Habari za Punde

Innaa Lillaahi Wainaa ilayhi Raajiuun : Waziri wa zamani wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar Suleiman Othman Nyanga Amefariki leo. Nimjuavyo kidogo* : *Suleiman Othman Nyanga*


Na Ally Saleh* *Alberto* 
Nilimuwahi Suleiman Othman Nyanga katika usakataji wake wa soka alipokuwa tayari amepata umaarufu na anaanza anza. 

Najua alikuwa ni sehemu ya wachezaji waliopata bahati kupitia mfumo wa ligi za watoto miaka ya 60 ukiongozwa na magwiji kama Maalim Hija Saleh, Maalim Ghussun Hilal na Maalim Rajab Mzee.

Mimi nilianza kumuona wakati wa michezo ya maskuli ambapo miaka ya 60 na 70 kiwango cha riadha na soka kilikuwa juu kutokana na mchango wa Serikali katika michezo.

Nilimuona Nyanga katika vikosi vya maskuli, baadae kombaini ya vijana, timu ya Miembeni, timu ya taifa ya Zanzibar na pia alicheza Taifa Stars.

Nyanga anatokea familia ya soka ambapo kama nakumbuka uzuri kaka zake wawili walikuwa wa kudumu katika kikosi cha Miembeni siku hizo ikiitwa Kwalalumpa.

Nakumbuka kumuona Miembeni na wachezaji kama golikipa Shaibu, Chunda, Ambar, Malik na Salhina kwenye mechi za Mao Tse Tung na sasa Mao Dze Dung. 

Kwenye timu ya taifa ya Zanzibar Nyanga alikuwa na kina Mansab, Kishore, Jeff, Dingo, Mustafa Kassim. Katembo, Pandu, Shaffi, Juma Komwae, Shah na Nassor Mashoto kutaja baadhi yao. 

Kama niko sawa Nyanga alikuwa katika kikosi kilocheza Challenge Cup ilofanyika Zanzibar miaka ya mwanzo ya 70 na Zanzibar ikaweka rekodi ya kuifunga Kenya 3-1.

Nilishuhudia mechi hio nikitoka nyumbani Shangani kwa miguu na kudowea baskeli wakati wa kurudi. 

Nilipata kitita cha tiketi  za mechi zote za Challenge kutoka kwa mzee wangu Sk Abdulrahman Ali maana siku hizo wafanyakazi wote walipewa tiketi kwa lazima na kukatwa kwenye mishahara yao. 

Nyanga alikuwa ni toleo jipya kwa Zanzibar kwa sababu ya staili yake ya uchezaji. Alikuwa na nguvu, mbio, na mashuti makali... Na hakika mashuti yake yakilenga. Alikuwa labda akifanana na Revelino wa Brazil ya 1970 kule Mexico. 

Sidhani kama kuna rekodi alifunga magoli mangapi au alisaidia mangapi, lakini ni hakika Miembeni ilifaidika na mchango wake. 

Na wengi  wa zamani tunadhani kipindi cha mpira cha Nyanga na wenziwe 70 mpaka 80 na mwanzo 90 ndio kilikuwa bora zaidi kwa Zanzibar. 

Ila Nyanga alipata tatizo mapema sana liloathiri kiwango chake... Bega lake. Alikuwa na tatizo la kutoka bega wakati akiwa uwanjani. Japo mwenye akiweza kulitia. Ila ikawa ni kikwazo kwake kiuchezaji

Nyanga aliwahi kuwa kocha wa timu ya Miembeni ila sina hakika kama akipata matokeo mazuri sana. Miembeni imewahi mara moja tu kuchukua ubingwa wa Zanzibar sina hakika kama yeye alikuwa kocha. 

Ila najua alikuwa mfadhili mzuri sana sana wa Miembeni wakati huo na Bwana Muhammed Hashim aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano na Muwakilishi. 

Inawezekana kipindi hicho cha ufadhili wake ndio Mimbeni ilipata ubingwa japo wengine waliuita ni wa Mahakamani dhidi ya Small Simba. 

Ni msiba mkubwa kwa Miembeni FC popote ilipo hivi sasa na ni hasara kubwa timu ya jina kama hii kupotea kwenye ramani ya soka. 

Leo Miembeni haipo kama mzishi mkuu wa Suleiman Othman Nyanga kimpira, mmoja ya wachezaji niliowaona na naamini wangeweza kucheza ligi yoyote duniani. 

Alikuwa namba 10 ya uhakika ambayo peke yake aliweza kubadilisha matokea japo alikuwa mtu mkimya lakini alikuwa na utani sana. 

Nyanga aliingia kwenye siasa na hata kuwa Waziri wa Fedha wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Alikuwa rafiki mzuri wa wengi na alikuwa mtu wa msaada na mkarimu kupindukia. 

Kwaheri Nyanga, tangulia kwenye safari ya wote.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.