vya kufanyia vipimo kwa wageni na wenyeji wanaoingia na kutoka Nchini.
“Serikali imedhamiri kuruhusu chanjo ya ugonjwa wa Covid- 19 lakini suala hilo litakuwa ni la hiayari na hakuna mti atakaelazimishwa kuchanjwa bila ya ridhaa yake” Alifafanua Makamu wa Pili wa Rais
Katika kukabiliana na suala la uharibufu wa Mazingira alisema serikali itaendelea kufanya ufuatiliaji wa maeneo mbali mbali yaliopatwa na athari ili kuyarejesha katika yake ya awali yakiwemo maeneo yaliochimbwa mchanga na kifusi kwa upande wa Unguja na Pemba pamoja na maeneo yote yalioingiwa na maji chumvi.
Sambamba na hayo, Mhe. Hemed alieleza bado suala la usafi wa miji bado haliridhishi hivyo alisistiza kuwa serikali kwa kushirikiana na serikali za mikoa, wilaya, halamashauri, mabaraza ya manispaa na mabaraza ya miji itaendelea kusimamia suala la usafi wa miji hususani maeneo ya mijini kwa kuzingatia kuwa Zanzibar ni nchi ya kitalii.
Vile vile, Makamu wa Pili wa Rais alisema serikali imejipanga kutatua changamato ya usafiri wa baharini jambo ambalo linasababisha usumbufu kwa wananchi kwa kukosa usafi wa meli wa uhakika wa kuwavusha katika visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na Dar es Salam, hivyo serikali italichukulia suala kwa uzito wake na inaendelea kulifanyia kazi kwa kuzikodisha meli hizo, kuziuza pamoja na kuzifanyia matengenezo.
“Katika suala hili la usumbufu wa Usafiri tunawaomba wananchi wawe wavumilivu huku serikali ikitendelea na utaratibu wa kutatua changamoto hizo” Alieleza Makamu wa Pili.
Baraza la wawakilishi limeakhirishwa hadi siku ya Jumatano ya tarehe 08 Semptemba, 2021 Saa Tatu kamili za Asubhi.
No comments:
Post a Comment