Habari za Punde

Wananchi wa Kijiji cha Paris Waaswa kutoficha Wahalifu -Mhe Chilo.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Paris kilichopo Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika leo ambapo amewataka kutowaficha wahalifu wanaohatarisha usalama wao.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Na Abubakari Akida,MOHA

Wananchi wa kijiji cha Paris kilichopo Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja Visiwani Zanzibar wametakiwa kutowaficha wahalifu wanaopatikana katika maeneo yao ili kuweza kuishi kwa amani na salama ili lengo la nchi kuendelea kiuchumi litimie.  

Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji hicho kwenye Mkutano wa Hadhara ambapo kabla ajazungumza nao alipata nafasi ya kusikiliza maoni mbalimbali kutoka kwa wananchi hao.

Amewataka wananchi hao kutoyafumbia macho matendo ya uhalifu ikiwemo uuzaji na utumiaji wa dawa za kulevya,matendo ya udhalilishaji,uporaji na wizi

“Kuna wengine wamesema yapo matukio ya kihalifu hapa yanafanyika, watu wanaiba hapa, watu wanatembea uchi, bangi zinauzwa hapa, sasa akitokea mtu anatokea sehemu ya mbali kama mlivyosema  anafanya matendo ya uhalifu basi mripoti kwa Jeshi la Polisi,mkishajua huyu ndio muuza unga maarufu hata mimi niambieni nitawatauma askari wangu waje wamshughulikie,msimpige wala msichukue sheria mkononi chukueni hatua za kinidhamu na kisheria sio mumpige mtakuja kutengeneza balaa linguine” alisema Naibu Waziri Chilo

Awali mkazi wa Kijiji hicho Said Mpangaleni akizungumza  katika mkutano huo amesema kuwepo kwa uhalifu uliokithiri katika Kijiji chao imepelekea  kudumaa kwa shughuli za kimaendeleo watu wakihofia usalama wao

“Hapa pana genge la uuzaji na utumiaji dawa za kulevya na ndio linaratibu uhalifu wote katika Kijiji hiki,mtu akishakula maunga yake kinachofatia ni uhalifu tu kwa kweli tumekua tukiishi kwa hofu,bora sisi wanaume tuna afadhali lakini dada zetu wanaporwa mchana kweupe,serikali itusaidie kwenye hili kwani kwa hali hii huo uchumi tunaoambiwa hatuwezi kuupata hali huku ni tete” alisema Said

Wakitoa neno la shukrani baada ya mkutano huo wawakilishi wa wananchi hao wameiomba serikali kufungua kituo cha polisi katika maeneo hayo kwani itarahisisha udhibiti wa uhalifu katika Kijiji chao hali itakayopelekea kustawi kwa amani huku pia wakiomba kuongezwa kwa askari wa ulinzi shirikishi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.