Habari za Punde

Rais Dk Hussein Mwinyi afurahishwa na juhudi za Benki ya CRDB kufungua matawi Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na kuhutubia katika hafla ya uzinduzi wa Tawi la Benki ya CRDB Michezani Mall Huduma ya Islamic Banking Michezani Mall Jijini Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi  ametoa pongezi kwa uongozi wa benki ya CRDB kwa kumuunga mkono katika kutekeleza yale mambo aliyowaahidi wananchi tangu Serikali ya Awamu ya Nane ilipoingia madarakani.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo katika uzinduzi wa Tawi jipya la Benki ya Kiislamu (Al Barakah) la CRDB, alilolifungua katika jengo  la Michenzani Mall, Jijini Zanzibar.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa huo ni mfano wa kuigwa na taasisi nyengine za fedha kwani amefarajika sana kuona juhudi za Benki hiyo katika utekelezaji wa sera na mipango ya Serikali katika kuendeleza uchumi wa buluu.

Alisema kuwa bado anazikumbuka ahadi ilizotoa benki hiyo mnamo Novemba 28,2020 katika ukumbi wa Hoteli ya Verde wakati benki hiyo ilipoandaa mkutano maalum kwa viongozi waandamizi na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ambapo tokea wakati huo benki hiyo imekuwa ikiyatekeleza kwa vitendo mambo waliyoyaahidi.

Hivyo, Rais Dk. Mwinyi na yeye aliiahidi benki hiyo kwamba Serikali anayoiongoza itaendelea kutoa ushirikiano unaohitajika ili benki hiyo iweze kuendesha shughuli zake kwa ufanisi zaidi na kuweza kutimiza matumaini na matarajio ya wateja wao.

Alisema kuwa njia ya pekee ya kutekeleza dhamira ya benki hiyo ni kuhakikisha kwamba huduma za fedha zinatolewa na taasisi binafsi na za Serikali zinazokidhi viwango na mahitaji halisi ya wawekezaji, watalii na wananchi na kuendelea kufungua matawi ya kisasa katika miji na vijiji mbali mbali vya Unguja na Pemba.

Alisisitiza kwamba huduma za benki ndio msingi katika kukuza uwekezaji na kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi yaliyolengwa kufanywa na Serikali ya Awamu ya Nane.

Aidha, alisema kuwa ili uchumi uweze kujengeka na kuimarisha hali ya maisha ya wananchi basi kwanza ni lazima pawepo na mzunguko wa fedha kupitia Benki zilizopo nchini ambapo pia ni vyema benki nazo lazima ziwe na mifumo mizuri ya kukusanya na kuweka akiba za wateja pamoja na kukopesha amana hizo kwa misingi ya uadilifu.

Aliongeza kuwa hivi karibuni katika hotuba yake ya kutimiza mwaka mmoja akiwa madarakani alitangaza mipango na mikakati ya Serikali ya kuchochea uchumi kwa kuingiza jumla ya TZS bilioni 460 katika uchumi wa Zanzibar hatua iliyolenga kuimarisha mzunguko wa fedha na kuondoa mdororo uliopo wa shughuli mbali mbali za kiuchumi kutokana na kuzuka kwa maradhi ya UVIKO 19.

Dk. Mwinyi alizihimiza benki na taasisi za fedha zote zilizopo Zanzibar kuwa na mipango imara ya kutumia fursa zitakazojitokeza katika utekelezaji wa mipango hiyo, kwa kufanya kazi kwa karibu na taasisi za Serikali pamoja na Wajasiriamali, ili kwa pamoja kuweza kutekeleza mipango iliyopangwa na kuipongeza benki hiyo pamoja na BOT kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango kwa kufanya mijadala juu ya fedha hizo.

“Nimefurahi kuona juhudi zinazochukuliwa na benki ya CRDB za kufungua matawi kwa ajili ya kutoa huduma ambazo zinafuata misingi na taratibu za Kiislamu (Islamic Banking) ambayo imepewa jina la Al Barakah Banking, bila shaka ubunifu na utayari huo unaungwa mkono na wananchi wengi wa Unguja na Pemba, hasa ikizingatiwa kwamba huduma hizo zinapendwa sana na wananchi wengi wa Zanzibar”,alisisitiza Dk. Mwinyi.

Pamoja na hayo, Dk. Mwinyi alieleza kwamba licha ya mafanikio yanayopatikana lakini bado kuna malalamiko ya msingi ambayo benki zilizopo ziyafanyie kazi ikiwa ni pamoja na kiwango cha riba kinachotozwa na benki za hapa nchini ni kikubwa, mikopo kutolewa kwa masharti magumu na ya muda mfupi,huduma za benki kupatikana zaidi mjini, msongamano wa wateja hasa mwisho wa mwezi katika benki na viwanja vya ndege.

Pia, Dk. Mwinyi aliwahimiza wafanyakazi wanaotoa huduma wahakikishe wanazingatia misingi ya uadilifu,wawe wakarimu na wenye lugha nzuri kwa wateja huku akiwahimiza wananchi nao kwa upande wao kuachana na utamaduni wa kuweka fedha majumbani na badala yake wajenge utamaduni wa kuweka fedha benki ili ziweze kuimarisha uchumi.

Nae Waziri wa Fedha na Mipango Jamal Kassim Ali aliitaka benki ya CRDB pamoja na benki nyengine hapa nchini kuzitumia fursa zilizowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kukuza uchumi ukiwemo uchumi wa Buluu.

Naibu Gavana wa BOT Bernerd Kibesse kwa upande wake alieleza jinsi benki hiyo inavyotoa misaada na mashirikiano kwa benki za hapa nchini na kuipongeza CRDB kwa kuwa na matawi mengi sambamba na kuanzisha huduma hizo za kibenki hapa Zanzibar.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Mussa Nsekela alieleza mipango na mikakati ya benki hiyo kwa Zanzibar na Tanzania nzima kwa jumla ambapo alisema kuwa huduma hizo za benki ya Kiislamu zitatolewa na benki hiyo kwa Tanzania nzima.

Mapema Rashid Rashid mkuu wa Kitengo cha Benki ya Al Mubarakah cha CRDB alieleza mikakati na mipango ya benki hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa huduma hizo Tanzania nzima ikiwemo huduma ya kuweka fedha kwa ajili ya Hijja.

Imetayarishwa na Kitengo cha Habari,

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.